ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 23, 2013

Wazee Mtwara waibukia D'Salaam kupigania gesi

Wazee wa Mtwara wakishangaa kupigwa picha mara baada ya kuwasili nje ya Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo...
Wazee wa Mtwara wakijipanga kuingia katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo...
Wanahabari wakifuatilia mkutano huo.
Katibu wa Wazee wa Mtwara Bw. Seleman Madem ambaye aliongozana na Wazee wa Mtwara kuja jijini Dar es Salaam kuongea na vyombo vya habari juu ya sakata la gesi. 

Wazee hao ambao wametoka katika umoja unaoshirikisha vyama mbali mbali vyasiasa ikiwemo ABC, APP NA MAENDELEO, CHADEMA, DP, NCCR MAGEUZI, SAU, TLP na UDP. Bw. Mademu alisema kuwa wananchi wa Mtwara wanadai kuwa pamoja na yote hayo kufanyika wao mpaka sasa hawajashirikishwa. Wanamtwara wanasema kuwa hawakuwa na dhamira mbaya ya kuandamana bali ilikuwa ni kuishinikiza serikali juu ya sakata la gesi.

Pia waliviasa vyama vya siasa kujichukulia umaarufu binafsi kwa ajenda ya Gesi, ambao kauli mbiu yao unasema, 'Gesi kwanza Vyama baadae'. Pia walipinga vyombo vya siasa kuripoti vibaya suala la Mheshimiwa Jemsi Mbatia kuwa hakushushwa jukwaani na wanasema mkutano uliisha kwa amani.
kwa picha zaidi bofya read more
Mwenyekiti wa CHAUMA mkoa wa Mtwara Bibi Fatuma Selemani ambaye alikuwa ni mmoja ya wazee waliokuja kuongea na waandishi jijini Dar es Salaam akitilia mkazo suala la Gesi. Wazee hao walikuja jijini Dar es Salaam kuongea na waandishi wa Habari ili kuweza kuishinikiza serikali isiisafirishe gesi ya Mtwara kuja Dar es Salaam. 

Jambo ambalo lililoshangaza baada ya Mtandao wa Kajunason Blog kufanya uchunguzi wake ilibaini kuwa wazee hao waliletwa na Chama cha NCCR Mageuzi kinachoongozwa na Mh. James Mbatia kuja jijini Dar es Salaam kumsafisha. Kwa mujibu wa barua iliyopatikana ndani ya ofisi za ukumbi huo zilionyesha kuwa Ukumbi huo ulikodiwa na Chama hicho jambo lililoonyesha wazi kuwa wazee hao waliletwa na chama hicho japo wenyewe walikataa katu katu kuwa wameuza kuku, mbuzi zao kuja jijini Dar kuzungumzia sakata la gesi jambo ambalo si kweli. Kwa vile mwanzo wazee hao waliongelea swala la gesi na kupinga kuwa Mh. Mbatia eti hakupigwa wala kufanyiwa fujo mara baada ya kwenda mjini Mtwara kufanya mikutano yake ya ndani.
Waandishi wa habari wakifuatilia kwa makini. Kama ulipitwa na Sakata la Mheshimiwa James Mbatia huko Mtwara 
Picha kwa hisani ya Kajunason Blog

Sakata la kugundulika kwa gesi mkoani Mtwara, limezidi kupamba moto baada ya wazee wanaodai wanatoka mkoani humo kuibuka jijini Dar es Salaam na kutoa tamko wakiitaka serikali kuacha mara moja mpango wake wa kuisafirisha gesi kwenda Dar es Salaam.

Badala yake, wazee hao wanaodai kutoka Manispaa ya Mtwara-Mikindani, wametaka kijengwe kituo cha kusafishia gesi hiyo mkoani humo.

Katika tamko lao lilisomwa mbele ya mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana na Suleiman Mademu, wazee hao walisema wanawawakilisha wananchi wa mkoa huo pamoja na vyama tisa vya siasa nchini.

Vyama hivyo ni ADC, APPT-Maendeleo, Chadema, DP, NCCR-Mageuzi, Sau, TLP na UDP.

Mademu alisema serikali inafanya kinyume cha ilivyowaahidi wananchi wa Mtwara huko nyuma wakati gesi hiyo ilipogundulika.

Alisema katika ahadi hiyo, serikali ilisema wananchi wa Mtwara watakuwa wa kwanza kunufaika na gesi hiyo kwa kujenga kituo cha kuisafisha.

Kutokana na hali hiyo, aliunga mkono hatua ya wananchi wa Mtwara kufanya maandamano Desemba 27, mwaka jana kupinga gesi hiyo kusafirishwa kwenda Dar es Salaam.

Alisema maandamano hayo yalifuata taratibu za nchi na kwamba, hatua hiyo ni moja ya njia za kufikisha vilio na matatizo yanayowakabili wananchi.

Alisema katika kufanya maandamano hayo, hawakuwa na dhamira mbaya kwani maandamano yalikuwa ya amani na yalilenga kufikisha kilio chao serikalini.

“Tunaomba ieleweke hivyo na tunahitaji kuelewa tena kwa vitendo ni namna gani gesi iliyogunduliwa itatunufaisha kwanza Wanamtwara kabla ya kuwanufaisha watu wa maeneo mengine nchini. Hili ndilo swali letu la msingi,” alisema Mademu na kuongeza:

“Wanamtwara hatupendi kuendelea kuelezwa kwamba tutanufaika na gesi iliyogunduliwa kwa kuahidiwa viwanda kama ambavyo imekuwa desturi ya serikali yetu.”

