ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 11, 2013

PONDA ALIPUKA ASEMA MKAKATI WA KUKAMATWA KWAKE ULIANDALIWA



Sheikh Ponda Issa Ponda
SIKU moja baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mjini Dar es Salaam, kumwachia na kumweka chini ya uangalizi wa mwaka mmoja Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, jana aliibuka na kusema umefika wakati wa Waislamu kufanya uamuzi mzito.
Akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu, baada ya swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Mtambani, Dar es Salaam, Sheikh Ponda, alisema hatua ya yeye kuwekwa ndani kamwe haitamkatisha tamaa na kurudi nyuma katika mapambano ya madai ya Waislamu nchini.

Alisema kutokana na hali hiyo, kwa muda mrefu Waislamu wamekuwa wakinyanyaswa kinyume cha sheria, wakati wana madai ya msingi ndani ya taifa lao. Alisema hatua yeye kukamatwa, ni wazi ilikuwa ni mkakati maalum unaoratibiwa na Serikali, wenye lengo la kuwafunga midomo masheikh wa Kiislamu ili wasiseme jambo lolote ambalo ni manyanyaso kwa jamii yao.

“Ni wazi hivi sasa, hawa wenzetu wanapigana nasi kitaalamu kwa kutunyamazisha midomo, kamwe hatuwezi kurudi nyuma. Hali ya Waislamu ni nzito na tunahitaji kufanya maamuzi mazito.

“Ni wazi kabisa, ninataka kulisema hili lieleweke kuwa Uislamu wetu hauko kwa ajili ya Katiba, wala Utanzania wetu, bali ni kwa ajili ya asili ya dini yetu tu.

“Kwa muda mrefu, walikuwa wakifanya mikakati ya kunishughulikia eti sio raia wa Tanzania, niliwajibu wazi pale Mtoni kuwa hakuna mtu yeyote wa kuniweza kuninyang’anya. Na sasa wamebadili mfumo wa kutushughulikia masheikh kwa kesi za uongo.

“Ninataka kuwaambieni ndugu zangu, Waislamu hatutarudi nyuma, iwe katika amani au mapambano, ili mradi tu tuweze kuisongesha mbele dini ya Allah (Mwenyezi Mungu),” alisema Sheikh Ponda.

Maisha ya gerezani
Alitumia mkusanyiko huo, kusimulia maisha aliyokumbana nayo katika gereza la Segerea.

Alisema aliweza kushuhudia mambo mengi, yakiwamo ya watu wengi kuwekwa mahabusu bila kesi zao kushughulikiwa.

“Waliponikamata walinipeleka katika gereza la Segerea na kuniweka selo ya watoto, ambapo alikuja mtoto mdogo ambaye nilimuhoji na kusema ana umri wa miaka 10. 

“Katika hali ya kushangaza, mtoto yule alisema amewekwa ndani kwa sababu ya tuhuma za kuiba pochi iliyokuwa na Sh 40,000.

“Kama iliwezekana kwa mtoto huyo kukamatwa, imekuwaje kwa mtoto aliyekojolea Koran pale Mbagala Oktoba 10, mwaka jana, hadi leo hajakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Leo hii, kwa mujibu wa takwimu zetu zinaonyesha magereza mengi na makaburi nchini yamejaa masheikh ambao kila mara wamekuwa wakifikwa na madhila ya kesi za kusingiziwa.

“Leo kina Sheikh Farid, Mselem hadi leo hii maskini ya Mungu wamewekwa ndani kwa kesi za kusingizia tu, ila Mbeya yametokea machafuko kati ya Wakristo ambao walichoma msikiti, lakini hadi leo hii hakuna hata kiongozi aliyefikishwa mahakamani.” 

Wakati akiyasema hayo, waumini wa dini ya Kiislam kila mara walikuwa wakikubaliana na maelezo yake kwa kutamka ‘Takbir ... Takbir’ neno lenye maana kwa lugha ya Kiarabu ‘Mungu mkubwa’.

Juzi Mei 9, mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimtia hatiani Sheikh Ponda na wenzake 49, ambao waliachiwa huru katika kesi iliyokuwa ikiwakabili. 

Washtakiwa hao, waliachiwa huru na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Victoria Nongwa.

Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka na upande wa utetezi uliwakilishwa na Wakili Yahya Njama.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Nongwa alisema: “Jamhuri imeshindwa kuthibitisha mashtaka kuanzia shtaka la kwanza, tatu, nne na la tano kwa washtakiwa wote, katika mashtaka hayo washtakiwa wote kuanzia wa kwanza hadi 50 hawana hatia.

“Katika shtaka la pili la kuingia kwa nguvu katika Uwanja wa Markaz Chang’ombe, upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha kwamba Ponda aliingia kwa nguvu, hivyo anatiwa hatiani kwa kosa hilo.

“Shtaka la kuingia kwa nguvu halielezi adhabu inayostahili kutolewa, lakini mahakama inaweza kumpa adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela au faini au vyote kwa pamoja.

“Kwa mshtakiwa wa kwanza (Ponda) hakuna kumbukumbu kwamba ni mkosaji wa makosa mengine… mahakama inazingatia pia mshtakiwa alikaa rumande kwa muda mrefu kuanzia Oktoba 18 mwaka jana hadi leo, hivyo inamwachiwa kwa masharti.

Alisema mahakama inamwachia Ponda kwa masharti ya kulinda amani, awe mwenye tabia njema kwa miezi 12 na endapo atashindwa atarudi mahakamani apewe adhabu nyingine inayostahili.

MTANZANIA

No comments: