Advertisements

Friday, May 3, 2013

Spika akanusha kupokea ripoti ya Jairo

DAVID JAIRO
By Halima Mlacha, Dodoma
SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, amekanusha ofisi yake kupokea rasmi ripoti ya kuchunguza tuhuma zinazomkabili aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini David Jairo, na kuiacha iozee mikononi mwake.

Amekanusha jana bungeni baada ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, kuomba mwongozo, akinukuu moja ya magazeti ya kila siku (si HabariLeo), lililoripoti kuwa ripoti hiyo imewasilishwa kwa Spika na inaozea mikononi mwake.

Mnyika alisema katika swali lake alilomuuliza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Alhamisi iliyopita, alihoji juu ya kuwasilishwa rasmi kwa ripoti hiyo na kujibiwa na kiongozi huyo kuwa haijawasilishwa kwa Bunge.
“Sasa leo (jana) nashangaa kwenye gazeti hili (akilionesha), limeandika Serikali yakamilisha ripoti yake, Bunge lachambuliwa kama karanga, Ripoti yaozea mikononi mwa Spika, Serikali yakumbushwa ya Richmond, hapa ukweli ni upi?,” alihoji Mnyika.

Alisema endapo ni kweli ripoti hiyo ya Jairo, imewasilishwa kwa Spika na kuozea mikononi mwake, hatua hiyo haitendei haki Bunge kwa kuwa ilitakiwa iwasilishwe bungeni na kujadiliwa na wabunge.
Alisema na kwa mujibu wa gazeti hilo, ripoti hiyo imelichambua Bunge kama karanga, hali ambayo Mnyika alisema haijatoa haki kwa wabunge, kwani walipaswa kuambiwa ukweli na kupewa nafasi ya kuijadili.
Akijibu mwongozo huo, Makinda aliikataa hoja hiyo na kusema Bunge hilo halijawahi kufanyakazi yake kwa kutegemea magazeti.

“Kwanza siikubali hoja hii, mimi kama Spika sina taarifa hizo za kupokelewa kwa ripoti ya Jairo ofisini kwangu, lakini pia siwezi kufanyakazi na magazeti, tena haya magazeti ambayo mara nyingi yanaandika uongo mtupu,” alisisitiza Makinda.

Jairo alituhumiwa kuchangisha taasisi zilizopo chini ya wizara yake Sh milioni 85, kwa madai kuwa alikuwa anahonga wabunge ili wapitisha bajeti ya wizara hiyo katika mwaka wa fedha wa 2011/2012.
Mnyika katika swali lake wiki iliyopita, alitaka kufahamu sababu za Serikali kutowasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio yaliyotokana na taarifa ya Kamati Teule ya Bunge.

Alitaka kufahamu pia ni kwa nini waliotakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria, haijatekelezwa. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alikiri Serikali kuzembea katika kutoa mrejesho kuhusu suala hilo na kusema kuwa sehemu kubwa ya maazimio hayo yamefanyiwa kazi.


Habari Leo Gazeti

No comments: