Ahadi Mwandeko (22) amenyofolewa nyama mkononi akiwa usingizini.
MWALIMU wa Shule ya msingi Motomoto iliyoko katika kijiji cha Motomoto kata ya Ruiwa wilaya ya Mbarali Mkoani hapa, Ahadi Mwandeko (22) amenyofolewa nyama mkononi akiwa usingizini.
Mwalimu huyo ambaye alikutwa na jeraha katika mkono wake wa kulia asubuhi baada ya kutoka kuamka alisema hajia ni kitu gani kilichomzuru hadi kufikia kuwa na jeraha kubwa mkononi.
Akizungumzia mkasa huo alipotembelewa na waandishi wa habari shuleni kwake Mwalimu Mwandeko alisema akiwa usingizini aliota kama anaugomvi na mwanamke ambaye hakuitambua sura yake, lakini baada ya kuamka asubuhi alijikuta akiwa na jeraha huku likivuja damu nyingi.
Alisema baada ya kukuta hali hiyo alienda kwa Mwalimu mkuuwa shule hiyo Lyidia Mdowe kwa ajili ya kumpa taarifa ya jambo lililomkuta ambapo alishauriwa kwenda Hospitali kwa ajili ya matibabu.
Aliongeza kuwa baada ya kufika katika Zahanati ya Ruiwa alipatiwa matibabu na kurejea shuleni ambapo Mwalimu mkuu alitoa taarifa kwenye Serikali ya kijiji ambapo Mwenyekiti wa Kijiji hicho Kassim Mwagalla aliitisha mkutano wa hadhara.
Mwalimu Mkuu Mdowe alisema hali hiyo imezua hofu kwa walimu wengine ambao ni wageni kiasi kwamba hata ari ya ufundishaji imepungua baada ya kuona yaliyotendeka kwa mwalimu mwenzao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji hicho Kassimu Mwagalla ambaye alilihusisha tukio hilo na ushirikina alitoa rai kwa wanakijiji kuacha vitendo hivyo kwa kuwa vinadhoofisha utendaji kazi wa watumishi hususani walimu ambao si wazawa wa eneo hilo.
Aliongeza kuwa tabia hiyo ikizidi kuendelea itasababisha walimu kuondoka ili kukimbia kupatwa na matatizo kama hayo ambayo hayasaidii maendeleo ya kijiji chao.
Pia aliwasihi kuacha mara moja tabia hiyo ambapo aliongeza kuwa mtu yoyote atakayebainika kuhusika na sakata hilo atahamishwa kijijini hapo ambapo pia aliwataka wakazi waliohamia eneo hilo kinyemela kujiandikisha ili kijiji kiwatambue.
Baadhi ya wanakijiji waliozungumza na waandishi wa habari walionekana kushangazwa na vitendo hivyo ambapo walisema dunia ya sasa ni tofauti na zamani ambayo walikuwa wakiamini kwenye ushirikina.
“ Mtu yeyote aliyekula nyama ya mwalimu huyu airudishe la sivyo tukimuona nay eye atakiona cha moto lakini pia haya mambo yalipitwa na wakati yalikuwa yakifanyika zamani bora wayaache” alisema Moses Njeje mkazi wa kijiji cha Ruiwa.
Chifu wa eneo hilo Shadrick Melele alipotafutwa kuzungumzia hali hilo amekemia vitendo hivyo ambapo pia amesema kuna mwanamke ambaye anasadikiwa kuhusika na tukio hilo amejitokeza na kumwomba msaada chifu.
Hata hivyo Chifu huyo aliahidi kulifanyia kazi sakata hilo na kulitafutia ufumbuzi ikiwa ni pamoja na kuwaonya wanaohusika na matatizo hayo ambapo Kata hiyo imekuwa ikijihusisha na matukio mengi ya kishirikina ambayo yamewahi kuripotiwa likiwemo la Chifu mwenyewe kunusurika kuzikwa akiwa hai.
Na E.Kamanga Mbeya
No comments:
Post a Comment