Advertisements

Thursday, April 3, 2014

VITENDO VYA UJANGILI VYAPUNGUA KWA ZAIDI YA ASILIMIA 50


Mmoja wa tembo waliouawa na majangili.
Vitendo vya ujangili  vimepungua kwa asilimia 58 huku idadi ya meno ya tembo yanayokamatwa, ikiwa imeongezeka, kutokana na kukamatwa meno yaliyowindwa siku za nyuma.
Hayo yalisemwa jijini hapa  jana na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori  kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Paul Sarakikya.
Alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari,  juu ya hali ya ujangili katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.
Alisema katika kipindi hicho, siku za doria za kukabili ujangili zilikuwa 30,372 zilifanyika ndani na nje ya hifadhi za taifa na mapori ya akiba nchini. 
Zilihusisha watumishi walioko kwenye idara ya mapori ya akiba na kanda za kikosi dhidi ya ujangili.
Alisema katika kipindi husika, mizoga ya tembo 39 ilionekana ndani na nje ya hifadhi za taifa na mapori ya akiba. Pia meno ya tembo mazima 171 na vipande 22 vya meno ya tembo ghafi, vipande 302 vya meno ya tembo yaliyochakatwa yenye jumla ya kilo 662.62, yalikamatwa, yakitokana na vitendo vya ujangili. 
Aidha ng'ombe 2,663, msumeno na mbao 745 zilikamatwa. Jumla ya kesi 124 zenye watuhumiwa 544 waliojihusisha na vitendo vya ujangili, zilifunguliwa kwenye mahakama mbalimbali nchini.
Kesi 38 kati ya hizo zenye watuhumiwa 113, zinaendelea mahakamani na kesi 62 zenye jumla ya watuhumiwa 85 ziliishia kwa watuhumiwa kulipa faini ya Sh 25,510,000.

1 comment:

Anonymous said...

si wengechukua na nyama wakaenda kutafuna nyama ya tembo tamu sana mijameni jaribuni mtaona utamu wake