Alisema wanachohitaji ni vitendo kutawala badala ya ahadi kama ilivyozoeleka nchini. Mademu alisema wanazo rekodi mbalimbali za kupewa ahadi ambazo hazitekelezeki.

Alizitaja ahadi hizo kuwa zinahusu kujengewa barabara, kuwekewa umeme, kuimarishwa kwa bandari, mikopo kwa ajili ya ujasiriamali na viwanda vidogo kwa ajili ya kubangua korosho.

“Hivyo basi, sisi tukiwa sehemu ya wazee wa Mtwara tunaitaka serikali ifanye mambo yafuatayo: Wanamtwara tunahitaji kuona kituo cha kusafisha gesi kinajengwa mkoani Mtwara kwani ipo bandari yenye kina kirefu itakayotumika katika mchakato mzima wa biashara hii ya gesi. Hii itasaidia kuipanua, kuitangaza na kuitumia ipasavyo bandari ya Mtwara hata ikiwezekana kutumiwa na nchi za jirani kama vile Msumbiji,” alisema Mademu.

Pia alitaka viwanda kama vile vya mbolea, saruji walivyoahidiwa waone kwa vitendo mchakato wa kuvijenga akisema hatua hiyo itawapa matumaini yasiyokuwa na shaka kuhusu kupata ajira, kukuza uchumi kwa maslahi ya pamoja.

Vilevile, aliitaka serikali iratibu mchakato mzima wa matumizi ya rasilimali gesi kwa kuishirikisha mikoa ya Kusini kwa hatua zote na kwa uwazi na kituo cha kufua umeme kijengwe Mtwara.

Pia alivitaka vyama vya siasa visijitafutie umaarufu binafsi kwa ajenda hiyo ya gesi na badala yake vishirikiane kwa njia ya kuleta maendeleo yao, kwani kaulimbiu yao ni “gesi kwanza vyama baadaye.”

Sakata la kugomea ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi hiyo liliibuka baada ya wananchi wa mkoa huo wakishirikiana na baadhi ya vyama vya siasa kufanya maandamano, mkoani humo, Desemba 27, mwaka jana, kupinga mpango huo wa serikali.

Maandamano hayo yalifuatiwa na kauli zilizotolewa kwa nyakati tofauti na viongozi wa serikali, wabunge, vyama vya siasa, baadhi wakiunga mkono msimamo wa wananchi hao na wengine wakiupinga.

Waliotoa kauli za kuwaunga mkono wakazi hao ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe; Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika; Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnein Murji.

Waliotoa kauli ya kupinga hatua ya wananchi hao kwa hoja kuwa gesi ni mali ya Watanzania wote ni Rais Jakaya Kikwete; Rais mstaafu, Benjamin Mkapa; Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia.

Wiki iliyopita, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Wilman Ndile, alisema suala la gesi kwa sasa ni tishio kubwa kwa amani na utulivu kwa wakazi wa Mkoa wa Mtwara.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka viongozi wa asasi mbalimbali mkoani humo kutoa elimu kuhusu gesi kwa wakazi wake ili kudumisha hali ya amani na utulivu ambavyo vinaelekea kutoweka siku hadi siku.

MMOJA MBARONI
Jeshi la Polisi mkoani Lindi linamshikilia kwa mahojiano mkazi wa Kata ya Vigaeni, Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Hamisi Juta Selemani (32), kwa tuhuma za kuvaa vazi lenye maandishi yanayodaiwa kuashiria vitisho dhidi ya watendaji wa serikali.

Habari kutoka kwa watu walioshuhudia tukio hilo na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga, zinaeleza kwamba Juta alikamatwa Januari 19, mwaka huu saa 12:30 jioni katika eneo la Bwalo la Polisi.

Baadhi ya watu hao ambao hawakupenda majina yao kutajwa, wameliambia gazeti hili kwamba siku hiyo, Juta akiwa amevalia kanzu nyeupe yenye maandishi yasemayo “gesi kwanza uhai baadaye,” alikamatwa eneo hilo akiwa kwenye baa.

Kamanda Mwakajinga alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, alithibitisha kukamatwa kwa kijana huyo na kueleza kwamba wanamshikilia kwa mahojiano kutokana na kanzu aliyokuwa ameivaa siku hiyo kuwa na maandishi pamoja na picha zinazoashiria vitisho dhidi ya watendaji wa serikali.

Mwakajinga alisema kanzu hiyo ina maandishi yasemayo “gesi kwanza uhai baadaye” na picha zinazoonyesha mtu ameshika mshale na mwingine ameshika panga mkononi.

“Kanzu aliyoivaa ilikuwa na maandishi yasemayo hivyo pamoja na picha inaonyesha mtu kashika mshale unamchoma mwingine na mwingine mkononi ameshikilia panga. Hivi akishasema gesi kwanza uhai baadaye anataka kutuambia nini?” alihoji Kamanda Mwakajinga.

Kamanda huyo alisema kijana huyo atafikishwa mahakamani baada ya taratibu kukamilika ikiwamo Mwanasheria wa Serikali kutoa baraka.

Imeandikwa na Samson Fridolin na Enles Mbegalo, Dar na Said Hamdani, Lindi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: