Advertisements

Friday, April 25, 2014

MR NICE; MUNGU NDIYE ANAKUPANGIA MABAYA?



Mwanamuziki Nice Lucas Mkenda 'Mr Nice'.

MMOJA wa wasanii waliopata kutamba sana katika muziki wa kizazi kipya ni Nice Lucas Mkenda , maarufu sana mitaani kama Mr Nice. Huyu, kwa wasiomfahamu ni miongoni mwa nyota wa mwanzo mwanzo kabisa wa Bongo Fleva kupata shoo nyingi, ndani na nje ya nchi miaka ile ya 2000.
Jamaa siyo tu anajua kuimba, lakini zaidi alijua namna ya kulimiliki jukwaa, anaweza sana kucheza hasa ile staili ya kukata viuno.Kutokana na uwezo wake huo, ndipo alipoamua kujiita Mfalme wa Takeu, mtindo wake binafsi na staili ya muziki wake alioubuni na kuupatia sana.

Kama kuna mtu unaweza kumlinganisha na Nice jukwaani, labda anaweza kuwa H. Baba, mkongwe mwingine ambaye pia alikuwa anapiga dizaini kama hiyo. Kazi kubwa na nzuri aliyoifanya ndiyo ilimfanya akimbiliwe sana na mapromota, akialikwa kila mahali Afrika Mashariki na Kati. 

Hivyo haikushangaza, wakati flani miaka ile alipowahi kusema kwamba alikuwa anaingiza kiasi cha shilingi milioni 40 kwa wiki!Alikuwa anaingiza pesa na nafikiri pia alijua kuzitumia. Kudhihirisha hilo, ni msafara mkubwa aliokuwa akiambatana nao katika harakati zake za kula maisha. Ungeweza kumkuta Club Ambiance kwa mfano akiwa amezungukwa na idadi kubwa ya wapambe.

Hali kama hiyo ungemkuta nayo pia Kwa Macheni, ile baa maarufu sana pale Magomeni jijini Dar es Salaam, Club Billicanas, Maisha Club na sehemu nyingine zote za starehe.

Ninaamini kabisa miaka kama saba au zaidi kati ya mwaka 2002 hadi 2010, pesa haikuwa tatizo kwa Mr Nice, mkali wa vibao kama Kidali Po, Fagilia, Kikulacho na Rafiki.

Wapambe wa Mr Nice wakiwa katika starehe hawakuwahi kupungukiwa vitu mezani, iwe vinywaji au chakula, achilia mbali wale wasio na aibu, walioambatana na mademu zao, kwani bili zao zote zililipwa bila matatizo.

Leo hii tunapozungumza, sijaonana naye muda mrefu kidogo, lakini nina uhakika huyu siyo yule ambaye wakati flani akielekea Rwanda, aliwahi kupokewa na umati mkubwa wa mashabiki alipotua uwanja wa ndege, wakiongozwa na waziri mmoja wa serikali ya Rais Paul Kagame!

Hivi karibuni nilipata kuona mahojiano kati yake na chombo kimoja cha habari. Alizungumza mambo mengi yanayohusiana na muziki, maisha na harakati nyingine. Kilichonisukuma kusema naye hapa, ni kauli yake kwamba mambo yanayomtokea ni mipango ya Mungu.

Hapa alimaanisha kuporomoka kwake kimuziki na bila shaka, kuondoka kwa fedha ‘nyingi’ alizowahi kuzimiliki.Kwanza nimpe pole sana Mr Nice, mmoja kati ya marafiki zangu wengi ndani ya ‘game’ kwa mikasa mfululizo iliyomtokea, kwani katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja alipatwa na majanga mawili makubwa.

Kwanza, akiwa viwanja vyake vya nyumbani, Kona Bar, Sinza Africa Sana alipigwa vibaya na washkaji baada ya kumtuhumu kuwa alitaka kutumia ustaa wake kuwapoka demu wao.

Siku chache baadaye akapata ajali akiwa ndani ya Bajaj na abiria wenzake wawili aliokuwa nao kufariki dunia, lakini Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema akamponya rafiki yetu Mr Nice.
Ni kweli, Mungu ndiye muweza wa kila jambo.

Anaweza kukupandisha na kukushusha akitaka. Lakini wakati mwingine lazima tuwe wakweli ndani ya nafsi zetu.Hivi amekuwezesha kupata fedha, wewe ukakosa mipango nazo, zikapotea, unasema ni mipango yake?

Mimi nadhani wa kulaumiwa hapa ni Mr Nice mwenyewe. Hili ni tatizo la wengi. Huwa tunadhani kwamba vipaji tulivyopewa tunaweza kuwa navyo milele, wakati ukweli ni kwamba hii huwa ni mitaji tu ya kuweza kutusaidia kutambua fursa nyingine za maisha. Unapopata bahati ya kuingiza fedha nyingi, ni vizuri kuwekeza ili kuweza kujimudu siku zijazo.

Leo hii P Diddy anawaongoza wasanii wa muziki wa Hip Hop wanaoingiza fedha nyingi nchini Marekani, si kwa sanaa, bali kwa uwekezaji alioufanya baada ya kupata pesa kupitia fani hiyo.

No comments: