Askofu Shao akiwasha mshumaa wa Pasaka muda mfupi kabla ya kuanza Ibada ya mkesha kwenye kanisa la St.Joseph mjini Zanzibar jana.
Askofu wa Kanisa katoliki Zanzibar, Augustino Shao amesema kuwa Kwa muda wa miaka isiyopungua miwili, jamii kisiwani Zanzibar imejengewa chuki na kutoaminiana kwa misingi ya itikadi za dini,siasa na mahali alipotoka mtu. "Chuki hii ilienezwa na vyombo vya habari, viongozi wa dini, walimu mashuleni na wanasiasa."
Akitoa ujumbe wa Pasaka kwenye Ibada ya mkesha iliyoanza saa 12 jioni badala ya saa 4 usiku kutokana na hali ilivyo tete hapa visiwani, Askofu Shao alifafanua kuwa Watoto na Vijana wa Taifa moja walisadikishwa kwamba kila asiye wa imani yao ni mwovu.
Mafundisho haya ya uongo yaliendelea kwa muda mrefu bila kukemewa na hivyo yakachukuliwa kuwa kweli. "Madhara ya chuki na uongo huu ni makubwa kwa sasa na kwa vizazi vijavyo."Alisema Askofu Shao na kuongeza kuwa uongo na chuki iliyoenezwa juu ya watu wa imani nyingine na chuki juu ya watu wa Bara wanaoishi Visiwani imefikia hali ya hatari kiasi cha watu kunyimwa usafiri na mahali pa kuishi.
Ameomba vyombo husika kuchukua hatua mara wapatapo taarifa za uadui huo.
Waimbaji wa kwaya ya St.Joseph ya mjini zanzibar wakiimba kwenye Ibada ya mkesha jana.
Askofu wa kanisa katoliki jimbo la Zanzibar, Augustino Shao akitoa Sakramenti ya Kipaimara
kwenye Ibada ya mkesha wa Pasaka mjini Zanzibar jana.
Picha na Martin Kabemba
No comments:
Post a Comment