Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe
Kigogo wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Ally Mkufya
(60), anadaiwa kujiua kwa kujipiga risasi shingoni.
Mkufya
ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Wilaya
hiyo, alijipiga risasi jana alfajiri akiwa chumba alichokuwa akiishi
kwenye baa yake ya Tete Pub Extra ambayo pia ina sehemu ya nyumba ya
kulala wageni, iliyopo pembeni ya barabara ya kwenda Tanga mjini.
Kigogo huyo
wa CCM ambaye pia ni mfanyabiashara anayemiliki baa kadhaa, anadaiwa
kukatisha maisha yake kwa kujipiga risasi shingoni wakati huo akiwa
amejifungia chumbani.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe, akizungumzia kifo hicho
alisema uchunguzi unafanyika ili kujua chanzo cha kujiua kwa kujipiga
risasi ingawa baadhi ya watu wanasema kifo hicho kimetokana na sababu za
kifamilia zilizomfanya ahame nyumbani kwake na kuishi baa kwa muda
mrefu.
Viongozi wa
chama wilayani humo akiwamo Mwenyekiti Peter Jambele, Katibu Mwenezi ,
Makame Seif na Katibu wa CCM wa Wilaya ya Muheza, Josephin Mbezi,
walielezea kusikitishwa na kifo hicho walichosema ni kibaya.
Awali
akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mlinzi wa baa hiyo, Idd
Abdallah, alisema alipoingia kazini juzi jioni hakukutana na mwajiri
wake licha ya kwamba alikuwa na kawaida ya kukaa nje hadi usiku baa
inapofungwa.
Alieleza
kuwa aliingiwa na hofu na kuwauliza wahudumu, lakini alijibiwa kuwa bosi
wao amejipumzisha chumbani kwake kwa kuwa anajisikia homa na kwamba
hali iliendelea hivyo hadi muda wa kufunga baa ulipofika na wahudumu
kuondoka.
Mlinzi huyo
alisema kuwa ilipofika asubuhi wahudumu walifungua baa na kufanya usafi,
lakini cha kushangaza Mkufya alikuwa hajaamka jambo ambalo halikuwa
kawaida yake kulala hadi wakati huo.
Hofu hiyo iliwafanya kugonga mlango, lakini haukufunguliwa hivyo kulazimika kuwapigia simu ndugu zake ili waje kwenye baa hiyo.
Abdallah
alisema walipofika chumbani kwake walivunja mlango na kumkuta amekufa
kwa kupigwa risasi shingoni na bunduki aina ya Short ikiwa pembeni yake
huku damu zikiwa zimetapakaa chumba kizima.
Alisema
walipiga simu polisi na askari walifika kuuchukua mwili wa marehemu hadi
hospitali Teule wilayani Muheza ambako umehifadhiwa.
KAULI YA MKEWE
NIPASHE
ilifika nyumbani kwa marehemu jana na kumkuta mkewe, Anna Mkufya, akiwa
katika majonzi makubwa. Hata hivyo, hakuwa tayari kuzungumza lolote juu
ya tukio hilo.
Marehemu ameacha watoto watano na anatarajiwa kuzikwa kesho katika kijiji cha Semgao wilayani Muheza.
NA STEVE WILLIAM
CHANZO NIPASHE
No comments:
Post a Comment