ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 27, 2014

TUNAZISUBIRI SIKU 100 ZA UWANJA WA SIMBA HUKO BUNJU

Mwenyekiti wa Simba Aden Rage 

Uongozi huo ulioingia madarakani Mei 10, 2010 utakuwa umetimiza kipindi cha miaka minne baada ya kupokea uongozi kutoka kwa Hassan Dalali aliyekuwa mwenyekiti na katibu wake, Mwina Kaduguda.
KAMA hakuna kitakachobadilika, Mei 10, 2014 itakuwa siku ya mwisho kwa uongozi wa Simba uliopo madarakani. Hiyo ni kwa mujibu wa katiba ya klabu hiyo.
Uongozi huo ulioingia madarakani Mei 10, 2010 utakuwa umetimiza kipindi cha miaka minne baada ya kupokea uongozi kutoka kwa Hassan Dalali aliyekuwa mwenyekiti na katibu wake, Mwina Kaduguda.
Tumeanza kwa kutahadharisha kwamba kama hakuna kitakachoharibika, Rage na timu yake watakaa pembeni katika kipindi hicho na kuwapa nafasi viongozi wapya.
Tunatambua kwamba lolote linaweza kutokea iwe ni kwa makusudi au bahati mbaya na kuwa sababu ya uchaguzi huo kusogezwa mbele na hivyo uongozi kuendelea kuwapo madarakani. Hata hivyo ni matumaini yetu kwamba katiba itazingatiwa pia Rage na timu yake wataondoka madarakani na kuipisha safu mpya.
Kwa maana hiyo kuanzia leo, Alhamisi Februari 27 hadi Mei 10, Rage na timu yake wanakuwa wamebakiwa na siku 72 za kuiongoza Simba. Ndani ya Simba kwa sasa hali si shwari, ukiachana na matokeo mabaya ya timu kwenye Ligi Kuu, uongozi na wanachama wana matatizo yao.
Mathalani mkutano wa katiba uliopangwa kufanyika Machi 16 mwaka huu nao umeshaanza kuibua mzozo baina ya wanachama kuhusu ajenda za kuzungumzwa. Wakati mwenyekiti akitaka mkutano uwe na ajenda moja ya kuongeza na kupitisha vipengele katika katiba hiyo. Hata hivyo baadhi ya wanachama hawakubali mkutano huo kufanywa kwa ajenda moja tu.
Wapo baadhi ya wanachama ambao wanaamini mkutano huo unafaa kuwa fursa ya kujadili zaidi ya jambo moja hasa kutokana na jinsi mambo yanavyokwenda klabuni hapo. Tukiachana na mambo yote hayo, Simba kwa sasa kuna suala zima la ujenzi wa uwanja, klabu hiyo imekuwa ikifanyia mazoezi katika viwanja vya ovyo vilivyojaa vumbi na ambavyo haviendani na hadhi ya klabu kama Simba.
Katika kukabiliana na tatizo hilo, uongozi wa Simba chini ya Katibu Mkuu, Ezekiel Kamwaga umeahidi kuhakikisha Simba inakuwa na uwanja wake katika kipindi cha siku 100.
Tukiwa miongoni mwa wadau waliolipigia kelele suala la uwanja kwa muda mrefu, awali ya yote tunapenda kuelezea furaha yetu kuhusu mpango huu na hivyo tunazisubiri kwa hamu siku 100 ili tuone kitakachofanywa.
Kwa maana nyingine, kama katiba ya Simba itafuatwa, uwanja huu utakuwa tayari baada ya Rage na wenzake kuondoka madarakani na kazi kumaliziwa na uongozi mpya.
Hili si jambo baya ila litafanikishwa kwa muda uliopangwa iwapo tu uongozi wa sasa utaanza kufanya kazi kwa kuhakikisha baada ya siku 100 kila kitu kinakamilika.
Tunafahamu ukweli kwamba kuahidi na kutekeleza jambo ni mambo mawili tofauti, siku 100 hizi tumezisikia kwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi, tulizisikia kwa mwenyekiti wa Simba anayemaliza muda wake.Kwa maana hiyo, kwetu ahadi hii ya siku si jambo kubwa badala yake tunasubiri kuona nini kitafanyika hizo siku 100 zitakapotimia.
Hivi sasa kinachofanywa ni kuandaa tu sehemu ya kuchezea, ni wazi kwamba hilo ni jambo linalowezekana kama uongozi utakuwa na dhamira ya kweli vinginevyo siku 100 hizi zitakuwa kama nyinginezo zilizozoeleka kutoka kwa viongozi wa michezo na hata siasa.
Credit:Mwanaspoti

No comments: