ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 25, 2013

MAKUNDI YA WANAUME NA MITAZAMO YAO YA KIMAPENZI KWA WANAWAKE -9

KATIKA kuchambua kundi la wanaume wenye gubu (Kundi la Tatu) na bahati mbaya ambayo wapo nayo kutokana na uhusika wao kimapenzi, wiki iliyopita niliishia pale nilipoanza kutoa mfano wa Rehema na mume wake mwenye wivu kupindukia.

Hebu leo tuyasome maelezo yote ya Rehema ambaye aliniambia: “Kutokana na usumbufu wa mume wangu, niliamua kufanya kazi kwa bidii ili nami nimiliki vitu vyangu. Kwani kila siku alikuwa ananinyanyasia gari lake, eti linanipa kiburi.

“Wakati mwingine alinitukana nikaumia, pale aliposema huwa nawapa lifti wafanyakazi wenzangu wa kiume kwa sababu ni mabwana zangu. Kuna siku alinitukana kabisa kuwa huwa nafanya mapenzi kwenye gari alilonipa yeye.
“Nikatamani nimiliki gari langu mwenyewe, kwa hiyo nilichokifanya nilijiendelea na masomo, yaani nilifanya kazi na kusoma kwa wakati mmoja. Nilijiwekea malengo kwamba baada ya chuo nitapandishwa cheo na kipato kitaongezeka, hivyo malengo yangu yatatimia.

“Chuo kikaleta mzozo, kila siku natukanwa. Asubuhi naingia kazini, jioni chuo natoka usiku. Kila ninaporudi ananiburuza mpaka chumbani, ananivua nguo na kunifanyia vitendo vya kishenzi kwa madai kuwa ananikagua kama nilifanya mapenzi na mwanaume.

“Siku nyingine alidai nimetoka kufanya mapenzi. Nikiwa katika hedhi, alinivua pedi mpaka aone damu ndiyo aridhike. Akidai eti naweza kufanya mapenzi na kuvaa pedi ili kumuongopea. Niliumia sana, hasa kitendo cha yeye kunisingizia nimefanya mapenzi wakati sijafanya.

“Pale chuoni nilikutana na mwanaume anayeitwa Rama. Aliyagundua matatizo yangu, akawa ananishauri, nikiwa mnyonge aligundua na kunifariji. Nikatokea kumpenda sana, maana alinipa faraja ambayo ni msamiati kwa mume wangu.
“Miezi saba tangu nianze chuo, nilijikuta naanza uhusiano wa kimapenzi na Rama. Siku za mwanzoni niliogopa sana kwa kuhofia mume wangu kujua. Ila nilijisemea lolote na liwe kwa maana mume mwenyewe hana wema, hujafanya anakwambia umefanya na anakutukana matusi ya nguoni na kukupiga mbele ya mtoto na dada wa kazi.

“Huwezi kuamini, uhusiano wangu na Rama uliendelea na hata mtoto wangu wa pili, baba yake ni Rama lakini mume wangu hajui. Sasa hivi nimeshamzoea, namchukulia kama zoba pamoja na ukali wake ambao hujitia anao. Angekuwa mume mwelewe nisingemsaliti. Nilimsaliti kwa sababu ya fujo zake.”
Mfano huo wa Rehema unatosha kukufanya utambue umuhimu wa utulivu kwenye uhusiano wa kimapenzi. Hii ndiyo sababu ya kueleza kuwa moja ya bahati mbaya ambayo wanaume wa kundi hili wanayo ni kusalitiwa na wenzi wao wa maisha.

Tatizo lingine ni kuogopwa. Kwa vile wana gubu, hata uchangamfu wao hupatikana kwa mgawo. Wake zao hunywea kila wanapogundua kwamba kisirani kimeanza. Watoto na memba wengine wa familia, hupatwa mchecheto ndani ya nyumba.

Hiyo siyo sifa nzuri kwa mwanaume. Baadhi huona sifa kwamba wanaogopwa lakini shika ukweli huu kwa faida yako kwamba wengi wamekosa mengi mazuri kutokana na hulka zao za jazba na hasira za haraka. Wivu unaozaa gubu ni kichocheo cha nyumba nyingi kuparanganyika.
Itaendelea wiki ijayo.

GPL

No comments: