Wednesday, June 5, 2013

MUDA WA USICHANA NI MFUPI, JIPANGE!-2


UNAWEZA kusoma kichwa cha mada hii ukaona cha kawaida tu lakini ukituliza ubongo wako, utagundua kilichoandikwa hapo juu ni kizito sana kwa maisha ya wanawake.

Kwa bahati mbaya sana, wengi hawapati nafasi ya kujifunza mambo muhimu kama haya lakini kwa sababu wewe umepata nafasi hii ni vyema ukaitumia vyema.
Usidanyike dada yangu, mwanaume anaweza kuoa hata akiwa na zaidi ya miaka 40 tena akaoa ‘mtoto’ mdogo mwenye miaka 22 ila kwa mwanamke ni vigumu. Huu ndiyo ukweli.
Tuendelee na somo letu.

KWANZA WAZAZI
Wazazi ni mashuhuda wa kwanza kuhusu ninalozungumza hapa. Ni kweli kuna wakati wasichana huzaa nyumbani kabla ya ndoa ila kwa kipindi cha kuanzia miaka ya 2000 idadi imeongezeka.
Ni vizuri wazazi kwa pamoja mkaamka na kuwapa mabinti zenu elimu bila kificho kuhusu suala zima la mapenzi. Hakuna haja ya kuwaficha, maana ukinyamaza ndiyo tunawapoteza.
Wenyewe wakikutana huko kwenye mitandao ya kijamii wanazungumza kila kitu kwa uwazi. Wapeni elimu watoto wenu. Kama una binti ana umri wa miaka 15 usiendelee kuamini ni mdogo, mfundishe.
Mweleze athari za kuingia kwenye mapenzi mapema. Mfundishe namna ya kujiandaa kuwa mama bora hapo baadaye. Mpe mifano, mwelekeze faida za kuwa mama ndani ya ndoa na si mama wa nyumbani tu!

WALIMU
Kwa upande wa walimu hawana tofauti kubwa sana na wazazi. Tena hawa ni wazazi wa karibu zaidi kwa sababu wanakaa na watoto muda mrefu zaidi shuleni.
Wekeni aibu pembeni, zungumzeni na wanafunzi kwa uwazi kwa sababu wanawaamini na kuwaogopa. Tumieni lugha ya kirafiki na muwafanye wajitambue. Watoto siku hizi wanaharibika wakiwa na umri mdogo sana.
Ni vyema walimu wakatenga muda wa kuwafundisha watoto kujitambua (angalau kuanzia wa darasa la tano na kuendelea) kulingana na umri wao. Mkiwaelekeza hawatadanganyika maana kila kitu watakuwa wameshakijua.

CHAGUA MARAFIKI
Wewe msichana unayesoma hapa, achana na kampani za marafiki wabaya. Usizoeane na mtu ambaye tabia zake mitaani, shuleni au kazini kwako siyo nzuri.
Kaa mbali na marafiki wabaya. Hawana faida kwako zaidi ya kujiweka karibu na hatari ya kuingia kwenye kuharibu usichana wako. Wengi huharibika kwa kufuata mkumbo. Tafuta marafiki wanaojitambua na wenye tabia njema.

KATAA MAJARIBIO
Kuna baadhi ya wasichana wanadanganyika na wanaume wanaowaambia kwamba eti wawazalie kwanza ndipo wawaoe. Usidanyike na uongo wa aina hii. Wewe si mwanamke wa majaribio. Kama ni vipimo vipo hospitalini. Si mwilini mwako.
Akikuzalisha na kukuacha itakuwaje? Usikubali kuingia kwenye mtego wa aina hii. Kuna mwingine anakuwa na mwanaume halafu eti anapata mimba bila kujua. Hilo ni tatizo.
Kwa nini uishi kwa bahati mbaya? Kwa nini usijilinde kwa kutumia kinga? Hata kama mmepima na kugundulika mpo salama, vipi kuhusu mimba? Hata kalenda nayo hujui?
Mwanamke ndiye mwenye nafasi kubwa zaidi ya kuzuia mimba. Lazima uwe na ufahamu na umakini wa hali ya juu. Hisia zako zisikuponze.
Usikubali ‘bahati mbaya’ yako ya siku moja ikaharibu maisha yako yote. Kuwa makini maana starehe ya muda mfupi tu inaweza kuharibu maisha yako na mwanaume huyo akaendelea na mambo yake.

UMRI WA KUZAA
Mwanaume anapaswa kujituliza ili apate mtu sahihi wa kuingia naye kwenye ndoa katika umri ulio sahihi. Kwa mfano msichana akiingia kwenye ndoa akiwa na zaidi ya miaka 30 ni tatizo.
Hebu jiulize, atazaa na kuwatunza watoto wake kwa muda gani? Kwa maneno mengine, mwanamke atakayeolewa na miaka 32 (kwa mfano) atakuwa na nafasi ya kuzaa mtoto mmoja tu (maana wataalamu wa afya ya uzazi wamefafanua kwamba, kuanzia miaka 36, mwanamke anakuwa kwenye hatari akiwa mjamzito).
Kama ndivyo, ikiwa amezaa akiwa na miaka 32 inamaana kuwa, mwanaye akiwa darasa la kwanza (kama ataanza akiwa na miaka sita) yeye atakuwa na miaka 38 na akimaliza la saba, atakuwa na umri wa miaka 45 wakati mtoto atakuwa na miaka 12.
Kwa hesabu hizo, mwanamke huyo akiwa na miaka 52 (kwa siku hizi ni bibi tayari) mwanaye atakuwa anamaliza kidato cha sita akiwa na miaka 19 (bado elimu ya chuo). Huyu ni mtoto wa kwanza!
Kumbe basi, mwanamke huyo angekuwa ameingia kwenye ndoa angalau akiwa na miaka si zaidi ya 25 anakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuzaa kwa nafasi, mpishano sahihi na kulea watoto wake vizuri.

JIPANGE SASA
Naamini yote hayo ni elimu tosha kwako. Bila shaka kuna kitu kimeingia ubongoni mwako. Ni vyema basi ukajipanga kutoka sasa, bado hujachelewa.
Kuwa na msimamo katika maisha yako. Msingi wa hili ni kugundua njia iliyo sahihi na kuifuata. Mada imeisha, wiki ijayo nitakuwa hapa na kitu kingine kipya kabisa, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers, ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

3 comments:

Anonymous said...

sikubaliani na msemo huu hata kidogo kwamba eti mwanamke ndo akifika umri wa miaka 40 tabuu kuolewa mwanamme yeye anaweza kuowa kajisichana kadogo kadogo si kweli mimi nimefika umri huo tena katika umri huo ndo naolewa na nimeshaazaa watoto triple(watatu) mmoja wa kike na wawili wa kiume na kwa umri wangu utashanga mwenyewe kuana wanaume wadogo wadogo wananitongoza na nawatolea nje kuwambia wanaiheshimu mimi mke wa mtu na wengi wanajua nina mume laki basi tuu utoto wao ndo unao watuma

so si kubaliani na hilo riski hutoa mungu na maisha ndo aliyokupangia mungu binadamu unaweza ukapanga na mungu akakupangulia so cha muhimu ni kuomuomba yeye tu peke ndo ajuaye maisha yetu

Anonymous said...

Dada umenena, unakunywa nini?.

Anonymous said...

nakunywa soda ya fanta je utaninunulia? ukisha nunua nilite brooklyn new york okay