ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 21, 2013

UTAMU AU MATESO YA MAPENZI HUTOKANA NA MTINDO WAKO WA MAISHA - 6

Nilishaeleza katika makala yangu huko nyuma kwamba maisha ya kimapenzi ni kama kioo. Yaani ukiyachekea nayo yatakuchekea, ila ukiyanunia, nayo yatakukunjia sura
Hakuna njia mbadala wa kuyachekea mapenzi zaidi ya kuwekeza upendo pale ambapo unahitaji kupendwa. Ni kichekesho kwa mbaguzi, mwenye chuki kwa wenzake halafu eti anataka apendwe.

Kosa kubwa ambalo wengi wetu hulifanya ni kujenga matarajio. Kila mmoja wetu anataka afanyiwe mengi lakini yeye mwenyewe huwa hajiulizi ni kipi anachopaswa kufanya kwa lengo la kumridhisha mwenzake. Ni vizuri kujua kuwa kadiri wewe unavyotaraji kufanyiwa na mwenzako anatarajia umfanyie.

Katika mapenzi hutakiwi kuingia na sura bandia. Kila ‘aliyefeki’ uhusika wake kwenye uhusiano wa kimapenzi, aliishia kuharibikiwa. Hata kama una udhaifu wako, acha uonekane ili uwe huru muda wote. Vinginevyo, utajichimbia kwenye dunia ya mateso ya kujitakia.
Kukubali udhaifu wako uonekane, kunakupa sifa kwamba wewe ni mwelewa. Hilo ni jambo la muhimu kuliko kujionesha wewe ni mkamilifu, halafu baadaye yale uliyokuwa unayaficha yanaonekana, sasa inakuwa aibu kwako. Mtu bandia kila siku hufeli, mwenye uhalisi wake atazidi kwenda mbele.

Uhusiano wa kimapenzi siyo kitu rahisi. Huweka wazi kila kitu ambacho mtu anakifikiria ndani yake au anachokitarajia. Kwa kawaida, mtu anavyohusika kwenye mapenzi ndivyo ambavyo hutoa kielelezo cha namna anavyotaka maisha yake na mwenzi wake yawe.

Mapenzi yanakutaka uwe unatabasamu ili na yenyewe yatabasamu kwa ajili yako. Huwezi kuwa kwenye kipindi kibaya halafu ukayatendea haki mapenzi. Ukiwa na siku mbaya, watu wanaokuzunguka, hususan mwenzi wako atakugundua. Vivyo hivyo, ukiwa hauna furaha.

Ukiwa mtu wa kulia, yenyewe yatalia na wewe na hutayafurahi hata siku moja. Watu jasiri ambao huamini katika mapenzi yanayochanua, badala ya kulia, huangalia tatizo na kulipatia ufumbuzi ili waweze kucheka kisha mapenzi nayo yawachekee.

Tukirejea pale tulipoishia wiki iliyopita kwenye kipengele cha kuchagua mapambano ni kwamba wapo wale ambao, hata pongezi kwao inaweza kuibua malumbano. Sasa kwa vile wewe unataka furaha, inakubidi uangalie namna bora ya kukabili mambo.
Mfano, unamwambia mwenzi wako umependeza, badala ya kukujibu asante, anaweza kukuuliza: “Kwani siku nyingine huwa sipendezi.” Ukimjibu huwa anapendeza, atakuhoji ni kwa nini huwa humsifii, badala yake umemsifia siku hiyo.

Pengine badala ya kupokea pongezi, yeye akajibu: “Ni kawaida yangu.” Vilevile, inawezekana akakuhoji maswali mpaka ukakoma siku nyingine kumpongeza kwa kupendeza. Hayo ni mambo ambayo unapaswa kuamua ama kuyarekebisha au kuyakimbia kama utakuwa unataka furaha katika uhusiano wako wa kimapenzi.

Huo ni mfano tu lakini angalizo kwako ni kwamba uamuzi wa kukimbia ni sawa lakini huyo ambaye utakutana naye ni binadamu, naye utamkuta ana kasoro zake, kwa hiyo utatakiwa uamue kuainisha upungufu alionao kabla ya kuchagua mapambano na mbinu za kupambana. Usikimbie, hebu tulia na ufanye juu chini kumbadilisha.

Hata hivyo, wakati ukimbadilisha jaribu kujiuliza maswali ambayo yana msaada mkubwa sana kwako unapoyapatia majibu. Ainisha vitu vinavyokukwaza kwa mwenzi wako halafu jiulize kabla hujaingia rasmi kwenye mapambano ya kuyaondoa hayo mambo yanayokukwaza ili uyafurahie mapenzi yako.
Kuna maswali matatu ya kujiuliza. Haya kama dira yako lakini kama unadhani yapo mambo mengine ambayo yanajitokeza kwenye uhusiano wako na unapaswa kujiuliza na kupata majibu kwa haraka. Sababu ya kujiongeza maswali ni kwamba kuna mazingira hutofautiana kati ya uhusiano mmoja hadi mwingine.

Itaendelea wiki ijayo.
GPL

No comments: