Friday, May 30, 2014

Rais Kikwete atoa ushauri malengo ya milenia

Rais Jakaya Kikwete akifuatilia kwa makini hotuba ya Waziri Mkuu wa Canada, Stephen Harpet ( kulia), kwenye ufunguzi wa mkutano wa Afya ya Mama na Mtoto, jijini Toronto,nchini Canada jana.PICHA:IKULU

Rais Jakaya Kikwete ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kuwa malengo ya milenia yanatekelezwa kwa ukamilifu, hata baada ya kuisha muda uliowekwa wa kuyatimiza, kabla ya kuweka malengo mengine mapya.

Rais Kikwete alitoa ushauri huo juzi mwanzoni mwa mkutano wa kimataifa unaohusu afya ya mama na mtoto jijini Toronto, Canada, wakati akijibu maswali kuhusu matokeo ya malengo ya milenia kuelekea mwisho wa muda wa kuyatekeleza mwakani 2015.

"Tukamilishe pale ambapo hatujamaliza na kuimarisha yale yote tuliyoyafanikisha au kuyafikia” alisema Rais Kikwete na kuyataka mataifa kuhakikisha kuwa, malengo manane ya milenia waliyojiwekea, yanatekelezwa kwa ukamilifu kwani ni mazuri na muhimu kwa jamii.

"Baada ya kuyaimarisha na kuyatimiza haya malengo manane tunaweza kupanga na kutafuta mengine na pia tuhakikishe kuwa haya ya sasa hayasahauliki wala kutelekezwa ili tusije kurudi nyuma katika jitihada zetu” alisisitiza.

Malengo ya Milenia Kama yalivyoainishwa na Umoja wa Mataifa ambayo nchi zinazoendelea zinatakiwa kuwa zimeyafikia ifikapo mwaka kesho wa 2015 ni, kuondoa umaskini uliokithiri na njaa, elimu ya msingi kwa wote, usawa wa kijinsia na fursa sawa kwa wanawake, kupunguza vifo vya watoto wachanga na upatikanaji wa huduma bora za uzazi.

Mengine ni kupambana na ukimwi, malaria na magonjwa mengine, kulinda mazingira na kujenga mshikamano wa kimaendeleo duniani.
CHANZO: NIPASHE

No comments: