Wednesday, May 1, 2013

MBINU ZA KITAALAM ZA KUDHIBITI USALITI! -4


KUWA memba wa ukurasa huu pekee kunakupa nafasi kubwa ya kufurahia mapenzi na kukuweka mbali kabisa na mateso. Ni kweli mapenzi hayana kanuni lakini wakati fulani ukipata nafasi ya kujifunza vitu vipya unajiweka kwenye uhakika wa kujitenga na mateso.

Maumivu ya mapenzi yanaelezwa kuwa ni makali zaidi pengine kuliko kitu chochote. Wakati fulani maumivu hayo hushinda hata yale ya makovu ya kutapeliwa kibiashara na mengine mengi yanayokera.
Utafiti unaonesha kwamba, wanaume ambao wana ndoa imara na wanaishi maisha ya furaha, wana nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa katika maisha yao. 

Utafiti huo unaendelea kueleza kwamba, wanaume hao wawapo kwenye majukumu yao ya kazi huwa wachapakazi zaidi kuliko wale wenye ndoa zenye migogoro kila kukicha.
Kutokana na utafiti huo, bila shaka sasa unaweza kuona ni kwa namna gani mapenzi yanaweza kusababisha matatizo au mafanikio katika maisha. Ni suala la kufahamu na kuchagua tu.
Marafiki zangu wapenzi, leo ndiyo namalizia mada hii ambayo imedumu hapa kwa wiki nne mfululizo. Ingawa ni ndefu ni matumaini yangu kwamba haijakuboa na badala yake imekuongezea kitu.
Katika matoleo yaliyopita, nilieleza kwa mapana juu ya usaliti na sababu zake. Kubwa zaidi nililokazia ni namna ya kukomesha usaliti huo ndani ya ndoa.

Yapo mengi niliyoeleza huko nyuma, leo nitamalizia na vipengele vingine muhimu zaidi ambavyo bila shaka vitawaongezea vitu vipya ubongoni mwenu.
Kama mtakumbuka, nilieleza zaidi mambo ambayo kama yakizingatiwa kwa umakini yatasaidia kwa kiasi kikubwa kulinda ndoa au uhusiano dhidi ya usaliti.
Naomba nisisitize tena, mada hii imelenga zaidi juu ya usaliti ndani ya ndoa. Hebu twende tukamalizie sehemu hii ya mwisho nikiamini kwamba utajifunza kitu.

ZUNGUMZA NAYE KUHUSU HOFU YA MUNGU
Jenga mazingira ya mwenzi wako kuogopa Ukuu wa Mungu. Jambo hili linawezekana ikiwa utamsisitiza au kumrejesha katika Mamlaka ya Mungu kiimani. Mweleze kuwa kwenda kinyume na matakwa yake ni rahisi ndoa kubaki bila uangalizi, mwishowe shetani kuingiza mafarakano.

Mhimize kufanya Ibada, tengeni muda wa kusali/kuswali/kuomba dua pamoja kabla ya kulala na kuamka. Mweleze mustakabali wa ndoa yenu uko mikononi mwake, utakuwa umemjenga sana.
Kumsisitiza kuhusu kuwa karibu na Mungu, kwake litakuwa jambo jema na utakuwa umejiongezea thamani kwake. Atajua kwamba yupo na mtu makini ambaye akili yake inafanya kazi sawasawa na mwenye hofu juu ya aliyemuumba.

Amini usiamini kwa njia hii utakuwa umejiweka mbali na usaliti maana angalau utakuwa na mwenzi ambaye unajua anaamini katika imani yake sawasawa na ni mwoga wa kukosea.

SUALA LA MAGONJWA
Mustakabali wa ndoa yenu, hauwezi kuwa mzuri kama magonjwa hatari yakiingia. Ukimwi ni tishio, tenga muda wa kuzungumza naye ‘seriously’ kuhusu hili.

Elewa kwamba kwa kumweleza kuhusu hatari ya maradhi ndani ya nyumba, si kama utakuwa unamtisha, lakini utakuwa unampa ukweli ambao unaonekana wazi.
Suala la maradhi ya kuambukiza kwa njia ya ngoni si jambo la kufumbiwa macho, ni lazima lijadiliwe kwa mapana na nafasi kwa wanandoa. 

Kuzungumza naye juu ya hili kutamfanya kwanza aamini kwamba hata wewe upo salama na unajua unachokifanya hivyo, ikiwa yatatokea ya kutokea, yeye ndiye msababishaji. Kwa vyovyote vile hakuna anayependa kuonekana kuwa yeye ndiye aliyesababisha matatizo ndani ya nyumba, hivyo utakuwa umesaidia kumuweka kwenye hofu ya uaminifu.

Hii itakuwa hatua nyingine yenye faida kwako. Kumbuka lengo kuu ni kuhakikisha kwamba husalitiwi na mwenzi wako anakuwa mali yako peke yako. Tuendelee kujifunza.

JUU YA WATOTO
Matokeo ya familia isiyo na masikilizano ni mwanzo wa mwisho mbaya wa watoto, usaliti husababisha mafarakano ndani ya nyumba na hapo sasa ndipo mtakapoanza kuingia kwenye hatari ya kuwatumbukiza watoto kwenye matatizo.
Hili mnapaswa kulijadili kwa kina. Zungumza naye sana juu ya mipango mbalimbali ya wanenu. Onesha unawapenda na wanahitaji sana msaada wenu kama wazazi.
Kuzungumzia kwako watoto, kutampa nguvu kwamba yupo na mwenzi sahihi anayetumia muda wake kufikiria familia yake. Hilo litadizi kumfanya aachane na mawazo ya usaliti kwa sababu ana uhakika yupo na mwanamke sahihi. Kama ndivyo, akatafute nini nje?

TAMAA
Tamaa ni kati ya mambo yanayosababisha usaliti unaozaa nyumba ndogo baadaye. Msisitize juu ya tamaa na umtake awe na uvumilivu na mambo msiyo na uwezo nayo.
Huu ni ushauri, lakini ukiutoa kwa kumaanisha, unaweza kujenga kitu fulani kichwani mwake na akajikuta hashawishiki kirahisi kwa tamaa ndogondogo.

KUNA USALITI WA BILA KUKUSUDIA?
Wapo rafiki zangu ambao wanaweza kunishangaa kwa kuuliza kama kuna usaliti wa bila kukusudia. Ukweli ni kwamba upo. Kama ilivyo kuua bila kukusudia, pia kuna usaliti bila kukusudia.
Usaliti huu hufanyika kutokana na mhusika kujenga/kujengewa mazingira ya kufanya hivyo. Epuka kuwa karibu na mtu ambaye mna jinsia tofauti. 

Usiruhusu mazoea sana hasa ya kuchat au kuwa naye sehemu tatanishi. Jiheshimu na uwe mtu wa mipaka. Anayetakiwa kukuzoea sana ni mke/mume wako tu.

Kuna baadhi ya watu wanakuwa na ukaribu au utani na watu wa jinsia tofauti. Mazoea yanapozidi huweza kukuingiza kwenye matatizo. Kamwe usipende kuwa na utani usio na maana na mtu wa jinsia nyingine.
Unaweza kujikuta umeingia kwenye matatizo na mwisho wake ukabaki unajilaumu tu wakati unaweza kupingana na tatizo hilo. Amini usiamini, inawezakana kabisa kukaa mbali na usaliti.

Kwanza jijenge wewe mwenyewe halafu mfundishe na mwenzako. Kufanya hivyo kutakufanya uishi maisha ya amani na furaha katika ndoa yako. 

Mada imeisha. Wiki ijayo nitakuwa hapa kwa mada nyingine nzuri zaidi, NAWAPENDA SANA!
GPL

No comments: