Advertisements

Sunday, December 15, 2013

Manji azua hofu kwa wachezaji Yanga

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji kutangaza kutogombea tena nafasi hiyo, wachezaji wa timu hiyo wameomba kuonana naye.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo zimedai kuwa baada ya wachezaji wa timu hiyo kupata taarifa hizo wameingiwa na hofu.
Kutokana na hali hiyo, wachezaji hao wametuma maombi yao kwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo wakiomba kukutana na Manji ili kujua ni jambo gani lililomfanya afikie uamuzi huo wa kutangaza kutogombea tena nafasi yake ya uenyekiti.
Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo ambaye aliomba kutotajwa jina lake kwa madai kuwa siyo msemaji wa klabu hiyo, aliliambia gazeti hili kuwa, sababu ambazo Manji alizitoa wakati akitangaza uamuzi huo wachezaji hao wamedai kuwa haziwaingii akilini.
Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga aliyemaliza muda wake, Lawrance Mwalusako alipoulizwa juu ya suala hilo alisema kuwa ofisi yake haijipata ombi hilo la wachezaji hao la kutaka kukutana na Mwenyekiti wa klabu hiyo.
Alisema endapo ombi hilo litamfikia ofisini kwake utaratibu utafanyika na wachezaji hao watakutana na kuweza kuzungumza na kiongozi wao huyo.
Baadhi ya sababu ambazo Manji alizitoa kuwa ndiyo zilizomfanya asigombee tena uongozi wa klabu hiyo ni pamoja na kutaka kuwapisha watu wengine wenye uwezo wa kuiongoza klabu hiyo nao kuchukua jahazi.
Alisema kutokana na hali hiyo ndiyo maana alichukua uamuzi wa kutangaza mapema kutowania nafasi hiyo ili kuwapa nafasi nzuri wanaotaka kufanya hivyo waweze kujipanga mapema.
Mwananchi

No comments: