Advertisements

Wednesday, July 17, 2013

Azam yazipa Yanga, Simba shilingi Mil 280

Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage.
Na Saleh Ally
UONGOZI wa kampuni ya Bakhresa inayomiliki klabu ya Azam umemwaga dola milioni moja (zaidi ya Sh bilioni 1.6) ili kupata haki ya udhamini wa Ligi Kuu Bara kama warushaji wa matangazo ya televisheni.

Kutokana na kumwaga fedha hizo, kampuni hiyo kupitia kituo chake kipya cha televisheni yake ya Azam TV, kitakachoanza kurusha matangazo hivi karibuni, kitapewa haki ya kuonyesha mechi zote za Ligi Kuu Bara. 
Kampuni hiyo iliyokuwa inapambana na Supersport ya Afrika Kusini iliyokuwa tayari kutoa dola 500,000 imeihakikishia bodi ya ligi hiyo kuwa iko tayari kutoa fedha hizo na kila klabu zikiwemo Yanga na Simba zitapata Sh milioni 140 kila moja kwa msimu.
Pamoja na fedha hizo kutoka kwa wamiliki hao wa Azam FC ambayo ndiyo wapinzani wakubwa wa Simba na Yanga, klabu hizo kongwe zimesema zinataka kulipwa zaidi kwa kuwa ndiyo zenye mashabiki wengi.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji.

Katika kikao kilichofanyika juzi, kumezuka mjadala mkubwa huku Simba na Yanga zikisisitiza kwamba haitakuwa haki zenyewe kupewa Sh milioni 140 sawa na klabu nyingine ambazo zina mtaji mdogo wa mashabiki.
“Lakini watu wa bodi ya ligi wameonyesha kutokuwa waungwana maana wameendelea kulazimisha Simba na Yanga zilipwe sawa na klabu hizo ndogo. Sisi tunaona hii si sahihi,” kilieleza chanzo cha uhakika.

Chanzo kingine kimeeleza, uamuzi huo wa kampuni ya Bakhresa kupewa nafasi kulikuwa kunapingwa ‘kiana’ na watu wa klabu hizo kubwa bila ya kujali inatoa fedha nyingi mara mbili ya SuperSport kwa madai eti ni kubwa na wataonekana nchi nyingi.
Lakini wajumbe wengine walisisitiza suala la fedha lipewe kipaumbele na fedha nyingi ndiyo zichukuliwe, hapo ndipo kukaibuka suala la mvutano wa Yanga na Simba kutaka kupewa zaidi.
Taarifa zinaeleza tayari ufungaji wa mitambo ya Azam TV inaendelea kwa kasi ya ‘kimondo’ na baada ya siku kadhaa itaanza kazi huku ikitumia mitambo ya kisasa zaidi nchini. Kwa hisani ya GPS

No comments: