TUMEZOEA kuanza siku kwa kunywa vinywaji moto kama vile kahawa au chai na hii imekuwa ndiyo desturi ya maisha ya watu wengi duniani. Lakini siyo lazima kuanza siku yako kwa kunywa vinywaji hivyo, ambavyo tafiti nyingi zimeonesha chai na kahawa vikitumiwa kupita kiasi vinaweza kuwa na athari kwa mtumiaji.
Katika kuangalia njia mbadala na bora ya kufungua kinywa na kuanza siku vizuri, imebainika kuwa glasi moja ya maji ya uvuguvugu yaliyochanganywa na juisi ya limau kipande kimoja, yana faida kubwa mwilini na yanafaa kutumiwa kama kifungua kinywa asubuhi.
Zifuatazo ni baadhi ya faida kubwa za kunywa maji kwa kuchanganya na juisi ya limau asilia kama zilivyoanishwa na kuthibitishwa na tafiti mbalimbali za kisayansi:
HUSAIDIA USAGAJI CHAKULA: Maji ya uvuguvugu husaidia kuuamsha na kuuchangamsha utumbo na maji ya limau hulainisha na kuondoa sumu yoyote inayoweza kuwa imeganda kwenye utumbo na kuipeleka kweye njia ya haja kubwa ili kutolewa kama uchafu.
HUONDOA SUMU KWENYE NGOZI NA MWILINI: Unywaji wa maji ya uvuguvugu yaliyochanganywa na juisi ya limau husaidia sana kuondoa sumu na uchafu kwenye ngozi kwa njia ya mkojo. Aidha, kiwango kingi cha Vitamin C kilichomo kwenye juisi ya limau huondoa takataka zote za kwenye mwili na damu, hivyo kuiacha ngozi yako safi, laini na nyororo.
HUIMARISHA KINGA YA MWILI: Kama tulivyoona hapo juu, limau lina kiwango kingi cha Vitamin C ambayo ni muhimu katika kujenga kinga ya mwili na huzuia magonjwa ya mafua na kikohozi. Halikadhalika limau lina kiwango kingi cha ‘potasiamu’ ambayo huamsha ubongo na kudhibiti shinikizo la damu.
HUONDOA ULEVI WA KAHAWA: Kuna watu wameshazoea kunywa kahawa kila siku na kuwa kama ulevi, kwani wanapokosa kunywa huwa kama wagonjwa, lakini kwa kunywa maji na limau hali hiyo ya ‘uteja’ huondoka na kujisikia huru na mchangamfu.
HUSAIDIA KUPUNGUZA UZITO: Limau pia lina kiwango kingi cha kirutubisho aina ya kamba lishe (pectin fiber) ambacho ukikila kinakufanya ujisikie kushiba. Hivyo maji haya ni mazuri sana kwa watu wenye kuhitaji kupunguza uzito au kuimarisha uzito walionao.
MAMBO YA KUZINGATIA KABLA YA KUANZA
Hakikisha kiwango cha joto cha maji utakayotumia kiwe cha kati, si ya moto wala baridi. Maji moto sana siyo mazuri kwasababu yataua virutubisho vilivyomo kwenye limau na ya baridi sana yanaweza kusumbua tumboni. Pia yawe maji safi na salama.
Ili kuyalinda meno yako dhidi ya uchachu wa limau, pendelea kutumia mrija kunyonyea maji hayo. Hakikisha unakamua juisi yako kutoka kipande cha limau halisi na siyo juisi ya limau iliyosindikwa kwenye chupa.
Ukiwa na mazoea ya kuanza siku yako kwa kunywa mchanganyiko huu wa maji na juisi ya limau, afya yako itaimarika, hutapatwa na magonjwa kirahisi na ngozi yako itakuwa laini na nyororo.
Global Publishers
No comments:
Post a Comment