MREMBO aliyewahi kupamba video kadhaa za wasanii wa Bongo Fleva ukiwemo wimbo wa Kidato Kimoja ulioimbwa na J.I, anayekwenda kwa jina la Maya Silemwe, amedaiwa kumtelekeza mwanaye wa kumzaa aitwaye Junior Justine (3).
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea hivi karibuni katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani, Ubungo jijini Dar es Salaam ambapo mtoto huyo aliokolewa na msamaria mwema.
Akisimulia mkasa mzima ulivyokuwa, shangazi wa mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Monalisa, alisema wao kama familia wameumizwa sana na kitendo kilichofanywa na Maya.
“Maya amezaa na kaka yangu Justine anayeishi Marekani na amekuwa akimjali sana kwa kumtumia fedha za matumizi mara kwa mara. Kisa ni kwamba kaka alimwambia Maya ampeleke mtoto Bukoba (nyumbani kwa baba wa mtoto) akasalimie, Maya akakubali lakini akamwambia atapitia kwanza Arusha (nyumbani kwao) ndipo waende Bukoba.
“Justine akamuelewa lakini kumbe alidanganya, hakwenda Arusha na kuna watu walimuona akiingia kwenye klabu moja hapahapa Dar es Salaam, wakamjulisha kaka. Sasa alipompigia kumuuliza, akawa anajing’atang’ata, siku iliyofuata akadamkia Ubungo ili kumsafirisha mtoto kwenda Bukoba kwa mama yetu (bibi wa mtoto) lakini alitaka kumsafirisha kwa kumtumia kondakta,” alisema Monalisa na kuongeza:
“Alikubaliana na kondakta huyo kisha akamwachia namba ya simu ya mama na yake ili waweze kuwasiliana na kumpokea mtoto huko Bukoba.
Kwa bahati mbaya siku ile yule konda alikuwa hasafiri mpaka siku inayofuatia. Mtoto akaanza kuhangaika stendi siku nzima bila uangalizi mzuri.
“Bahati nzuri mama mmoja msamaria mwema akafuatilia na kuonana na huyo konda, akamuomba namba za mama wa Bukoba kisha akawasiliana naye, kwa kuwa alikuwa na safari ya kwenda huko siku iliyofuata, akaamua kuchukua jukumu la kusafiri naye.”
Monalisa alikubali kutoa namba za simu za msamaria aliyejitolea kusafiri na mtoto huyo, alipopigiwa alikiri lakini aliomba sana asitajwe .
“Mimi kama mzazi iliniuma sana kumuona mtoto mdogo anahangaika stendi bila uangalizi. Nilishangaa sana kuona mzazi aliyeingia ‘leba’ anawezaje kumwacha mwanaye mdogo namna ile asafiri mwenyewe?” alisema.
Risasi lilimtafuta baba mzazi wa mtoto huyo, Justine aishiye Marekani ambapo alisema: “Jambo hilo limeniumiza sana. Kwa kweli kama ningekuwa huko nyumbani (Bongo) ningehakikisha namfundisha adabu huyo mwanamke kupitia sheria.
“Nashukuru kusikia kwamba mwanangu alifikishwa salama Bukoba.”
Mama wa mtoto huyo alipopigiwa simu alizua kioja baada ya kukataa kwamba hajawahi kumuacha mtoto kwa konda Ubungo na pia akadai eti hana mtoto na wala hajawahi kuzaa katika maisha yake yote.
Wakati tukijiandaa kwenda mitamboni juzi Jumatatu, habari zilizopenyeza katika chumba chetu cha habari zilisema kwamba mrembo huyo alimpigia simu mama mkwe wake na kumchimba mkwara mzito. Habari kwa hisani ya (Audiface)
2 comments:
wewe baba mtoto nawe unamakosa tena makubwa kama ni adabu anza kujifunza wewe. kwa akili yako unafikiri pesa peke yake ndio inalea mtoto? mbona usirudi kulea mtoto wako au ukamchukua mtoto wako ukabeba nae boxi huko ughaibuni acha maneno machafu baba na mama leeni mtoto msilete longo longo zenu kwenye vyombo vya habari
mtoto analelewa ki doti komu muacheni mtoto atulie kwa bibi wazazi mmeshindwa kazi
Post a Comment