Tuesday, February 26, 2013

Jamhuri yafunga ushahidi kesi ya Ponda

Upande wa Jamhuri katika kesi inayomkabili Sheikh Ponda Issa Ponda (54) na wenzake 49  ya kula njama, kuingia, kujimilikisha ardhi kwa jinai, wizi wa mali ya Sh. milioni 59.6 umefunga ushahidi wake baada ya kuita mashahidi 17 kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.
Kabla ya kufunga ushahidi huo mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa, shahidi wa 17 wa Jamhuri, Kostebo Ismail, alidai kuwa mshtakiwa Faisal alipotoa maelezo polisi alieleza kwamba alisikia tangazo kupitia redio Imani kiwanja cha Marcas kimevamiwa.
Shahidi huyo alitoa ushahidi wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam na kudai kuwa kwa mujibu wa mshtakiwa huyo, tangazo hilo lilisema chini ya usimamizi wa Sheikh Ponda wanatakiwa wakaweke nguvu ili wajenge msikiti kwa kuwa kiwanja hicho kilichopo Chang’ombe siyo cha Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), bali ni cha waislamu wote nchini.
Naye shahidi wa 16, Sajini Taji Amoss (54), alidai kuwa alimhoji mshtakiwa Hussein Haji ambaye alieleza kupokea wito kutoka kwa Sheikh Ponda kwamba wakafanye usafi katika kiwanja cha Marcas.
Katika kesi hiyo, Ponda na wenzake  wanakabiliwa na  mashtaka manne, likiwamo la wizi wa mali yenye thamani ya Sh 59.6 milioni, uchochezi na kuingia kwa jinai katika ardhi inayomilikiwa na kampuni ya Agritanza Ltd kwa nia ya kujimilika  isivyo halali.
CHANZO: NIPASHE

No comments: