Unapogundua kuwa mke au mwanamke wako yupo kwenye hisia za kipindi cha mpito, hakikisha unakuwa naye karibu, vinginevyo atakusaliti.
Janga kubwa zaidi ni kwa wanawake ambao wapo kwenye uhusiano wa kawaida. Mwanamke anakuwa anahitaji ndoa, anatamani avae pete ya uchumba na hatimaye aitwe mke wa fulani, anashuhudia kila siku wenzake wanaolewa. Hapo ataanza kuteswa na hisia za kipindi cha mpito.
Mwanamke wa aina hiyo, kwanza atakuwa anamuuliza mwenzake ni lini naye atavaa pete ya uchumba. Majibu ya mwanaume ndiyo huamua ama awe mwaminifu au asaliti, kwani akigundua mwenzi wake haeleweki, ni rahisi kutumbukia kwa mwanaume ambaye ataonesha yupo tayari kumuoa wakati wowote.
Je, hujawahi kukutana na mwanamke akakwambia hivi: “Kuna jamaa kanitongoza, amesema yupo tayari kwenda nyumbani kujitambulisha hata leo, kwani wewe una mpango wa kujitambusha nyumbani lini?” Kama umeshawahi kuambiwa, basi akili ikae kichwani kwako.
Maana yake ni kwamba anakuzindua uchangamkie tenda, vinginevyo wenzako watachukua mzigo. Naye atakaa akikupima na kukusikilizia, akishaona hueleweki, atakuacha na kuangukia kwa yule ambaye atamuona yupo tayari kumvusha kwenye hicho kipindi cha mpito.
Kwa mwanamke, kitendo cha kuchelewa kuolewa hukitafsiri kama aibu kwake. Huumia zaidi pale wenzake wanapoolewa. Fikiria yeye ndiye mkubwa halafu mdogo wake anachumbiwa na kuolewa, wakati huohuo, yeye anabaki akikusikilizia. Chunga sana na kama unamhitaji, hebu tangaza nia mapema.
Endapo utampa matarajio chanya, utamfanya atulie. Hatakuwa na wasiwasi kwa sababu ataamini naye siku yake itafika, atavaa shela, pete kwenye kidole. Hebu mwambie kwamba unajipanga muoane kwa sherehe bomba. Hapo utakuwa umempa tiba mahususi yenye tulizo la hisia za kipindi cha mpito.
Hicho ni kipengele kimoja, hisia za kipindi cha mpito zipo katika matawi mengi. Inawezekana mwanamke wako akapoteza kazi, akawa anasumbuliwa na mawazo. Unachotakiwa kufanya ni kuwa karibu naye, kumfariji. Ukikaa mbali naye, atapata mfariji ambaye atachukua nafasi yako.
Kwa kawaida, mwanamke humwamini mtu kwa haraka sana. Siku zote hisia zao zipo kati. Anaweza kukuona leo wewe ni sawa na malaika wake hapa duniani, ukimweka mbali kidogo tu nyakati za matatizo, atakayemfariji humwona malaika bora zaidi. Ukichelewa, atakushusha thamani kutoka malaika wa mbinguni hadi Shetani wa Jehanamu.
Hili ni angalizo kwa pande zote mbili. Mwanaume anatakiwa kuwa makini na mwenzi wake wakati wa hisia za kipindi cha mpito, vilevile mwanamke naye anapaswa kujichunga. Hisia zake, hazitakiwi kumpeleka mahali ambapo anaweza kumsaliti mwenzi wake au ndoa yake.
Wengi walijuta sana baadaye, baada ya kugundua kwamba wanaume ambao waliwavuta na kuwaona ni bora sana kwa sababu waliwafariji, ni majanga mtindo mmoja. Ukweli ni kuwa mwanzoni anapokuja kwako, hawezi kukuonesha tabia zake za ajabu, daima atakufanya umuone ni mtu bora sana.
Hivyo basi, usingoje kujuta baadaye, kwani majuto ni mjukuu.
Itaendelea wiki ijayo.
Global publishers
No comments:
Post a Comment