Tuesday, February 5, 2013

Kigamboni yawagonganisha Tibaijuka, madiwani Temeke

BARAZA la Madiwani katika Manispaa ya Temeke, wameilalamikia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutowashirikisha wao wala halamashauri kwa ujumla katika ujenzi wa Mji Mpya wa Kigamboni.

Madiwani walisema hayo katika kikao cha maendeleo ya wilaya hiyo kilichofanyika katika Manispaa hiyo.
Katika kikao hicho,Diwani wa Kata ya Kurasini Winfrey Kimati aliibuka na hoja juu ya mradi wa ujenzi wa Kigamboni, ambapo aliilaumu wizara hiyo kwa kutokuzingatia kanuni maalumu.
Kimati alisema wizara  haikushirikiana na Halmashauri ya Temeke na badala yake iliwahusisha madiwani wanne kutoka kata tofauti za Kigamboni. Aliongeza kuwa jambo hilo linashangaza na kuhoji ni kwanini wizara hiyo iwahusishe madiwani hao bila kuishirikisha halmashauri kwa ujumla kwa kuwa madiwani wote wapo chini ya halmashauri hiyo.
“Tunahitaji kikao maalumu na wizara juu ya utaratibu maalumu kuhusiana na ujenzi huo na huyo anayewapeleka madiwani wa kata ina maana hajui kama wapo kwenye halmashauri? Aliuliza Kimati.
Kwa upande wake,Diwani wa Viti Maalumu, Amina Khatibu alisema  suala la Kigamboni liangaliwe kwa umakini kwa kuwa matatizo yakianza kutokea watakaoanza kuathirika ni madiwani kwa kuwa wao wapo karibu na wananchi.
``Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ichukue tahadhari mapema yasije yakatokea kama ya Mtwara, hatutaki Kigamboni kuwa uwanja wa vita, taratibu juu ya ujenzi huo ni vema zikawekwa wazi.
Aliongeza kuwa ni vyema madiwani wakaelimishwa juu ya taratibu za ujenzi huo,ili iwe rahisi kuwaelezea wananchi kwa kuwa wao wapo nao karibu hivyo itakuwa ni rahisi kuwafikishia ujumbe.
Madiwani hao walisema wasiwasi wao upo juu ya wananchi kwa kuwa wengi wao bado hawana uelewa mzuri juu ya hatma yao mara ujenzi huo utakapoanza, hivyo ni vyema wizara ikakutana na halmashauri ili iweze kuwafafanulia suala hilo.
Diwani wa Kata ya Makangarawe, Victor Mwakasendile alisema tatizo ni ushirikishwaji na kusisitiza kuwa hawaukatai mradi huo kwa kuwa wao ni madiwani wa wilaya hiyo na ujenzi unafanyika katika wilaya husika.
Mbali na hayo walisema kuna taarifa kuwa madiwani hao wa kata  zilizopo Kigamboni wanaenda Dodoma kuongea na Profesa Anna Tibaijuka, licha ya kuwa hawafahamu wanaenda kuongea naye nini, jambo hilo lilizidi kuwashanganza madiwani hao iweje waonane na Waziri bila Halmashauri kufahamu.
Hata hivyo madiwani hao walifikia muafaka wa kumuandikia barua Tibaijuka ili waweze kuonana naye mara atakapotoka bungeni jambo ambalo liliungwa mkono na Mkurugenzi wa manispaa hiyo.
Tibaijuka akijibu hoja hizo kupitia gazeti hili, aliwatuhumu madiwani hao kwamba waliwafukuza watendaji wake kwenye kikao.
Alisema kuhusu kuwashirikisha walijaribu sana kuwashirikisha lakini waliwafukuza watendaji wake. “Tumewashirikisha kadri walivyokubali kutusikiliza’ alisema Tibaijuka.
Mwananchi

No comments: