Advertisements

Wednesday, January 30, 2013

wazanzibari watakiwa kupanga uzazi


Salma Said, Zanzibar. Januari 30. 2013.

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imewasisitiza Wazanzibari kutumia uzazi wa mpango ili kupunguza idadi ya watu ambao imekuwa ikiongezeka siku hadi siku katika visiwa vya Zanzibar.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi wakati akiufunga Mkutano wa Kumi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar  katika ukumbi wa Baraza hilo uliopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Kwa mujibu wa Sensa ya 2002, Zanzibar ilikuwa na watu wapatao 980,000 na katika Sensa iliyofanywa mwaka jana 2012, ambapo ni miaka kumi baadae, Zanzibar imekuwa na idadi ya watu 1,303,560 jambo ambalo Baloazi Seif anasema serikali inapaswa kutoa elimu ya uzazi wa mpango kwa wananchi wake.

Mheshimiwa Spika ongezeko la watu 323,560.  Hili ni ongezeko kubwa sana.  Hatuna budi sasa tufanye maarifa ya kupunguza kasi ya kuzaliana ili watoto wetu tuwalee vizuri zaidi,” alisema Balozi Seif mbele ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Balozi Seif alisema idadi hiyo ya watu iliyoongezeka Zanzibar, Serikali haina budi kuwa na mipango madhubuti ya kudhibiti ongezeko la kasi la idadi hiyo ya watu na hivyo kushauri kuongeza bidii katika kufanya kazi na kuzalisha kwa wingi bidhaa zitakazokidhi mahitaji ya watu wake ndani na kupata ziada ya kuuza nje ya nchi.

Balozi Seif alisema serikali inahitajika kuimarisha huduma za jamii, ikiwemo elimu, afya, upatikanaji wa maji safi na salama na makaazi huku akiwasisitiza viongozi wote katika ngazi zote na  wananchi kwa ujumla wazidishe ushirikiano na kuzidisha ari ya kujituma na kuwajibika zaidi katika maeneo yao ya kazi katika sekta ya umma na sekta binafsi.

Alisema wakati wa maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar jumla ya miradi 53 ya maendeleo iliwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa ambayo yenye thamani ya wastani wa shilingi bilioni 97 katika sekta ya elimu, maji safi na salama, afya, kilimo, uvuvi na miundombinu ya habari, mawasiliano na barabara.

Hii ni hatua kubwa ya maendeleo ambayo nchi yetu imepiga katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Nachukua nafasi hii kuwashukuru kwa dhati viongozi katika ngazi zote na wananchi wote kwa kushirikiana katika kufanikisha sherehe zetu hizi adhimu ambazo zilifana sana,” alisema.

Balozi Seif alisema Serikali itaendelea na jitihada za kuimarisha sekta za Kiuchumi na Ustawi wa Jamii lengo kuu likiwa lile lile la kukuza uchumi na kupunguza umaskini miongoni mwa wananachi walio wengio hapa nchini.

Alisema jitihada hizo muhimu zitafanikiwa vyema endapo wananchi wote kwa kushirikiana na viongozi wao watakubali kuwajibika kikamilifu  na baadhi yao kuacha tabia za kuchafua mazingira sambamba na uharibifu wa miundo mbinu ambayo Serikali Kuu tayari imeshaiweka.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa  ikiongozwa na Rais wake, Dk. Ali Mohammed Shein inafanya kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.

“ Katika kufanikisha hayo Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya elimu, afya, biashara na viwanda, kilimo, mifugo na uvuvi, miundo mbinu na kuhakikisha wananchi wote mijini na vijijini wanapata maji safi na salama kwa kuimarisha  afya zao,” alifafanua Balozi Seif.

Akizungumzia suala la sheria zinazotungwa na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa nia ya kuwatumikia wananchi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliwanasihi watekelezaji wa sheria hizo wazisimamie na kuhakikisha  kuwa zinatekelezwa ipasavyo bila ya kumuonea haya au aibu mtu yeyote atakayezikiuka sheria hizo.

Alisema Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamekuwa wakilalamikia kuwa sheria nyingi zimetungwa lakini  kumekuwa na udhaifu wa kusimamia utekelezaji wake. Aliitolea mfano sheria ya usimamizi wa usalama Bara ambayo jamii imekuwa ikishuhudia waendesha baskeli wanatumia vyombo vyao hasa usiku bila ya taa wakati baadhi ya madereva  huendesha gari bila ya nambari ambapo haijuilikani madhumuni yao kufanya hivyo.

Balozi Seif aliipongeza Tume Teule ya Baraza la Wawakilishi iliyoundwa kuchunguza utendaji wa shirika la Umeme Zanzibar na Kamati Teule ya kuchuguza utendaji wa Baraza la Manispaa kwa umakini wao na kufanya uchunguzi wa kina kuhusu utendaji katika taasisi hizo mbili.

Alisema Serikali imezipokea ripoti hizo za Kamati Teule zilizowasilishwa katika Baraza la Wawakilishi na itazifanyia kazi taarifa hizo pamoja na mapendekezo yake kwa umakini  mkubwa na kuchukuwa hatua kadri itakavyoonekana inafaa.

Balozi Seif aliwahakikishia wajumbe wa Baraza hilo kwamba wale wote waliotajwa kwenye ripoti hizo watashughulikiwa ipasavyo kwa kuzingatia haki na Utawala Bora kama baadhi ya wajumbe hao walivyoshauri.

Kuhusu suala la ununuzi wa meli kubwa kwa ajili ya usafiri wa uhakika wa wananachi wa Zanzibar na mwambao wa Afrika Mashariki, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema  Serikali  inatarajiwa kutiliana saini mkataba   na Kampuni ya  Damen kutoka nchini Uholanzi  kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya ya abiria na mizigo.

Balozi Seif alisema meli hiyo itakayokuwa na uwezo wa kuchukuwa abiria 1,200 na tani 200 za mizigo inatarajiwa kuchukuwa miezi 18 utengenezaji wake  mara baada ya mkataba huo kutiwa saini.
“ Wananchi wa Zanzibar wategemee  kama mambo yote yatakwenda sawa, kupata meli mpya mnamo robo ya mwisho wa mwaka 2014, ingawa inawezekana ikawa zaidi kabla ya hapo,” alifafanua Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi  walijadili na kupitisha miswaada minne ya sheria pamoja na mawaziri kujibu  maswali ya wajumbe wa Baraza hilo yapatayo 72. Miswaada hiyo ni  mswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya ruzuku kwa vyama vya siasa nambari 6 ya mwaka 1997 pamoja na  mswada wa sheria ya marekebisho ya usafiri nambari 5 ya mwaka 2006.

Mengine ni mswada  wa sheria ya kuanzisha shirika la Utangazaji Zanzibar, kazi, majukumu na utawala wake  pamoja na mambo mengine yanayohusiana na hayo na Mswada wa sheria ya kuanzishwa kwa Shirika la Meli Zanzibar kazi, uwezo na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa hadi Jumatano ya  Aprili 3, 2013.

No comments: