ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, April 20, 2013

MARAFIKI, ULIMI WAKO, KABURI LA MAPENZI YAKO-2

Wiki iliyopita, nilieleza kuwa kama marafiki wenyewe wanachukuliana wapenzi, ni kwa nini isikupe sababu ya kuamini kwamba wewe upo sahihi zaidi kwenye uamuzi wako kuliko mshauri?
Pengine anakujaza maneno ya chuki kwa mwenzi wako, mwisho ukamwona hafai, baada ya majuma mawili unagundua yupo naye.
Ukiweka pembeni hoja ya kuchukuliana wapenzi, ukweli mwingine ni kwamba rafiki anaweza kukufanya uachane na mwenzi wako mnayependana na kuelewana vizuri ili ukajiweke kwa mwenye fedha. Mwisho wa hilo siku zote kuna majuto, kwa maana pesa itakuwezesha kutatua mambo mengi lakini haziwezi kukupa penzi linalokidhi moyo.
Kama ambavyo umewahi kushuhudia mateso ya mtu kulazimishwa kuoa au kuolewa na yule asiyempenda kwa sababu mbalimbali, hususan kichocheo cha shinikizo la wazazi, ndivyo hutokea pale uhusiano unapojengwa na fedha. Shika neno hili kuwa binadamu ni rahisi sana kuzizoea fedha pale anapokuwa anazipata.
Anapozoea maisha ya fedha, moja kwa moja humuona wa kawaida sana, yule mwenzi wake aliyemkubali kwa sababu ya mali. Ni hapo ndipo humsaka yule atakayempa tulizo la kweli la moyo. Vitendo vya wenye fedha wengi kusalitiwa, ikupe sababu ya kuyazingatia haya.
Kwa nini baadaye uje kuvuna aibu ya kuonekana msaliti? Amua leo kwamba pamoja na hali yoyote ya kimaisha uliyonayo na mwenzi wako, mtalindana kwa shida na raha. Yote yanawezekana, endapo kwa maelewano yenu na nia ya dhati, mtajitolea kusaka maisha bora zaidi, yatapatikana tu.
Epuka kukimbilia mali zilizotafutwa na mwingine kisha wewe uje uvune tu. Wengi wamenyanyasika sana na matokeo yake wakaishi maisha ya mpenzi wa picha. Yaani, akimkumbuka labda aangalie picha, vinginevyo muda mwingi anakuwa ‘bize’ na kazi au na wapenzi wengine ambao ataona wanaendana na wakati.
Wewe alikuona unafaa kwa wakati wako, jeuri yake ya fedha inamfanya atafute wengine ambao ataona wanamtosheleza kutokana na wakati wao. Inawezekana akakuacha au akaamua kukufanya mpenzi wa mapozeo. Yaani siku nanga zikipaa, anakuja kwako umpe joto, akishatosheka na kukupa kisogo, humuoni tena mpaka baada ya miezi mitatu.
Linda penzi lako. Kwa hali yoyote aliyonayo mwenzi wako, unatakiwa kuhimili vishindo vya aina zote. Fedha na vishawishi vya marafiki, wewe achana navyo. Hapa namaanisha jinsia zote, kwani ipo mifano mingi ya wanaume kuwaacha wenzi wao na kukimbilia kwa wanawake wenye fedha au kutokana na maneno ya marafiki.
Acha tamaa, tunza moyo wako; dhana ya mashindano katika mapenzi ni muhimu sana. Itakupa sababu ya kupigana kwa akili bila kutumia nguvu, kuhakikisha unakuwa bora. Husika kikamilifu mpaka mwenzi wako akiri kwamba hajawahi kuyafurahia mapenzi kama anavyofurahia akiwa na wewe.
Ni muhimu tu kujua kwamba marafiki hawawezi kuwa kila kitu kwenye maisha yako ya kimapenzi. Endapo utawaendekeza, wao ndiyo watakaokuwa wa kwanza kuupeleka kaburini uhusiano wako wa kimapenzi. Sasa hapo unaweza kuamua mwenyewe, kujenga au kubomoa.

Itaendelea wiki ijayo.

Global Publishers

No comments: