ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 3, 2013

Kampeni za udiwani ; Kiongozi CCM mbaroni kwa kutishia bastola

Arusha. Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM, Wilaya ya Arusha, Victor Mollel anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kuwatishia kwa bastola wafuasi wa Chadema wakati wa mkutano wa kampeni za udiwani Kata ya Themi.

Mbali na Katibu huyo, pia Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM), Kata ya Engutoto, Joseph Laizer naye anashikiliwa kwa madai ya kuwatishia kwa shoka wafuasi hao katika vurugu hizo.

Katika tukio hilo, viongozi hao wa CCM wanatuhumiwa na viongozi wa Chadema kuwa walivamia mkutano wa kampeni katika eneo hilo la Kambarage, Kata ya Themi ambako Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alikuwa akimnadi mgombea wa udiwani, Melance Kinabo.

Viongozi hao walikamatwa juzi usiku mara baada ya mkutano huo na kuwekwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha na kufunguliwa majalada. Jalada la Laizer katika taarifa ya Polisi, ni namba AR/RB/6937/2013 na Mollel ni taarifa ya polisi yenye namba AR/RB/6938/2013.

Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM wilayani Arusha, Gasper Kishimbua alisema mtu mmoja amejeruhiwa katika vurugu hizo na kudai kuwa chanzo ni Chadema kupita karibu na mkutano wa CCM na kufanya fujo.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Dk Wilfred Soileli na Laizer walikanusha viongozi wa CCM kuvamia mkutano wa Chadema na kusema wao ndiyo waliovamiwa.

Dk Soileli alisema imekuwa ni kawaida kwa wafuasi wa Chadema kuwashambulia wafuasi wa CCM kila wanapopita karibu na mikutano yao.

“Huu ni uhuni, tunashangaa viongozi wetu kushambuliwa na baadaye kufunguliwa kesi, Victor hata hakuwepo kwenye mkutano alikwenda Polisi kumsaidia Laizer lakini ameunganishwa eti kafanya fujo kwenye mkutano, tumewawekea dhamana na tunaamini haki itatendeka,” alisema.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alishindwa kuelezea tukio hilo kwa kina akisema alikuwa kwenye msafara wa kiongozi wa kitaifa.

“Naomba unipigie baadaye nitakupa maelezo, nipo kwenye msafara wa kiongozi,” alisema Sabas.
Hata hivyo, alipopigiwa tena simu baadaye hakupokea.

No comments: