ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 12, 2013

JINSI YA KUGUNDUA NA KUANZISHA UHUSIANO ULIO SAHIHI!-3

TUNAENDELEA na somo letu la namna ya kugundua na kuanzisha uhusiano ulio sahihi. Nafarijika moyoni nikiamini somo linaeleweka vizuri. Kuingia kwenye uhusiano usio sahihi kunaweza kusababisha matatizo mengi.
Wiki iliyopita nilikazia zaidi katika eneo la namna ya kugundua kama mpenzi wako anakupenda. Kigezo cha uzuri wa sura, maumbile n.k siyo kipimo cha mapenzi ya kweli.

Hiyo ni kwa sababu vivutio hivyo vinaweza kuharibika au kuondoka kabisa wakati wowote lakini penzi la dhati lipo moyoni na kamwe haliwezi kuondoka. Tuendelee na vipengele vingine.

CHUNGUZA HISTORIA YAKE
Hapa sasa unatakiwa kuifahamu historia yake ya kiuhusiano. Hii ni baada ya kuingia katika uhusiano ila kumbuka katika kipindi hiki cha mwanzo, hushauriwi kumpa moyo wako kwa asilimia zote! Fanya hivi, toa asilimia 40 kwanza, zilizobaki fanya uchunguzi taratibu. Unaweza kufahamu historia yake ya uhusiano kutoka kwake ikiwa ana ushirikiano wa kutosha.

Kitu cha kufanya ni kumwuliza alikuwa na nani kabla yako na kwa nini aliachana nao. Kuna wengine huwa wanashindwa kusema ukweli katika hili lakini ikiwa atakuambia ukweli itakuwa rahisi kwako kujua vitu anavyovipenda na asivyovipenda.

Kubwa zaidi ni kwamba itakuwa rahisi kwako kujua kwamba mpenzi huyo atakufaa au hatakufaa kutokana na makosa yaliyosababisha kuachana na wapenzi waliotangulia.

Ukiona hujaridhika na historia yake, unaweza kutumia watu unaowaamini, wanaomfahamu vizuri. Katika hili lazima uwe makini sana, jitahidi asifahamu kwamba unamchuguza! Kwa kufahamu vizuri historia yake, kutakusaidia kufanya maamuzi sahihi na kuingia katika uhusiano safi usio na dalili za kukusababishia mateso hapo baadaye.

JIELEZE SAWASAWA
Kuna baadhi ya watu wana tabia ya kutoeleza ukweli juu ya tabia zao. Hili ni kosa. Ni vizuri unapoingia katika uhusiano na patna mpya, akajua ulivyo.

Huna haja ya kuficha, jieleze sawasawa ulivyo na aina ya vitu vinavyokuvutia na vile usivyovipenda. Hii itamsaidia kukufahamu na kwenda vile unavyopenda.

Hata hivyo, wakati ukijieleza ulivyo na mambo unayopenda ni vizuri pia ukajua kwa undani vitu asivyovipenda. Kwa kufanya hivyo itasaidia sana kumtambua mwenzi wako na kuepuka migongano katika uhusiano wenu.

Kwa hakika ukigundua vitu hivyo, uhusiano wako utakuwa mzuri na usio na migogoro. Hata hivyo ni vyema kuendelea kumchunguza mwenzako kila siku ili ukiingia kwenye ndoa iwe ndoa iliyo sahihi isiyo na majuto. Hebu sasa tuangalie upande mwingine, ndani ya uhusiano kabisa.

No comments: