ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, June 15, 2014

DALADALA MBEYA ZAPEWA ONYO‏

 Kaimu mkurugenzi wa jiji Dr Samwel Lazaro  akiongea 
 Meneja Sumatra Mkoa wa Mbeya, Petro Chacha  akiongea na waandishi wa habari
 Viongozi wa madereva wa daladala  wakisikiliza kwa Makini
Waandishi wa habari

MAMLAKA ya udhibiti wa usafiri wa majini na Nchi kavu(SUMATRA) Mkoa wa Mbeya umetangaza kuwafutia leseni za usafirishaji wa abiria wamiliki wa Daladala zinazofanya safari zake ndani ya Jiji la Mbeya endapo watagomea kubeba abiria.
 
Agizo hilo lilitolewa jana na Meneja wa SUMATRA Mkoa wa Mbeya,Petro Chacha, katika Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya kufuatia mgomo wa madereva wa daladala uliofanyika hivi karibuni kwa madereva hao kugomea kusafirisha abiria kwa amadai ya kuongezewa njia.
 
Chacha alisema mgomo huo ulikuwa ni batili na ulikiuka taratibu za leseni ya usafirishaji kutokana na madai ya Madereva na wamiliki wa magari hayo kukaa na uongozi wa Halmashauri na kujadiliana pamoja na kupata suluhisho.
 
Alisema kutokana na mazungumzo baina ya uongozi wa Jiji na wadau wa usafirishaji Mamlaka haioni sababu ya kuendelea kuwafumbia macho wamiliki ambao watashindwa kupeleka magari yao barabarani kuendelea na mgomo.
 
Alisema Mamlaka itawafutia leseni za usafirishaji wamiliki wote wa magari watakaoendelea kugoma ama kukusudia kugoma kwa suala la umbali wa safari au wakitaka kupandisha nauli bila kufuata taratibu zilizowekwa na Mamlaka.
 
Aliongeza kuwa kuongezewa kwa njia za daladala kumetokana na Halmashauri ya Jiji la Mbeya kujenga na kuimarisha barabara zake mbali mbali ili kuondoa msangamano mkubwa wa magari katika maeneo ya Kabwe, Mwanjelwa na Soweto kutokana na wafanyabiashara ndogo ndogo (machinga) kufanya biashara pembezoni mwa barabara kuu.
 
Alisema Halmashauri ya Jiji ilipendekeza kuwaondoa machinga barabarani na kuwahamishia katika barabara za pembezoni jambo ambalo lilitekelezwa vizuri na uongozi wa Halmashauri kwa kufanikiwa kuwaondoa Machinga hao barabarani.
 
Meneja huyo alisema kutokana na sababu hizo za kuondoa msongamano wa watu na magari katika maeneo ya Kabwe na Soweto Halmashauri ilishauri kuwa magari madogo ya abiria maarufu daladala yaendayo katika njia za Stendi Kuu, Uyole, Isyesye, Nsalaga na Ituha yapite Kabwe na Soweto kwa njia za mchepuko kupitia Block T na Moon Dust.
 
Alisema mbali na lengo la kuepusha msongamano pia ilikuwa na lengo la kupanua huduma katika njia hizo kwa wananchi walio katika maeneo hayo kwa kuwa sasa kuna miuondombinu ya barabara za lami katika maeneo hayo.
 
Chacha alisema SUMATRA kabla ya kutekeleza mapendekezo ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuhusu mabadiliko ya njia zilizotajwa kwa kufanya uhakiki wa urefu wa umbali baada ya mabadiliko ya njia hizo ili kuona kama njia zitabadili nauli.
 
Alisema pia Sumatra iliwashirikisha madereva wa daladala kwa kufanya nao vikao kabla ya kuanza utekelezaji ambapo hakuna mabadiliko yanayotakiwa kufanyika kutokana na kutokuwepo kwa ongezeko kubwa la umbali na nauli kubaki vile vile.

Na Mbeya yetu

No comments: