ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 11, 2013

Siri ya uvamizi wa Navy SEAL Somalia yabainika

Navy SEAL ni kikosi maalumu cha askari wa Marekani ambacho hutumwa kutekeleza oparesheni maalumu ikiwemo kuwakamata watuhumiwa maalumu wa kimataifa ambao wamekuwa wakitafutwa kwa muda mrefu.
NAIROBI, Kenya
Imebainika kwamba mtu aliyekuwa akitafutwa na kikosi maalumu cha Navy SEAL mwishoni mwa wiki ni raia wa Kenya ambaye alipanga kuvamia ofisi za Bunge na ofisi za Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Nairobi.
Kwa mujibu wa taarifa za kiusalama kutoka Serikali ya Kenya, kikosi hicho cha askari maalumu wa Marekani kilikuwa kikimtafuta mtu huyo usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita, lakini walishindwa kumnasa baada ya kukutana na upinzani mkali kutoka kwa wapiganaji wa Al Shabaab.
Navy SEAL ni kikosi maalumu cha askari wa Marekani ambacho hutumwa kutekeleza oparesheni maalumu ikiwemo kuwakamata watuhumiwa maalumu wa kimataifa ambao wamekuwa wakitafutwa kwa muda mrefu.
Taarifa hiyo ilimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Abdulkadir Mohamed Abdulkadir ambaye pia hufahamika kwa jina la Ikrima, kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na AP.
Askari wa kikosi hicho maalumu waliripotiwa kushindwa kutimiza lengo la kumnasa mtuhumiwa huyo kama ilivyopangwa, kwa mujibu wa mmoja wa maofisa ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Kwa mujibu wa ripoti ya ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa la Kenya, Abdulkadir ni mtu anayetajwa kuwa kiongozi wa kupanga mashambulizi yote ya kigaidi akipata maelekezo kutoka kwa wakuu wa Al Qaeda huko Pakistan ambaye amekuwa akisimamia mashambulizi yote yaliyofanyika Kenya kati ya mwaka 2011 na mwanzoni mwa mwaka 2012.
AP ilieleza kwamba mashambulio kadhaa miongoni mwa hayo yaliyokuwa yamepangwa na Al Shabaab yaliweza kuvurugwa kabla hayajatekelezwa.
Taarifa hiyo iliyotolewa kwa shirika la habari la AP na mengine kadhaa ilikuwa ikieleza mikakati ya baada ya uvamisi wa jengo la kibiashara la Westgate Mall mjini Nairobi uliofanywa na wapiganaji wa Al-Shabaab Septemba 21 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 60, huku mwanamama raia wa Uingereza, Samantha Lewthwaite maarufu kama ‘White Widow’ akitajwa kuhusika.
Taarifa hiyo imeeleza pia kwamba mwanamama huyo ni miongoni mwa waliokuwa wamepangwa kutekeleza uvamizi huo mpya wa ukumbi wa Bunge, ofisi za UN mjini Nairobi, Ofisi za makao makuu ya jeshi na maeneo mengine.
Pia wanadaiwa kupanga kutekeleza mauaji ya maofisa wa juu wa Serikali ya Kenya, wanasiasa na maofisa usalama.
Idara ya Usalama wa Taifa ya Kenya ilieleza katika taarifa yake ya awali kwamba kabla ya uvamizi wa Septemba 21, walipata taarifa za kuwepo kwa wanamgambo wa Al Shabaab mjini Nairobi na kwamba walipanga katika tarehe na siku isiyojulikana watavamia jengo hilo la Wastgate Mall na Kanisa Kuu la Holy Family Basilica.
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

si mnaona wenyewe ukweli unavyo jidhihiri ndo maana mtu unatakiwa utumiye akili zako tena ziwe zimetulia ndo utakuja kujua ukweli ya kila jambo linalotokea katika dunia hii chanzo chake ni nini na ukishika kamba ya mungu daima hutoponyoka ukiwa na mapepe na akili za mapepe mapepe basi utabishana na watu utakuwa huelewi si muelewa utatumiwa ufanye vitendo vya ajabu ajabu na wenye akili zao wanajua wanachokifanya.

mungu kisha sema kwenye alquran uongo hadumu daima ukweli ndo unaodumu daima na utajidhihiri.

hakuna kama mungu.