Tuesday, February 26, 2013

WAZIRI KAWAMBWA NA WAZIRI SHAMHUNA WAZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI ZANZIBAR.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamhuna akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na Mikakati walioiweka pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa Tanzania Shukuru Kawambwa juu ya kushirikiana na Tume ilioundwa ya kuchunguza matokeo ya Mitihani ya wanafunzi wa Kidato cha Nne,hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Elimu Zanzibar.
Baadhi ya Waandishi wa Habari Waliohudhuria katika Mkutano wa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamhuna kuzungumzia Mikakati walioiweka pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa Tanzania Shukuru Kawambwa juu ya kushirikiana na Tume ilioundwa ya kuchunguza matokeo ya Mitihani ya wanafunzi wa Kidato cha Nne,hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Elimu Zanzibar.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa Tanzania Shukuru Kawambwa (kulia)akiwa pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Zanzibar Ali Juma Shamhuna wakizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani)kuhusiana na Mikakati walioiweka juu ya kushirikiana na Tume ilioundwa ya kuchunguza matokeo ya Mitihani ya wanafunzi wa Kidato cha Nne,hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Elimu Zanzibar.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa Tanzania Shukuru Kawambwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na Mikakati walioiweka pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Zanzibar juu ya kushirikiana na Tume ilioundwa ya kuchunguza matokeo ya Mitihani ya wanafunzi wa Kidato cha Nne,hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Elimu Zanzibar.

Na salma said
Waziri wa Elimu na Ufundi Tanzania Bara, Shukuru Kawambwa amesema Zanzibar itatoa wajumbe watatu kuingia katika tume ya kuchunguza matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha nne iliyoundwa hivi karibuni na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Akizungumza na waandishi wa habari mbele ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ali Juma Shamhuna huko ofisini kwao Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar, alisema serikali zote mbili zitashirikiana kwa kufanya uchunguzi huo.
Kawambwa alisema tume hiyo itawashirikisha wajumbe kutoka vyuo vikuu na wataalamu wa elimu ili kubaini kasoro zilizojitokeza kwa kushuka kiwango cha elimu cha kidato cha nne ambapo matokeo yake yalikuwa mabaya zaidi ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Waziri huyo alisema tume hiyo yenye lengo la kutatua matatizo ya kushuka kwa mitihani, alisema itafanya kazi zake kabla ya kuwasilisha ripoti yake kwa serikali ambapo inatarajiwa kubaini matatizo yaliojitokeza katika mitihani hiyo.

Alisema serikali kwa upande wake imesikitishwa na matokeo ya mitihani ya mara hii na ndio sababu moja ya kuundwa kwa tume ili kuchunguza kiini na sababu za matokeo hayo mabaya ambapo asilimia 60 ya wanafunzi wamepata matokeo mabaya katika mitihani yao.
Waziri huyo alisema kuundwa kwa tume hiyo kutasaidia serikali kufahamu tatizo lililojitokeza katika sekta hiyo ya elimu ambayo imekuwa ikishuka.

Alisema hakuna muarubaini wa kutibu hayo zaidi ya serikali kushughulikia suala hilo kwa kutafuta walimu wazuri na kuwasikiliza matatizo yao na kisha kuwatimiziwa ili viwango vya elimu viweze kuwa vizuri.
Kawambwa alisema bado serikali haijaamua kurejea kwa mitihani kwa wanafunzi waliofanya vibaya lakini alisema watanzania wasubiri ripoti za tume ili kuona namna ya hatua za kuchukuliwa huku akiamini kwamba tume hiyo itafanya kazi vizuri kwa kuwa imeundwa kwa pande zote mbili za muungano.

Akizungumza katika mkutano huo waziri wa elimu Zanzibar Ali Juma Shamhuna alisema serikali imeongeza mshahara na maslahi ya walimu ili kupata viwango vya walimu wazuri na kuahidi kwamba kila hali itakaporuhusu itawatazama zaidi walimu hao.

Shamhuna alisema katika bajeti ya mwaka huu imeongezwa ikilinganishwa na bajeti ya mwaka jana ambapo alisema marupurupu ya walimu na posho zao zimeimarisha zaidi ingawa serikali haiwezi kumridhisha kila mwalimu lakini imekuwa ikijitahidi kadiri ya uwezo wake.

Katika hatua nyengine Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesikitishwa na matokeo mabaya ya mitihani ya wanafunzi wa kidatu cha nne ambayo yameonesha kufeli vibaya hasa katika shule za Zanzibar.

Masikitiko hayo yametolewa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Bi Mwanaidi Saleh alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Mjini Unguja.

Katibu Mkuu huyo alisema kufuatia matokeo hayo ya kufeli vibaya wanafunzi serikali imeanza kufanya uchunguzi wa matokeo hayo na sababu za kufanya vibaya ili kujua chanzo cha matokeo mabaya.
Alisema matokeo ya mitihani ni mabaya na yamewasikitisha watu wengi wakiwemo walimu na wazazi wa wanafunzi kwa ujumla lakini pia yamelifedhehesha taifa kwani matokeo mazuri daima huwa yanaipa sifa sekta ya elimu na serikali kwa ujumla.

Alisema mtu yeyote anapofanya mitihani hutarajia kupasi vizuri na kamwe hatarajii kufeli hivyo matokeo ya mwaka huu wanafunzi wengi wamefeli jambo ambalo halifurahishi kabisa.

“Mimi kama katibu mkuu na kama mzazi sijafurahishwa kabisa na matokeo ya wanafunzi mara hii kwa sababu watoto wamefeli vibaya sana, hata wizara haijafurahishwa na serikali pia” alisema Bi Mwanaidi.

Katibu Mkuu huyo alisema ingawa bado mapema kujua kiwango gani wanafunzi kutoka Zanzibar wamefeli katika mtihani huo, na kujuwa viwango vya madaraja ya ufaulu wa wanafunzi wote.
Alisema katika uchunguzi utakaofanywa ndio utakaobaini tathmini nzima ya mtihani huo na ufaulu wa wanafunzi kutoka Unguja na Pemba waliofeli na waliopasi.

Aidha Mwanaidi alisema kamati ya wataalamu wa masuala ya mitihani wameanza kukutana na kufanya tathmini kwa kuangalia vigezo mbali mbali na baadae watafanya mawasiliano na wataalamu wenzao wa elimu kutoka Tanzania Bara.
Kufeli vibaya kwa wanafunzi mwaka huu kumekuwa gumzo kubwa katika sehemu mbali mbali ambapo baadhi ya wasomi wanailaumu serikali kwa kushindwa kuweka mfumo mzuri wa elimu chini.

Mbali na wananchi kulalamikia sekta ya elimu lakini hata viongozi wa ngazi za juu serikali kama Makamo wa kwanza wa rais, Maalim Seif Sharif Hamad amehuzunishwa na matokeo hayo ambayo ni mbaya kuwahi kutokea kwa wanafunzi nchini.

Maalim Seif alishauri serikali kufanya utafiti wa kina juu ya ufaulu wa wanafunzi wengi na kwa kiwango kibaya kilichoshuhudiwa mwaka huu ambapo alisema lazima serikali itoe kipaumbele katika sekta ya elimu kwani elimu ndio ufunguo wa maisha kwa mwanadamu.

Akizungumza na wazazi katika kijiji cha Mjini Kiuyu huko Pemba, Maalim Seif alisema kiwango kikubwa cha kufeli kwa wanafunzi nchini kinatisha na ipo haja kuwepo kwa utafiti zaidi kujuwa sababu za kuanguka kwa wanafunzi hao.

Hichi ni kipindi cha pili mfululizo kwa matokeo ya mtihani wa kidatu cha nne kuwa mabaya kwa upande wa Zanzibar ambapo katika mwaka 2011 wanafunzi wengi walifutiwa matokeo yao kwa madai ya kugushi.
Miongoni mwa shule kumi zilizofanya vibaya matokeo ya kidatu cha nne nchini zipo shule kutoka Zanzibar ikiwemo Ndame ambayo wanafunzi wengi wamefeli vibaya na baadhi yao kupata alama ya sufuri na daraja na nne.

Kwa mujibu wa matokeo ya mtihani ya mwaka huu wa kidatu cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni wanafunzi 1,641 wamefaulu na kupata daraja la kwanza, wanafunzi 6,453 wamepata daraja la pili na wanafuzni 15,426 walipata daraja la tatu.

Kwa mujibu wa takwimu hizo zinaonesha wanafunzi 103,327 waliapata daraja la nne la wanafunzi 240,903 walifeli kabisa kwa kupata sufuri, jumla ya wanafunzi wanne wamejiuwa kufuatia matokeo mabaya ya mitihani yao.

No comments: