Saturday, May 18, 2013

Hofu yatanda bungeni

Dodoma. Hali ya wasiwasi imelikumba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kuwepo kwa tetesi ya shambulio la kigaidi katika maeneo ya Bunge.
Hali hiyo inafuatia ujumbe mfupi wa maneno uliosambazwa, ukitaadharisha kuwa kuna tukio la kigaidi limepangwa kufanywa katika eneo la Bunge.
Ujumbe huo uliosambazwa kwenye simu za baadhi ya wabunge ulisomeka hivi:-
"Kuna kikundi kina mkakati wa kufanya shambulio la bomu bungeni Dodoma na msikiti wa Msavu Morogoro. Ni ndani ya muda mfupi wakati bado vikao vya Bunge,"ailisema sehemu ya ujumbe huo.
Habari zaidi zinasema kuwa tayari jeshi la polisi imefanikiwa kupata mtu aliyetuma ujumbe huo, ambaye anadaiwa kutuma kutoka mikoa ya kanda ya kaskazini na wamefanikiwa kumleta mjini hapa kwa mahojiano zaidi ili kufanikisha upelelezi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Mussa Azzan Zungu, juzi alilitangazia Bunge hali hiyo ya hatari  wakati wabunge wakiendelea na mjadala wa hotuba ya makadirio ya matumizi wizara ya Uchukuzi ya mwaka 2013/14, na kulazimika kurudia tangazo hilo wakati akiharisha Bunge.  
“Waheshimiwa wabunge wote mnaombwa kuanzia kesho tarehe 17, mwezi huu, mwaka huu, kutoegesha magari yenu pembezoni mwa uzio unaozunguka ofisi ya bunge hapa Dodoma…Badala yake magari hayo yaingizwe katika geti la eneo la maegesho ya waheshimiwa wabunge ndani ya viwanja vya Bunge” alisema Zungu
mnaombwa kuanzia kesho tarehe 17, mwezi huu, mwaka huu, kutoegesha magari yenu pembezoni mwa uzio unaozunguka Ofisi ya Bunge hapa Dodoma…Badala yake magari hayo yaingizwe katika geti la eneo la maegesho ya waheshimiwa wabunge ndani ya Viwanja vya Bunge” alisema Zungu
Alisema mbunge yeyote atakaye taka kuegesha gari lake nje ya ofisi, anaombwa aegeshe ng’ambo ya upande wa kaskazini wa barabara itokayo jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alisema ulinzi umeimarishwa katika eneo lote la Bunge kuhakikisha hakuna chochote cha hatari kinachoweza kutokea.
“Vijana wangu wanafanya kazi yao vyema na iwapo kuna tishio lolote lile litafanyiwa kazi,” alisema Dk Nchimbi
Dk Nchimbi alisema ulinzi utaendelea kuimarishwa katika eneo hilo kuliko wakati wowote ambao Bunge limewahi kuwekwa katika usalama.
Mbunge wa kuteuliwa na Rais, (NCCR-Mageuzi) James Mbatia alisema ni kweli kuwa jana (juzi) Bunge lilipata taarifa hiyo na kuzua mshtuko miongoni mwao lakini akaitaka Serikali kusimamia kidete suala la ulinzi na usalama.
“Hili ni Bunge, mhimili huu mkubwa ukianguka… nchi imesambaratika, tishio la usalama bungeni lifanyiwe kazi haraka.
“Serikali iwe makini, kwa mfano simu zinazosambaza ujumbe wa kutishia amani zifuatiliwe ili kubaini chanzo cha taarifa nyingine za uchafuzi wa amani zinazosambazwa” alisema Mbatia
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, (CCM) Ester Bulaya aliitaka Serikali kuchukua tahadhari kwa viashiria vyote vya migogoro au kutengua amani kwani Bunge linapofikia hatua hiyo basi athari kubwa zinaweza kutokea.
“Nimeshtushwa na tahadhari hiyo iliyotolewa bungeni jana (juzi) kwa sababu nchi yetu imekuwa na amani, ina maana hali si nzuri” alisema Bulaya.
Mbunge huyo aliishauri Serikali kuimarisha ulinzi na kuyafanyia kazi matatizo na migogoro yote inayoendelea ili nchi yetu iwe na amani kama ilivyokuwa zamani.
“Waswahili wanasema, ‘Mzaha mzaha… hutumbua usaha’. Wasipochukua hatua leo pengine yanaweza kutokea makubwa zaidi,” alisema Bulaya.
Mwananchi

No comments: