Advertisements

Tuesday, November 19, 2013

Kariakoo yazizima; Wafanyabiashara wagoma kufungua maduka


Makaduka yakiwa yamefungwa katika Mtaa wa Kongo jijini Dar es Salaama jana kutokana na wafanyabiasha kugoma ili kushinikiza Mamlaka ya Mapato kusitisha matumizi ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD). PICHA|SALIM SHAO

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa Kariakoo jijini Dar es Salaam jana walifunga maduka yao kupinga utaratibu mpya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wa kutoza kodi kwa kutumia mashine za elektroniki (EFD).
Wafanyabiashara walifanya mgomo huo ili kushinikiza kuonana na ama Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa au Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda.
Wanadai kuwa mashine hizo za EFD zinauzwa bei ghali ya kati ya Sh800,000 hadi Sh1.2 milioni, gharama ya kuzifanyia matengenezo zinapopata hitilafu ni kubwa na pia wanadai kuwa kuna harufu wa ufisadi kwenye suala hizo kwa kuwa ni kampuni chache zilizochaguliwa kuuza mashine hizo.
Maduka karibu yote hayakufunguliwa tangu alfajiri tofauti na ilivyozoeleka na hata wafanyabiashara wachache waliojaribu kufanya hivyo walilazimika kuyafunga kwa hofu ya kufanyiwa vurugu na wenzao.
Baadhi ya maduka ya vifaa vya umeme, magodoro na friji yaliyopo Mtaa wa Uhuru yalikuwa wazi lakini baada ya muda mfupi yalifungwa.
Hata hivyo, maduka yaliyoko kwenye Soko Kuu la Kariakoo yalikuwa wazi muda wote.
Mgomo huo ulianza baada ya wafanyabiashara hao kupeana taarifa wakihamasishana kutokufungua maduka yao kushinikiza kusikitishwa kwa matumizi ya mashine hizo za kukokotoa kodi.
Msimamo wa Serikali
Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alisema mgomo wa wafanyabiashara wa Kariakoo hauwezi kubadili msimamo wa Serikali wa kukusanya kodi kwa kutumia mashine za EFD. Alisema suala la bei haliwezi kuwa kigezo cha kugoma kwa kuwa baada ya kununua fedha zao zitarejeshwa kidogokidogo kwenye marejesho ya kodi.
“Changamoto iliyopo ni kwamba wafanyabiashara wengi hawajui kama fedha hizo wanazonunulia mashine watarejeshewa kwenye makato ya kodi. Hatuwezi kuzibadilisha mashine hizo kwa kuwa siyo kama simu za mkononi, zimetengenezwa kwa mfumo maalumu wa TRA,” alisema.
Aliitaka TRA kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu manufaa ya kutumia mashine hizo.
TRA yakaza uzi
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo aliwataka wafanyabiashara kuacha kutafuta mbinu za kukwepa kulipa kodi na badala yake wawe wazalendo kwa nchi yao.
“Unajua wafanyabiashara wengi wanaumia kulipa kodi, sasa wanatafuta visingizio na kufanya mbinu chafu ili kukwepa. Mbinu zao tumezigundua kwani kuna baadhi yao wanadiriki hata kusema hata wakipewa bure mashine hizo watazichoma moto,” alisema Kayombo. Alisema madai ya wafanyabiashara hao kwamba kuna upendeleo katika kutoa zabuni ya kuuza mashine hayana ukweli wowote na kusema kampuni kumi na moja zimepewa zabuni ya kuuza mashine hizo baada ya kushinda mchakato ambao ulitangazwa kwa kufuata vigezo vyote.
Kuhusu suala la bei ambalo wafanyabiashara wanasema mashine hizo zinauzwa bei kubwa ya Sh800,000. Kayombo alisema: “Tumeliona hilo na baada ya majadiliano tumepunguza bei ya mashine hizo na sasa zinauzwa Sh600,000.”
Madai mengine ya wafanyabiashara kwamba mashine hizo zinatoa majibu tofauti, Kayombo aliwataka wanaopata tatizo hilo kutoa taarifa sehemu inayohusika kwa utatuzi.
“Hebu nikuulize ndugu yangu, hivi kama nyumbani kwako umeweka umeme, ukaamka siku moja na kukuta luku haifanyi kazi, utagoma au utatoa taarifa kwa mamlaka husika?
Msimamo wa wafanyabiashara wa Kariakoo
Mshauri wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Karikaoo (JWK), Johnson Minja alisema wanataka kuzungumza na Serikali ili kupata mwafaka wa suala hilo.
“Wafanyabiashara wana malalamiko mengi siyo suala la kuanzishwa kwa mfumo wa mpya wa elektroniki pekee, bali pia wamegoma kutokana na kero mbalimbali zinazolikabili eneo hili,” alisema Minja.
“Tuliandika barua kwenda Wizara ya Viwanda na Biashara tukimtaka Waziri husika kuonana naye na kujadili juu ya kuwepo kwa kero mbalimbali kama kukithiri kwa wamachinga, uchafu na jinsi ya kutumia hizi mashine mpya za kielektroniki lakini hatujapata majibu,” alisema Minja.
Mmiliki wa maduka ya magauni ya madera, Mwinyihaji Hussein alisema wataendelea na mgomo hadi pale Serikali itakapoona kuna haja ya kukutana nao na kuzungumzia suala hilo akidai kwamba kuna harufu ya ufisadi ndani yake.
“Kwa bei ambazo mashine hizo zinauzwa unafikiri ni wafanyabiashara wangapi ambao watamudu kuzinunua?... maduka yatabaki yamefungwa hadi kieleweke,” alisema. Mfanyabiashara wa vifaa vya umeme, Jedda Hasabubaba alisema wanaitaka Serikali kuchaji kodi hiyo ya VAT bandarini na si katika maduka.
“Ule utaratibu wa mwanzo, TRA ilikuwa inavuka lengo katika kukusanya mapato kwa nini tusiendelee na mfumo huo badala ya kutumia hizi mashine za kielektroniki?
Morogoro
Mgomo huo wa wafanyabiashara wa Kariakoo umekuja baada ya wenzao wa Morogoro kufanya hivyo kwa madai yanayofanana.
Hata hivyo, walisitisha mgomo huo kwa muda kuipa nafasi Serikali kushughulikia kero zao ambazo ni kupunguza gharama ya kununua mashine hizo na tozo ya kodi ya asilimia 18.

Imeandikwa na Joseph Zablon, Hadija Jumanne na Lilian Lucas.wa Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Hili tatizo la wafanyabiashara kugoma lilionekana Mbeya pamoja na sehemu nyingine. Hivi nyinyi TRA, hasa mameneja na viongozi wa mamlaka hii hamjajifunza kutoka matatizo mliopata kule mkoani Mbeya? sio hilo tu kwa nini mnadai hela mbele ilhali mkijua kuwa MAIN GOAL NI KUPATA WAFANYA BIASHARA WENGI WANAOTUMIA MASHINE ZENU? YAANI mnaingia kwenye mgogoro wa bure hata kama ni sheria basi tafuteni mbinu mbadala za kurahisisha . Halafu huyu kiongozi wa elimu ya walipa kodi ndio HOVYO kabisa na kauli zake za reja reja