Majeruhi wa mlipuko wa bomu Arusha, Mwalimu Fatuma Tarimo akionyesha kipande cha chuma baada ya kuondolewa kwenye mguu wake, katika Hospitali ya Muhimbili Dar es Salaam jana. Picha na Michael Jamson
Dar es Salaam/Arusha. Bomu lililorushwa na kuua watu watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 60 kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi huko Arusha, inadaiwa lilitengenezwa kienyeji.
Wakati kukiwa na madai hayo, mazishi ya marehemu hao Regina Kurusei, (45), James Gabriel (16) na Patricia Joachim (9) yanatazamiwa kufanyika leo Olasiti, Arusha na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda anatarajiwa kuhudhuria.
Ofisa mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alimdokeza mwandishi wetu jana kuwa kwa ujuzi na uzoefu wake wa masuala hayo, bomu hilo si la kiwandani akisema msingi wa imani yake ni jinsi vyuma vilivyotawanyika na kuumiza watu zaidi ya 20.
Watu saba wamefikishwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kuondolewa vyuma na kupata matibabu zaidi.
Mstaafu huyo alieleza kuwa mabomu mengi zaidi ya kienyeji hutengenezwa kwa kutumia bakuli za chuma, zikiwekewa baruti ndani na kufungwa kwa waya.
“Hawa jamaa huweka vipande kama 36 vya baruti na hufungiwa ndani ya bakuli kwa kubanwa sana ili kuvipa joto na bomu likitua, husababisha madhara makubwa,” alisema ofisa huyo ambaye alishiriki Vita ya Uganda mwaka 1978 hadi 1979.
Mstaafu huyo alisema mabomu ya aina hiyo yametumika kwenye mashambulizi ya kigaidi katika nchi mbalimbali duniani kama Lebanon, Vietnam, Libya, Ireland Kaskazini, Syria, Afghanistan, Iraq, Chechnya na India.
Mmoja wa majeruhi, Mwalimu Fatuma Tarimo amesimulia alivyoshuhudia bomu likitua mbele yake na kulipuka.
Tarimo, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alisema jana kuwa aliliona bomu hilo likiwa na rangi ya shaba. Pia alisema lilikuwa na waya kwa juu.
“Baada ya kutua, nilisikia kishindo kikubwa nikashtuka ikabidi niangalie. Baada ya kuona ni kitu kama chuma nilipata hofu nikafikiria kuondoka,” alisema mwalimu huyo wa Shule ya Msingi ya Burka Estate, nje kidogo ya Jiji la Arusha. Hata hivyo, alisema kabla ya kuondoka, alishtukia amenyanyuliwa juu na hakujua kilichoendelea kwani aliposhtuka alijikuta akiwa katika Hospitali ya Mount Meru.
Tarimo ametolewa kipande cha chuma katika mguu wake wa kulia.
“Nina maumivu bado lakini nina matumaini nimechukuliwa kipimo cha ‘T-Scan’ kwa matibabu zaidi,” alisema Mwalimu Tarimo ambaye anaaminika kuwa na kipande kingine kwenye mapafu.
“Nina maumivu bado lakini nina matumaini nimechukuliwa kipimo cha ‘T-Scan’ kwa matibabu zaidi,” alisema Mwalimu Tarimo ambaye anaaminika kuwa na kipande kingine kwenye mapafu.
Majeruhi mwingine, Jenipher Joackim ambaye amefiwa na mwanaye Patricia Joackim (9) hana taarifa za kifo hicho kilichotokea katika Hospitali ya KCMC.
“Nimeambiwa kwamba yupo ICU sijui anaendeleaje,” alisema.
“Nimeambiwa kwamba yupo ICU sijui anaendeleaje,” alisema.
Jeshi la Polisi mkoani Arusha limetangaza donge nono la Sh50 milioni kwa watu watakaosaidia upelelezi wa ulipuaji bomu huku likiwashikilia na kuwahoji watuhumiwa 12 hadi sasa.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment