Naibu meya wa Manispaa ya Iringa Gravas Ndaki akishangaa ajali ya karne yenye maajabu makubwa kwa mkoa wa Iringa ,ajali iliyotokea usiku wa jana eneo la Hoteli ya kati (makosa) au CRDB ya zamani katika barabara ya Iringa -Dodoma, baada ya gari aina ya RAV 4 yenye namba T 319 AFL (juu) kuhama njia na kuigonga Taxi yenye namba za usajili T 510 AYU yenye hakuna majeruhi wala aliyepoteza maisha.
Ramadhani Mrisho maarufu kwa jina la Makosa ambaye ana jina kubwa katika masikio ya wakazi wa mkoa wa Iringa na Tanzania kutokana na jinsi alivyokuwa maarufu katika mji wa Iringa kwa kumiliki mali mbalimbali na kutoa misaada kwa jamii ameibuka katika eneo la ajali na kupinga ulevi kwa madereva.
Dereva wa Taxi yenye namba T 510 AYU Bw Kelvin Kaduma akitengeneza gari yake baada ya kutolewa eneo la ajali.
AJALI mbaya imetokea mjini Iringa eneo la Makosa ama CRDB ya zamani kwenye barabara kuu ya Iringa - Dodoma baada ya gari aina ya RAV 4 yenye namba T 319 AFL kuhama njia na kuigonga Taxi yenye namba za usajili T 510 AYU iliyokuwa ikiendeshwa na dereva Kelvin Kaduma.
Ajali hiyo imetokea majira ya saa 10 usiku wa jana wakati dereva wa RAV4 hiyo akitoka maeneo ya mji wa Iringa akielekea mwelekeo ambao wakazi wa mji wa Iringa wamekuwa wakipata starehe zao eneo la Dragon Bar na Club Twistas kuendelea kumalizia starehe za mwisho wa wiki.
Mashuhuda wa tukio hilo wamemueleza mwandishi wa habari hizi eneo la tukio kuwa gari hiyo aina ya RAV 4 ilikuwa katika mwendo mkali mfano wa gari lililopo katika mashindano na hivyo dereva wake kushindwa kukata kona ya mnara wa Manispaa ya Iringa na hivyo kugonga ukuta wa barabara hiyo kabla ya kuhama na kuigonga Taxi hiyo kwa kuipanda juu.
Hata hivyo mashuhuda hao walisema kuwa dereva huyo wa RAV 4 alikuwa anaonekana kulewa zaidi kutokana na mazingira ambayo alikuwa akionekana kuwa ni mtu ambae amepata pombe kiasi.
Kwa upande wake dereva aliyegongwa na gari aina ya RAV 4 yenye namba T 319 AFL Bw Kelvin kaduma ambae alikuwa akiendesha Taxi yenye namba T 510 AYU alisema kuwa alishuhudia gari hilo RAV 4 likija kwa mwendo wa kasi na ndipo alipoamua kusimama ili kushuhudia na ghafla alijikuta akifunikwa na RAV 4 hiyo.
Alisema kuwa RAV 4 hiyo iliruka ukingo wa barabara ambao una michongoma na kujengwa kwa sementi na kutua juu ya Taxi yake na kushindwa kuendelea na safari na kuwa iwapo asingesimama kuona mtiti wa gari hilo basi dereva huyo wa RAV4 angekufa kwa kugonga nyumba iliyopo jirani ambayo ina hoteli ya Hast Tast.
(Picha Zote na Francis Godwin)Na Francis Godwin, Iringa
No comments:
Post a Comment