WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, amegoma kujiuzulu wadhifa wake huo, kama alivyotakiwa na wananchi mbalimbali, wakiwamo wasomi, wanaharakati na wanasiasa.
Kwa zaidi ya siku nne sasa, Dk. Kawambwa amekuwa akiandamwa na kutakiwa kuachia ngazi, kutokana na sekta ya elimu nchini kuzidi kudidimia kila kukicha.
Moto wa waziri huyo kutakiwa kujiuzulu ulikolezwa mwanzoni mwa wiki hii, kutokana na matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012 kuwa mabaya, ambapo asilimia 60 ya watahiniwa wake wamefeli.
Dk. Kawambwa alitangaza msimamo wake huo jana, katika uzinduzi wa mpango maalum wa mafunzo ya kompyuta, uliofanyika katika Shule ya Msingi Majengo, iliyopo wilayani Bagamoyo.
Dk. Kawambwa alisema hawezi kujiuzulu kutokana na wanafunzi kushindwa kufanya vizuri katika mitihani yao na kusema kuwa hayo ni mashinikizo ya kisiasa ambayo hayana maana.
Dk. Kawambwa, ambaye pia ni Mbunge wa Bagamoyo, alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa matatizo ya elimu nchini hayawezi kumalizwa kwa waziri kujiuzulu wadhifa wake.
“Unapozungumza waziri kujiuzulu hiyo ni lugha ya kisiasa, lakini hata kama waziri anajiuzulu ndiyo matatizo ya elimu yatakuwa yamekwisha?
“Licha ya matokeo ya kidato cha nne yamekuwa si ya kuridhisha, lakini wizara yangu inaangalia ili kuweza kuona tatizo lililowapelekea wanafunzi wengi kufeli katika mitihani hiyo.
“Kitu kinachotakiwa kufanywa kwa sasa ni kufanya tathimini ya matokeo haya mabaya na kutafuta njia za kufanya, lakini siyo kushutumiana na kulaumiana,” alisema.
Waziri huyo alisema kuwa watu wanaomtaka ajiuzulu hawana hoja za msingi za kutoa shinikizo hilo, zaidi ya kutaka kujipatia umaarufu tu kwa kudandia hoja za wakati uliopo.
“Baraza la Mitihani lilikaa na kupitia kwa makini matokeo haya, ili kutaka kujiridhisha kuwa kwa nini wanafunzi wengi wamefeli.
“Lakini licha ya kuipitia mitihani hiyo kwa mara kadhaa, bado ilionekana watoto wengi wameshindwa kufanya vizuri katika mitihani hiyo.
“Kitu cha kusikitisha zaidi ni kuona hata shule ambazo zilikuwa zinategemewa kufanya vizuri, zikiwamo zile za seminari, watu binafsi na shule kongwe za Serikali ambazo huwa zinafanya vizuri nazo zimeshindwa kufanya hivyo,” alisema.
Dk. Kawambwa alisema tatizo la elimu linaweza kupunguzwa au kumalizwa kwa kuangalia upya mfumo mzima wa elimu, badala ya kutafuta majibu ya jumla.
“Lazima mfumo wa elimu uangaliwe vizuri kwa kushirikisha jamii nzima, ikiwamo wazazi, wanafunzi wenyewe na Serikali kwa ujumla, ili kuweza kuona kiini cha tatizo.
“Lakini pamoja na hayo, tunataraji kukaa na Baraza la Mitihani kuangalia upya nini kilichojiri katika matokeo hayo ya kidato cha nne mwaka huu,” alisema Dk. Kawambwa.
Akizungumzia mpango huo wa mafunzo ya kompyuta wa badiliko, Dk. Kawambwa aliwataka walimu na wanafunzi wa shule zilizopata bahati ya kuwamo katika mpango huo kutumia fursa hiyo vizuri, ili kuweza kujichotea ujuzi na maarifa.
“Nawaomba mtumie vizuri mpango huu ambao umeletwa kwenu na wenzetu wa Uingereza kusaidia shule zetu hizi kupata nafasi ya kujifunza Teknohama kwa walimu na wanafunzi wao,” alisema.
Msaada wa kompyuta 20 ulitolewa na Ubalozi wa Uingereza nchini, kupitia kituo chake cha mafunzo (British Council) ikiwa ni moja ya mikakati yake ya kusaidia ukuaji wa sekta ya elimu kwa wanafunzi na walimu wa Tanzania kujifunza kupitia teknolojia hiyo ya kisasa.
Wakati huo huo huo, Benjamin Masese anaripoti kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) limeendelea kumbana waziri huyo.
Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) jana lilitangaza siku 14 likitaka viongozi watatu katika Wizara ya Elimu wajiuzulu, vingine wataitisha maandamano.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa BAVICHA, Deogratias Munishi, alisema tayari wamekwishawaagiza viongozi wao wa wilaya kuratibu maandamano hayo.
Munishi aliwataja viongozi hao wanaotakiwa kujiuzulu ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Profesa Hamisi Dihenga, Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari, Paulina Mkonongo na Dk. Kawambwa.
Munishi alisema sababu ya viongozi hao kuwajibika ni kutokana na matokeo ya taifa ya mtihani wa kidato cha nne ya 2012 kuwa mabaya ambayo chanzo chake ni udhaifu wa Serikali ya CCM.
“Kwa matokeo haya, ni wazi kuwa Serikali imeshindwa kutambua umuhimu wa elimu katika maendeleo ya nchi, imeshindwa kuweka miundombinu na mazingira safi ya kutoa elimu bora kwa raia wake.
“Serikali imeshindwa kutambua mfumo wa elimu ambao umesababisha matokeo haya mabovu ambayo yameongeza idadi kubwa ya vijana kukosa sifa ya kuajiriwa,” alisema na kuongeza:
“Salamu za BAVICHA ni kwamba kundi kubwa la vijana wanaofelishwa kila mwaka ndilo litakalowaondoa madarakani 2015, wazazi tunawaomba mjifikirie kile walichotendewa watoto wenu,” alisema.
Munishi alifafanua utafiti mfupi uliofanywa na Bavicha umebaini kwamba zaidi ya wanafunzi 800,000 waliohitimu masomo yao ya kidato cha nne na darasa la saba mwaka 2012 hawana sifa yoyote ya kuendelea na masomo wala kuajiriwa popote.
Hata hivyo BAVICHA imeitaka Serikali kutangaza rasmi kuwa elimu ya sasa ni janga la kitaifa na kuainisha hatua zinazofaa kuchukuliwa haraka.
No comments:
Post a Comment