ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 14, 2014

Tuzingatie mafundisho, sherehe za Maulid


Jana ilikuwa ni Siku ya Maulid, siku maalumu ambayo waumini wa dini ya Kiislamu duniani kote walisherehekea kuzaliwa kwa Kiongozi wao Mtume Muhammad (SAW), aliyezaliwa miaka 1435 iliyopita.
Tunatumia fursa hii kuwatakia waumini wa Kiislamu na wananchi wengine mapumziko mema tukitambua ukubwa wa siku ya jana kiimani.
Tunatambua kuwa kwa waumini wa Kiislamu, siku hiyo ina umuhimu mkubwa kwao, kwani siyo tu aliyozaliwa kiongozi wao, lakini ni mojawapo ya matukio ya kiimani yanayowaunganisha Waislamu maeneo mbalimbali duniani.
Muungano huu wa kiimani baina yao ndiyo unaozaa umoja wa waumini na ndiyo maana jana tarehe 12, mfungo sita (Rabbiul Awwal), sehemu kubwa ya Waislamu walijumuika katika mikusanyiko mbalimbali wakilenga kumswalia na kutaja sifa za Mtume (SAW).
Kutajwa kwa sifa za Mtume (SAW), katika siku hiyo na hata nyinginezo, siyo tu ni tanbihi kwa waumini wa dini ya Kiislamu katika masuala ya kiroho, bali ni mawaidha ambayo wanapaswa kuyatumia vyema katika maisha yao ya kila siku hasa katika kuimarisha amani na utulivu.
Katika vitabu mbalimbali vya Maulid ambavyo kwa kawaida huwa ndiyo rejea kubwa katika mikusanyiko ya Waislamu, Mtume Muhammad (SAW), anatajwa kwa sifa ya mtu aliyejitolea kuleta amani na haki miongoni mwa Waarabu wa zama zake katika miji mbalimbali ya Uarabuni hasa ya Makka na Madina.
Sifa hii si ya kunasibishwa na waumini wa Kiislamu pekee, wapenda amani wote bila kujali itikadi za kidini. Hatuna budi kuivaa sifa hii muhimu hasa wakati huu ambao kuna kila dalili kuwa baadhi ya watu nchini wameanza kuichezea amani iliyodumu kwa miaka mingi kwa misingi ya udini, ukabila au umajimbo. Mtume Muhammad (SAW), alipinga dhuluma, unyonyaji na kila aina ya maovu enzi zake. Tanzania haiwezi kujigamba kwamba imetulia, kwani katika siku za hivi karibuni, tumeshuhudia matukio mengi yanayohatarisha amani ya nchi.
Tumeshuhudia kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu yakiwamo mauaji na watu kujeruhiwa kwa silaha za moto na nyinginezo. Wapo wenzetu walioteswa kwa sababu mbalimbali pasipo wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
Tunaposherehekea Siku ya Maulid, haya ni miongoni mwa mambo muhimu yanayohitaji tafakuri ya hali ya juu. Watanzania hawana budi kuitumia Sikukuu hii ya Maulid kuwa mwanzo mpya wa kuelekea kuachana na uhalifu na maovu mengine mbalimbali.
Haki aliyoitetea Mtume Muhammad (SAW), idhihiri sasa katika nyoyo za kila Mtanzania. Kila mtu kwa nafasi na hadhi yake katika jamii atubu na kisha kuamua kuacha maovu, ili iwe chachu ya kutengeneza Tanzania mpya ya watu wenye maadili mazuri ya kidini. Mafundisho ya dini zetu yawe kipaumbele na tuyatumie kukuza maadili katika jamii. Hii ndiyo fursa pekee iliyobaki ya kuwa na Tanzania yenye maadili, kwani upo ushahidi mwingi kuwa sheria za nchi na vyombo vya dola, pamoja na ukali wake, vimeshindwa kuwadhibiti Watanzania kimaadili.
Tunawakumbusha Watanzania kutumia vyema mapumziko ya leo kwa hadhari kubwa kwa kuepuka kujiingiza katika kufanya maasi na uhalifu, mengi kati ya mambo hayo yakiwa ni uvunjifu wa sheria za nchi.
Kwa waliokabidhiwa jukumu la kuhakikisha uwepo wa usalama wa raia na mali zao, kwa maana ya Jeshi la Polisi, tunaamini watatimiza wajibu wao ipasavyo. Tunawatakia Waislamu na Watanzania wote kwa jumla mapumziko mema ya mkesha wa Maulid.
Mwananchi

5 comments:

Anonymous said...

Nawatakieni nyote heri ya siku hii muhimu duniani. Napenda tu kusahihisha, Muhammad (s.a.w) sio kiongozi wa Waisilamu tu. Hivyo ukitumia neni kiongozi wao, inakuwa sio sahihi. Muhammad(s.a.w) kufuatana na mafundisho na amri ya Mungu ni kiongozi wa watu wote, wanaomfata/kumuamini na wasiomfata/kutomuamini.

Maneno haya pia Bwana Yesu ameyathibitisha.

Ahsante sana

Anicetus said...

maoni yako- Anny- ni sawa kabisa: kiongozi hachagui wala habagui watu. Kwa mfano Martin Luther King alikuwa kiongozi aliyepigania haki za binadamu wote.

Anonymous said...

Kiongozi wa kidini ni kiongozi wa waumini na siyo vinginevyo!

Anonymous said...

Habagui, lakini anayemfuata ndiye anayemuongoza. Mtu anaelekea New York halafu adai anaongoza msafara wa wanaoelekea Texas! Does it make sense to you.

Anonymous said...

mmeweka quran halafu comment zenu za uchwara uchwaraaa mtupu

je malcolm x hajapigania haki za binadamu wote au kwa vile alikuwa muislamu acheni zenu