ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 17, 2014

Majambazi wajeruhi,wapora fedha Dar


Watu wawili wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa katika pikipiki aina ya boxer wamevamia gari la Kampuni ya Azam na kisha kumjeruhi kwa risasi dereva, wa kampuni hiyo na kumpora mfuko uliokuwa na pesa zaidi ya Sh. milioni moja.

Tukio hilo lilitokea jana saa 5:00 asubuhi, katika eneo la Banana, njia panda ya kuelekea Kitunda, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, dereva huyo, Cletus Kisekwa, akiwa na mwenzake wakitoka kukusanya fedha za mauzo kwenye maduka, ambayo kampuni hiyo husambaza bidhaa zake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alithibitisha kutokea kwa tukio.

Kwa mujibu wa Kamanda Minangi, gari hilo lilikuwa linatoka Kitunda kukusanya fedha na lilipofika eneo la Banana lilivamiwa na majambazi waliokuwa na bastola na kupora Sh. milioni 1.1 na kumjeruhi dereva.

Alisema kufuatia tukio hilo watu wawili, ambao hata hivyo, hakuwataja majina, wamekamatwa katika eneo la Uwanja wa Ndege wakiwa na bastola na kwamba, msaka bado unaendelea.

Baada ya majambazi hayo kukimbia kusikojulikana kwa kutumia pikipiki aina ya boxer, kondakta wa gari la kampuni hiyo lenye namba za usajiri T 293 CAY, aliyefahamika kwa jina moja la Abdallah, alichukua jukumu la kuendesha gari hilo hadi Hospitali ya Arafa M6, na kumpeleka dereva aliyejeruhiwa kwa risasi, huku akivuja damu nyingi.

Baada ya kufika katika hospitali hiyo, lakini kutoka na kuvuja damu nyingi, madaktari wa hospitali hiyo walishauri apelekwe katika Hospitali ya Amana.

Kondakta wa gari lililovamiwa, Abdallah akitoa maelezo kwa polisi wa kituo cha Stakishari wakiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ilala (OCD) katika hospitali hiyo, alisema walivamiwa na majambazi wakati wakitoka kuchukua fedha.

“Tulitoka eneo la Kitunda kwa ajili ya kukusanya fedha za mauzo katika maduka, ambayo huwa tunawapelekea bidhaa, lakini tulipofika eneo la Banana walijitokeza watu wawili waliokuwa na silaha wakiwa katika pikipiki na kumpiga risasi dereva baada ya kufungua mlango wa gari,” alisema.

Abdallah, ambaye alitoa maelezo kwa polisi, huku akilia, alisema majambazi hao baada ya kumjeruhi dereva walipora Sh. 765,000.

Alisema fedha hizo walipora katika duka moja na kwenye duka jingine walichukua Sh. 382,000.
CHANZO: NIPASHE

No comments: