Dar na mikoani. Wakati Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akisema CCM itazoa ushindi katika kata zote 25 katika uchaguzi mdogo wa madiwani ambao kampeni zake zinaendelea nchini kote, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema watashambulia ardhini.
Hatua ya Lowassa inakuja baada ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kuzindua kwa mbwembwe juzi kampeni za udiwani Kata ya Makuyuni, Monduli kwa kutumia helikopta.
“CCM ni jeshi la miguu. Tuko pamoja na wananchi na ndiyo maana tunafungua matawi kwa kishindo,” alisema Lowassa jana.
Lowassa aliyekuwa pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha, Namelok Sokoine walimrudisha CCM, Mkuu wa Wazee wa Kimasai, Samuel Soinge aliyekuwa Chadema, walipokuwa wakimnadi Goodluck Lerunya anayewania udiwani katika kata hiyo.
Akizindua kampeni katika Kata ya Mbalamaziwa, wilayani Mufindi mkoani Iringa, Kinana alisema: “Kutokana na jeshi kubwa na wafuasi tulionao na imani inayoendelea kuonyeshwa na wananchi kuiunga mkono CCM, tuna imani dhamira hii itafanikiwa bila shaka yoyote.
Chadema
Akihutubia mkutano wa kampeni katika Viwanja vya Soweto Arusha juzi, Lema alisema chama chake kimepata taarifa kuwa baadhi ya vyama vimejiandaa kufanya fujo ili kuvuruga kampeni za Chadema inayopigana kurejesha viti vinne vya udiwani katika Kata za Elerai, Kimandolu, Kaloleni na Themi.
“Kama jeshi la polisi hawatatulinda, tutajilinda wenyewe kupitia Red Briged. Tunao uwezo wa kujilinda na kuwadhibiti wenye nia ya kutuhujumu,” alisema Lema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas alisema jeshi hilo limejipanga kikamilifu kudhibiti vurugu na uvunjaji wa sheria kipindi chote cha kampeni na kuvitaka vyama vyote kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.
Akimnadi mgombea wa Chadema Kata ya Kaloleni, Emmanuel Kessy, Lema aliwaomba wapiga kura kuwachagua wagombea wa Chadema ili kukipa chama hicho uwezo wa kuongoza Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Singida na Arusha
Akimnadi mgombea udiwani wa CUF katika Kata ya Iseke, Tarafa ya Ihanja, Wilaya ya Ikungi, Singida, Abdallah Kinyeje, Mwenyekiti wa chama hicho Mtaa wa Mkunduge Kinondoni, Dar es Salaam, Tamim Omari Tamim alisema chama chake hakina udini, ukabila, ukanda, ubaguzi, kupandikiza chuki wala harufu ya vurugu zinazosababisha madhara na Watanzania kupoteza maisha.
CUF pia kimetamba kuibuka na ushindi katika uchaguzi mdogo katika kata tatu za Arusha Mjini, kati ya nne kutokana na kuwa na wagombea wanaokubalika. Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro alisema: “Hapa Kaloleni hakuna ambaye hamfahamu, Abbas Mkindi... Elerai kuna John Bayo na Themi yupo Petro Ndalivoi.”
Mwananchi
1 comment:
Ondoa huu uchafu humu unatupotezea muda kwenye blog yetu.
Post a Comment