Friday, February 22, 2013

Msafara wa Naibu Waziri wasababisha ajali

Naibu Waziri wa Maji, Binilth Mahenge
Msafara wa Naibu Waziri wa Maji, Binillth Mahenge, umepata ajali wilayani Muheza wakati akikagua miradi ya maji katika wilaya hiyo.
 
Ajali hiyo ilitokea juzi jioni katika eneo la Msangazi wilayani Muheza baada gari la Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Muheza kumgonga mtoto mdogo aliyefahamika kwa jina la  Adam Ramadhani.
 
Naibu Waziri alikuwa anaelekea kukagua miradi ya
maji iliyopo Ubembe kwa Mhosi na  Kibanda Nkumba juzi akiwa ameongozana na Mbunge wa Muheza, Herbert Mntangi, na Mkuu wa Wilaya, Subira Mgalu.
 
Ajali hiyo ilitokea wakati mtoto huyo akitaka kuvuka barabara kwenda upande wa pili bila kuangalia ndipo gafla ulitokea msafara huo na mtoto huyo kugongwa ubavuni katika gari la Mkurugenzi na kutupwa pembeni.
 
Hata hivyo, msafara huo ulisimama na mtoto huyo kupelekwa katika Hospitali Teule  Muheza na gari ya Mwenyekiti wa halmashauri ya Muheza, Amiri Kiroboto. Hata hivyo, hali yake inaendelea vizuri.
 
Naibu waziri huyo aliwapongeza viongozi wa Muheza  wakiwamo madiwani kwa kupanga bajeti yao na kuitekeleza katika sekta ya maji.
 
Mgalu alisema kwa wamefikia sehemu zuri katika utekelezaji wa miradi ya maji ya dharura na wakati wowote wananchi wataanza kupata maji.
 
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza Ibrahim Matovu alisema kuwa mradi huo wa maji wa Kitisa kupeleka maji Muheza mjini ujenzi wake utakamilika  mwezi huu.
 
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Muheza Kiroboto alimhakikishia Naibu Waziri kwamba miradi yote wataisimamia vizuri ili wananchi wa Muheza wapate maji.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: