ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 27, 2013

Mtoto avunjwa kidole na mwalimu wake baada ya kuingia darasani na nywele ndefu huko Mbeya.

Wiki ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na watoto ikiwa imeanza kuadhimishwa duniani Novemba 25 mwaka huu bado vitendo hivyo vimezidi kushamiri Mkoani Mbeya ambapo mwanafunzi wa darasa la nne shule ya msingi Aiport Kata ya Iyela jijini Jacline Staniely [9] ameumizwa mkono wake wa kushoto.
Jacline akiongea kwa ridhaa ya mama yake amesema alipigwa kwa kutumia ubao na mwalimu wa shule hiyo Novemba 19 mwaka huu na mwalimu Kanyika kwa kosa la kuwa na nywele ndefu.
Mwanafunzi huyo amedai kuwa siku ya tukio alipigwa vibaya na kumsababishia maumivu makali ambapo siku hiyo mama yake alikuwa safarini Nairobi Kenya hivyo hakupata matibabu ambapo alilazimika kumwambia mwalimu jirani[Bibi]ambaye alimpeleka hospitali kutibiwa.
Picha ya X ray ikionesha kidole kilichovunjika :

Hata hivyo Jackline amesema kuwa kutokana na maumivu makali alilazimika kufanya mtihani wa Taifa wa darasa la nne bila kupata matibabu ya kutosha.
Baada ya kurejea kutoka safari mama yake mzazi aitwae Rehema Adamson Ndeje[28] mkazi wa Block T jijini Mbeya amesema baada ya maumivu ya mwanae usiku ilimlazimu kwenda shuleni ili kujua kulikoni,ndipo alipoonana na mwalimu Kanyika baada ya kukutanishwa na Mwalimu mkuu.
Mama Jackine amesema hicho ni kipigo cha tatu kukubwa kwa mwanae kupigwa na mwalimu huyo ambapo alionesha makovu yaliyodaiwa yalitokana na vipigo vya mwalimu huyo miguuni akidai majeraha hayo yalidumu kwa miezi mitatu.
Hata hivyo Rehema aliamua kwenda Polisi Mwanjelwa kutoa taarifa za tukio na kila alipoitwa mwalimu huyo hakutokea ndipo jalada likapelekwa kituo kikuu cha kati ambapo mwalimu alikamatwa na mhanga kupewa PF 3 kwa ajili ya matibabu ambapo alipigwa picha na kuonekana moja ya kidole cha kati cha kushoto kimeathirika kutokana na kupigwa kwa kutumia ubao.
PF3
Mzazi huyo amesema hana nia mbaya na mwalimu Kanyika lakini kitendo cha kumwadhibu mwanae mara kwa mara ndicho kimemtia shaka hata kuamua kutoa taarifa Polisi ili sheria ichukue mkondo wake.
Mwandishi wa habari hii alipofika shuleni ili kujua mustakabali wa suala hili, mwalimu alimtoa nje akidai yeye ana majukumu mengine .
Mwandishi alimtafuta mmoja wa wanaharakati wa kijinsia ambaye alikiri kupokea lalamiko hilo ingawa alijibu kwa mkato kuwa mtoto huyo kaumia kidogo tu na ni usanii mtoto huyo kufungwa POP na kwamba bado PF3 haijajazwa kitu hivyo hawezi kuzungumzia lolote.
Kumekuwa na malamiko mengi katika Dawati hilo kutokana na matukio kutochunguzwa kwa wakati , hali inayotoa mwanya kwa vitendo hivyo kuibuka mara kwa mara na wahalifu kutoroka mkono wa sheria .
Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya ameahidi kulifuatilia suala hilo na ikibainika mtuhumiwea atafikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma zinazomkabili.
Na Ezekiel Kamanga 
Mbeya yetu

No comments: