Vatican City. Papa Francis, amewatakia Waislamu wote duniani, sikukuu njema ya Eid el- Fitr huku akiwahimiza kuheshimiana zaidi kupitia elimu.
“Mwaka huu wa kwanza kama kiongozi wa Kanisa Katoliki, nimeamua kutuma ujumbe huu kwenu marafiki zangu Waislamu nikiwa na heshima kubwa. Ninatambua uhusiano, udugu na urafiki baina yetu sisi,” alisema Papa Francis katika salamu zake.
Makao ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani, yameulezea waraka huo kuwa ni wa salamu maalumu za Sikukuu ya Eid al-Fitr inayofanyika duniani leo, baada ya kumalizika kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
“Ujumbe wangu katika mwaka huu ni kuwataka nyote kuakisi kwa pamoja matendo yetu ya kiimani kama Waislamu na Wakristo na kukuza ushirikiano na kuheshimiana,” alisema Papa Francis.
Ameongeza: “Kuhusu elimu kwa waumini wetu vijana wa Kiislamu na Kikristo, hatuna budi kuwalea na kuwakuza wakifikiri na kuzungumzia namna nzuri ya kuheshimiana katika imani za wenzao na waumini wao na kuepuka tabia ya kudharau au kubeza imani na mafundisho ya wengine.”
Kwa kawaida salamu hizo hutolewa na Vatican kupitia Baraza la Kipapa la Mijadala ya Kiimani, lakini safari hii Papa Francis ameamua kutuma salamu hizo mwenyewe tangu alipofanya hivyo Papa Yohane Paul II mwaka 1991.
Papa Francis aliendelea kueleza, “Kuhusu kitu gani tunatakiwa kuheshimana kama binadamu ni maisha, utu wa mtu na kupatikana kwa heshima na haki ya mtu.”
Papa Francis alisema watu wa imani mbili tofauti hawana budi kuheshimiana.
Ili kufikia azma hiyo familia, shule, mafundisho ya kidini na aina zote za vyombo vya habari vina wajibu wa kushiriki.
“Tunafahamu kuwa heshima ya mtu ni ya msingi katika uhusiano wowote wa binadamu, hasa kati ya watu ambao wanakiri imani za kidini. Kwa maana hii, kwa moyo wa dhati, tutakuza urafiki wetu.”
Kiongozi huyo wa waumini bilioni 1.2 duniani alisema kutakiana mema wakati wa sikukuu ni kuheshimiana, ingawa si kukubaliana kwa kila jambo linalofanyika kwenye imani nyingine.
“Tunashiriki nao katika furaha, hatuzungumzii imani na mioyo yao,” alisema.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment