
By EDO KUMWEMBE, SAO PAULO
Baadaye nagundua kuwa Joao aliwahi kufungwa jela na anaamini kuwa alikuwa mchezaji mahiri kuliko wachezaji wa sasa, lakini hakupata nafasi. Anaamini kuwa jela kuna wachezaji hatari sana ambao uovu wao umeshindwa kuwapa nafasi.
NIPO katika kaunta ya pub moja iitwayo Kamani, ni katikati ya Jiji la Sao Paulo. Natazama kupitia televisheni pambano baina ya Uholanzi na Hispania linalochezwa katika mji wa Salvador uliopo kilomita nyingi kutoka hapa. Ni safari ya saa 36 kwa basi kama ningeamua kwenda.
Nazungumza na mhudumu wa kiume, Joao da Silva, aliyesimama kando ya kaunta ambaye anaonekana anaongea Kiingereza kizuri. Anaonekana kudharau pambano linaloendelea licha ya ukweli kuwa ni pambano kali na la kusisimua. Robina van Persie na Arjen Robben wako katika ubora wao lakini Joao hana habari nao.
Namuuliza Joao kwanini hana muda na mechi hiyo. Anajibu kuwa hata mechi ya jana yake kati ya Brazil na Croatia hakuitazama. Ninapomuuliza kwa nini hakuitazama wakati taifa lake lina wachezaji mahiri na walitazamia kushinda, Joao ananipa majibu ya kusisimua zaidi ambayo yanasababisha nimnunulie kinywaji.
“Hapa Brazil jela zake zina wachezaji wenye ufundi mwingi kuliko hawa wachezaji unaowaona katika Kombe la Dunia. Hapa hakuna mpira. Kule kuna mafundi wengi kuliko Ronaldo de Lima, Ronaldinho na Neymar,” anasema Joao kwa kujiamini.
Baadaye nagundua kuwa Joao aliwahi kufungwa jela na anaamini kuwa alikuwa mchezaji mahiri kuliko wachezaji wa sasa, lakini hakupata nafasi. Anaamini kuwa jela kuna wachezaji hatari sana ambao uovu wao umeshindwa kuwapa nafasi.
“Kule jela kuna wachezaji wamecheza na Ricardo Kaka, wamecheza na Ronaldo de Lima, wamecheza na Ronaldinho na hata picha zipo. Tatizo walikuwa na haraka ya maisha wakaingia katika uovu. Hakuna chenga ambayo unaiona kwa Neymar ambayo wachezaji wa jela hawapigi.” Anasema Joao kwa kiburi kikubwa.
“Kule jela tunacheza soka la wachezaji watano watano na uwanja ni mdogo. Inabidi uwe na akili kubwa. Lakini niamini mimi kuwa kuna watu wana akili kubwa kuliko hao hapo mnaowaona katika televisheni wakicheza Kombe la Dunia,” anaongeza Joao.
Kufika hapo namwongezea Joao kinywaji kingine. Anajibu kwa Kireno Obligado akimaanisha asante. Anapata kasi ya kuongea zaidi na zaidi tena kwa kujiamini. Nagundua kuwa hata Kiingereza anachoongea kilitokana na yeye kujifunza akiwa jela alikokutana na wafungwa wa mataifa mbalimbali.
“Brazil maisha ni magumu. Wakati mwingine si wachezaji wote wanaofanikiwa. Kuna wanaoshindwa kwa sababu malezi ya wazazi hayawi mazuri. Unakuta mzazi anashindwa kumudu mahitaji muhimu ya mtoto. Kinachofuata ni mtoto kuingia katika ukabaji na kuachana na soka kwa sababu soka ina safari ndefu kuliko ukabaji,” anaongeza Joao
“Ukiwa jela hakuna unachowaza zaidi ya soka. Unaamka asubuhi unacheza soka, mchana unacheza soka na jioni unacheza soka. Unakuwa fiti zaidi na kila siku mbinu zako zinaongezeka kwa sababu mnacheza mchezo wa watu watano watano katika eneo dogo.
“Kuna timu mbalimbali ndani ya jela. Kuna Waafrika, kuna watu kutoka Ulaya na kuna timu za ndani ya Brazil. Wote hawa wamefungwa kwa makosa mbalimbali lakini kitu kikubwa ni dawa za kulevya.”
Joao anaonyesha hasira kwa wanasoka mastaa wa sasa wa Brazil kama akina Marcelo, Dani Alves, Neymar na wengineo ambao anaamini kuwa wanapata pesa nyingi bila ya sababu lakini pia uwezo wao wa kujituma uko chini.
“Wanapata pesa nyingi wanaendesha magari ya kifahari, lakini si unaona jana wamesumbuliwa na Croatia? Uwezo wao wa kujituma uko chini kabisa. Ni bure kabisa hawa.” Anasema Joao ambaye ni dhahiri sasa anaonekana kuwa miongoni mwa watu wanaounga mkono waandamanaji wanaopinga Serikali yao kutumia mabilioni ya pesa kuandaa fainali za Kombe la Dunia.
Kufikia hapo naamini maneno yake kwa sababu katika nyakati tofauti mastaa wengi wakubwa Amerika Kusini wamewahi kukaririwa wakidai kwamba kama wasingecheza soka basi wangeishia jela kwa makosa mbalimbali ya jinai.
Staa wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil, Ronaldo de Lima na nyota wa Argentina, Carlos Tevez, kwa nyakati mbalimbali wamewahi kukaririwa wakidai kwamba mchezo wa soka ndio ambao umewaokoa wasijiingize katika tabia za ukabaji na ubakaji vile vile.
Hata hivyo simuachi Joao bila ya kumuuliza mchezaji ambaye anamuona anacheza kama wachezaji wa jela za Brazil.
“Ni Lionel Messi,” anajibu kwa kujiamini. Hapo nashangaa zaidi. Wabrazili na Waargentina wana uadui mkubwa na inakuaje raia wa Brazil anamsifia Messi moja kwa moja?
“Anapambana uwanjani halafu hana mambo mengi nje ya uwanja. Hauwezi kumkuta Messi katika masuala ya umalaya, ni tofauti na ilivyo kwa wachezaji wa Brazil,” anajibu Joao kwa kujiamini kabisa.
Kufikia hapo, pambano la Uholanzi na Hispania linakuwa limemalizika. Hata hivyo naweka ahadi moja ya kwenda jela na Joao kwa ajili ya kujionea mwenyewe mafundi wa Kibrazili walioishia jela.
CREDIT:MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment