Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, kwa mara ya kwanza amezungumzia ugonjwa uliomweka katika kitengo cha wagonjwa wenye ungalizi maalumu (ICU) akiwa hajitambui kwa siku 42, na kueleza kuwa alikutwa na vijidudu vya malaria 500 mwilini mwake.
Akiwa amechangamka na mwenye matumaini mapya baada ya afya ya kuimarika, DCI Manumba aliyeelazwa katika moja ya hospitali za mjini hapa, alisema ni kwa mkono wa Mungu amepata nafuu kubwa baada ya juhudi kubwa za madaktari katika kupigania uhai wake.
Alisema anawashuru sana madaktari wote waliohangaika usiku na mchana katika hospitali alizolazwa kuanzia Muhimbili na Agha Khan, jijini Dar es Salaam, kabla ya kusafirishwa kwa ndege maalumu kuja kwa matibabu jijini hapa akiwa hajitambua kabisa.
Pia alimshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kutambua hali yake ilivyo kuwa na kusaidia kuletwa jijini hapa kwa matibabu zaidi ambayo kimsingi yamemrejeshea uhai wake.
“Kwa kweli sasa kama mnavyoniona sijambo sana. Nimeanza kufanya mazoezi. Sijambo kwa kweli ingawa bado niko hospitalini naendelea na matibabu,” alisema Manumba.
Alisema kwamba juhudi za madaktari wapatao watano, kila mmoja akijishughulisha na eneo lake la utalaamu ndiyo waliokoa maisha yake.
“Unajua malaria yale nilikaa nayo sana mwilini mwisho yakaanza kuzalisha sumu ambayo iliathiri vitu vingine vingi mwilini,” alisema Manumba na kuongeza kuwa kabla ya kudondoka alikuwa anaendelea na kazi kama kawaida bila kujua kuwa alikuwa ana malaria kali kwa kiwango hicho. Pia aliwashukuru wote walimuombea wakati akiwa na hali mbaya, na kuwaomba waendelee kumuombea ili apone kabisa na kurejea nyumbani kuendelea na kazi zake kama kawaida.
Manumba amelazwa hospitali tangu mapema Januari mwaka huu na kulazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na baadaye ICU katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.
Manumba alikuwa hajitambui baada ya kuugua malaria ghafla na hali hiyo ilisababisha pia figo zake zote mbili kushindwa kufanya kazi.
Baadaye mwezi huo, alisafirishwa kupelekwa nchini Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment