Mwenyekiti wa TEF, Absalom Kibanda amefanyiwa upasuaji nchini Afrika Kusini na taarifa kutoka kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe inasema Kibanda ameshatoka kwenye chumba cha upasuaji.
Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) utatoa ruzuku ya chapchap na kuungana na wadau wa habari nchini na nje ya nchi kuchunguza chanzo cha ukatili uliofanywa na watu wasiojulikana dhidi ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda.
Hata hivyo, taarifa mbaya ni kwamba Madaktari wameshindwa kuokoa jicho lake la kushoto na kuamua kuling’oa.
"Wamechukua hatua hiyo ya kitatibu baada ya kuwa tayari jicho hilo lilikuwa limepondeka kwa ndani hivyo lisingeweza tena kuona. Atawekewa jicho la bandia la plastiki ambalo hata hivyo halitakuwa likiona," ilisema taarifa hiyo.
Upasuaji huo uliochukua saa 5 na dakika 30 umefanyika kwa ufanisi mkubwa na ulikuwa ukiongozwa na madaktari bingwa watatu. Wawili kati yao ni wataalamu wa kichwa na mmoja ni mtaalamu wa macho.
Taarifa imeongeza kuwa katika upasuaji huo, hakukuwa na madhara ya ndani katika kichwa chake, hivyo kichwa kiko salama. Sura yake imejengwa upya kutokana na majeraha ambayo yalikuwa yametapakaa baada ya kupigwa.
Changamoto kubwa waliyokutana nayo madaktari waliomfanyia upasuaji ni kurejesha katika sehemu yake baadhi mifumo midogo inayozunguka jicho pia kurejesha taya la kushoto ambalo lilikuwa limeathiriwa na tukio la kupigwa kwake jambo ambalo limefanikiwa.
Ripoti kamili kuhusu upasuaji huo inatarajiwa kutolewa leo na madaktari hao.
Mkurugenzi wa TMF, Ernest Sungura, amesema kuna kila sababu ya kuchunguza tukio hilo ambalo ni mfululizo wa matukio yanayopunguza uhuru wa vyombo vya habari nchini na kujenga woga kwa waandishi kufanya uandishi wa habari za uchunguzi nchini.
“Kumejitokeza mfululizo wa matukio yanayopunguza uhuru wa vyombo vya habari kufanya kazi zake bila woga. Tulikuwa nchi ya thelathini duniani kwa kuwa na uhuru wa vyombo vya habari mwaka mmoja uliopita. Tumeshuka mpaka nchi ya sabini mwaka huu. Matukio ya aina hii yanaendelea kutuweka mahali pabaya, “ alisema Sungura.
Alisema TMF ina wajibu wa kuongeza uwingi na ubora wa habari za kiuchunguzi kupitia vyombo mbalimbali vya habari ambazo amesema zinahitaji mazingira salama na yasiyo kuwa na vitisho kufanikisha uandishi wa aina hiyo.
“Kwa vyovyote vile na kwa sababu zozote, wanaotoa vitisho kwa waandishi na kuwafanyia vitendo vya kikatili ni maadui wa uandishi wa habari za uchunguzi. Ni kwa msingi huu, TMF ipo tayari kutoa ruzuku ya chapchap na kuungana na wadau wengine wa habari kuchunguza kilichomtokea Kibanda, “ alisisitiza Sungura.
Aidha, alisema TMF katika awamu ijayo, itaandaa mpango mkakati unaolenga kuwalinda waandishi wa habari wanaofanya uandishi wa habari za uchunguzi ikiwemo kufikiria uwezekano wa kuwawekea bima ya kufanya kazi kwenye mazingira hatarishi.
Kibanda, ambaye ni Mhariri Mtendaji wa kampuni ya New Habari (2006) Limited, ni mwandishi ambaye yuko mstari wa mbele katika kuhimiza uhuru wa vyombo vya habari, uandishi unaozingatia maadili ya uandishi wa habari na maendeleo ya tasnia ya habari kwa ujumla.
Mhariri huyo alivamiwa na kushambuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake saa 6.15 usiku wa kuamkia Jumatano iliyopita, maeneo ya Goba Kunguru, Mbezi Juu, kata ya Kawe, jijini Dar es Salaam. Kwa sasa yuko nchini Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.
Kwa mujibu wa Katibu wa TEF, Neville Meena, Kibanda alijeruhiwa kichwani ambapo alipigwa na kitu ambacho yeye alisema ni nondo huku jicho la kushoto likiathirika (inadhaniwa kwamba lilichomwa na kitu chenye ncha kali), kucha ya kidole cha mkono wa kulia iling’olewa sambamba na meno mawili.
Katibu huyo alisema akiwa kwenye lango, ghafla walitokea watu watatu ambao walivunja kioo cha gari ambako alikoketi, na kumvutia nje na kutekeleza walichokusudia.
Mpaka sasa vyombo vilivyojitokeza kushtushwa na kilichomtokea Kibanda ambavyo TMF itaungana navyo kutafuta mustakabari wa Kibanda ni Editors Forum, MCT, UTPC, MISA, CPJ, FAIR, AJAAT, Haki za Binadamu na vinginevyo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment