ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 19, 2013

HII NI SHULE: MAPENZI NI KUHAMA ULIMWENGU WA KAWAIDA NA KUZAMA KWENYE ‘MALAVIDAVI’

BAADA ya mada hii, nikuahidi kwamba itabidi tuingie kwenye darasa la kitanda. Tujuzane jinsi ya kukitendea haki, tufanye yale yanayotakiwa ili tufurahie faragha, kadhalika na wenzi wetu watufurahie.
Wiki hii, nimechagua kutoa darasa kuhusu uhusika wa kimapenzi. Mapenzi yanajengwa na wapenzi wenye mguso wa kimapenzi ambao tabia zao zimejengeka kimapenzimapenzi, yaani watu wa malavidavi.
Hutakuwa mtu wa mapenzi ikiwa mwenyewe unajidai upo makini kila eneo. Lazima ubadilike kutokana na mazingira. Kazini unaruhusiwa kutekeleza umakini wako na kusimamia mambo yaliyonyooka ili kazi ziende inavyotakiwa.
Ukirudi kwenye mapenzi, unatakiwa uwe laini. Kwa maana mapenzi yenye huba hujengwa na watu wanaoamini katika mambo madogomadogo. Wanaotaniana, wanafanyiana masihara, wanaochekeshana na kucheka pamoja. Hayo ndiyo malavidavi!
Mapenzi hayatakuwa na mashamshamu kama wewe ama mwenzi wako au wote kwa pamoja mnapenda kukunja ndita. Mnajifanya ngangari. Kuna sehemu kwenye mapenzi inafaa upige magoti, ulie na kadhalika (hata kwa kuigiza) ilimradi mwenzi wako afurahi. Mapenzi ni sanaa tamu sana!
Wanasaikolojia wengi wanaamini kuwa asilimia 99 ya wanawake, wanapenda vitu vinavyofanana. Wanapenda kuwasikia wanaume wao wakiwaambia mambo matamu lakini zaidi, hupendelea 10 ya msingi kabisa.
Je, unapenda kuwa bora? Bila shaka unatamani mwenzi wako akuone wewe ndiye Alfa na Omega. Hakika unahitaji akiwa mbali awe anatamani aone sura yako au asikilize sauti yako au hata asome SMS tamu iliyoandikwa kitaalam na vidole vyako.
Hii ni hatua kubwa zaidi katika mapenzi. Ukiona mwenzi wako amefika kwenye kiwango hicho cha upendo, maana yake unamkonga kwelikweli. Amekushiba na umejaa ndani ya kuta za moyo wake.
Hayo hayaji kama zawadi. Mapenzi huzaliwa, hustawisha kabla ya kukua. Kuna mambo ambayo unatakiwa uyafanye kuhakikisha mwenzi wako anakuza upendo wako kwako. Ni kama msemo wa ukiona vyaelea ujue vimeundwa.
Jinsi ya kumchombeza mtu, hutegemea pia jinsia. Yapo mambo ambayo mwanamke anapenda aambiwe na mwenzi wake pia yapo matarajio ya wanaume kwa wapenzi wao. Kupitia yote hayo, tutayatazama katika muktadha mpana.

YAMPENDEZAYO MWANAMKE
Hapa chini kuna maneno 10 ambayo huwapendeza wanawake wengi. Yazingatie:

WEWE NI MREMBO (You’re beautiful)
Kiswanglish kinachukua nafasi pana hapa kwetu, kwa hiyo unaweza kumwambia kwa Kiswahili au Kiingereza, muhimu ni kuangalia jinsi anavyoweza kufurahia.
Inawezekana akawa si mrembo kama Irene Uwoya au Jokate Mwegelo lakini unayo nafasi ya kumfanya ajione yupo sawa nao. Mwambie kuwa akivaa, hutoka bomba kuliko hao. Mtamkie maneno hayo asubuhi kabla hamjaachana kwenda kazini. Neno lako litamfanya ajiamini siku nzima.

UNAYAWEZA (You’re a great lover)
Kama wewe una bahati ya kupata mwenzi ambaye amepita unyagoni na kufuzu kimitindo, ni heri yako. Ikiwa uliyenaye hajiwezi, basi usisite kumwambia kwamba ukiwa naye faragha, anakutosheleza kwa asilimia 100. Unaweza kumchombeza kwa kumwambia afanye ziada ili kukufurahisha lakini tangulia kumsifia.
Wanawake wengi, hupenda kujua kama wanaume wao wanatosheka pindi wanapowapa huduma ya faragha. Ukimsifia, unampa amani ya moyo na kumfanya ajiamini.

UNA AKILI SANA (You’re so smart)
Mwanamke hupenda kuonekana ana akili. Kama kuna kitu ambacho unaweza kumkwaza mwenzi wako ni pale utakapomtamkia kwamba yeye ni mjinga. Mfanye ajione ni bora kwa kumwambia kuwa ana akili sana.
Mueleze kuwa kutokana na akili alizonazo, unaamini familia yenu itapata maendeleo makubwa kwa sababu ubongo wake ni hazina.

Itaendelea wiki ijayo.

Global Publishers

No comments: