ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 11, 2013

Mvutano mkali umeibuka Mahakama Kuu ya Zanzibar

Mwandishi Wetu, Mwananchi
Zanzibar: Mvutano mkali umeibuka Mahakama Kuu ya Zanzibar katika kesi ya mtu anayedaiwa kumuua kwa kumpiga risasi Padre Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Zanzibar.
Upande wa mshitaka na upande wa utetezi katika kesi hiyo inayomkabili Omar Mussa Makame (35) ulivutana kwa hoja mbele ya Jaji Mkusa Sepetu katika Mahakama hiyo iliyopo Vuga mjini hapa.
Upande wa mashitaka ukiongozwa na ofisa kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Abdalla Mgongo ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kwa hiyo kuomba ipangwe siku nyingine.
Lakini, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Abdalla Juma ulidai kuwa una uhakika kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na hivyo kutaka kesi hiyo isikilizwe au mteja wao aachiwe.
Alidai kwamba hawamuombei dhamana mteja wao kwa vile kesi ya aina hiyo haina dhamana, lakini wanataka aachiwe hadi pale upande wa mashitaka utakapokamilisha upepelezi wake na kufungua kesi mpya.
Alidai kwa mteja wao kuendelea kukaa ndani ni kumnyima haki zake za binadamu na kuiomba Mahakama ioneshe meno kwa kumuachia huru mteja wao.
Jaji Mkusa baada ya kusikiliza pande zote mbili aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 21 mwaka huu atakapotoa maamuzi yake.
Omar aliyegombea ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF) Jimbo la Mlandege katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 alitiwa mbaroni Machi 17 mwaka huu.
Padre Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi Februari 17 mwaka huu wakati akienda kuongoza ibada ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Teresia liliopo Beit el Raas nje kidogo ya mjini hapa.
Mwisho
Masanja Mabula, Mwananchi
Pemba: Jumla ya miradi tisa yenye thamani ya shilingi 142 milioni imezinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru na kiongozi wa mbio hizo kitaifa, Juma Ali Simai katika Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba .
Akisoma risala kwa kiongozi wa mbio za Mwenge, Ofisa Tawala Wilaya ya Micheweni, Ahmed Khailid Abdalla alisema miradi hiyo ni ile iliyoibuliwa na wananchi na Serikali lenye lengo la kukabiliana na hali ya umaskini na kujiongezea kipato katika familia zao na taifa kwa ujumla .
Ofisa Tawala alisema kuwa katika kutekeleza shughuli za maendeleo katika Wilaya hiyo , ikiwemo suala la kuhifadhi mazingira kwa kuwashajiisha wananchi kupanda miti kwenye maeneo yao na kusimamia suala la utoaji wa elimu dhidi ya Ukimwi .
Akizindua miradi hiyo , kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, Juma Ali Simai aliwataka wananchi kutokubali kugawanywa kwa misingi ya kidini , kisiasa na kikabila bali washirikiane katika shughuli za kujiletea maendeleo .
Alisema kuwa Serikali zote mbili ya Muungano na Ile ya Mapinduzi zimekuwa zikchukua hatua za makusudi za kuwaunganisha wananchi kwa kutoa fursa ya kuuanzisha vikundi vya ushirika vya ujasiriamali na kuwataka kuitumia fursa hiyo kwa kuanzisha miradi ili waweze kuinufaika na mikopo inayotolewa na serikali zao .
Simai aliwataka vijana kujiepusha na vitendo viovu ambavyo vinaweza kuharibu maisha yao kwa kutojiunga na vigenge vya watumiaji wa dawa za kulevya .
Miongoni mwa shughuli ambazo zimefanywa Wilaya ya Micheweni ni upandaji wa miti , uzinduzi wa kituo cha tiba ya mifugo , uzinduzi wa daraja , ufungaji wa mafunzo ya taaluma ya Ukimwi na dawa za kulevya , kuweka jiwe la msingi kwenye nyumba ya bei nafuu , kuzindua kikundi cha uchomaji wa vyuma , uwekaji wa jiwe la Msingi katika shule ya Mgogoni na kukagua shamba la mkulima Masumbuko .

No comments: