ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 20, 2014

MANJI NA YANGA YENYE THAMANI YA BIL 12

Hata hivyo, uchaguzi wa klabu hiyo ambao ulikuwa umepangwa kufanyika mwezi huu, umesogezwa mbele kwa mwaka mmoja kutokana na uamuzi wa Mkutano Mkuu uliofanya maboresho ya Katiba, Uamuzi huo ulilenga kumwongezea Manji na uongozi wake muda wa mwaka mmoja hadi Juni mwakani.

MWENYEKITI wa Yanga, Yusuf Manji, ametimiza miaka miwili sasa tangu alipoingia madarakani mwaka 2012 katika uchaguzi mdogo wa klabu hiyo na Juni hii ndiyo ilikuwa mwisho wa awamu ya uongozi wake.
Hata hivyo, uchaguzi wa klabu hiyo ambao ulikuwa umepangwa kufanyika mwezi huu, umesogezwa mbele kwa mwaka mmoja kutokana na uamuzi wa Mkutano Mkuu uliofanya maboresho ya Katiba, Uamuzi huo ulilenga kumwongezea Manji na uongozi wake muda wa mwaka mmoja hadi Juni mwakani.


Kuhusiana na hilo, Manji anasema: “Lilikuwa ni jambo la kushitukiza kwangu, sikutegemea kama wangeamua kuniongezea muda kwani nilishaweka azma yangu wazi kuwa nisingependa kugombea tena kwa kipindi kingine, ile siku nilijiandaa kukabidhi ofisi na kila kitu nilishakiandaa tayari.


“Nilishtushwa zaidi walipotaka kuniongezea miaka minane, ni mingi sana, kikubwa mimi napenda kuwaondoa shaka wana Yanga kuwa mimi naipenda klabu hiyo, niwe Mwenyekiti au mwanachama wa kawaida, nikipenda kitu huwa sipendi nusu, hivyo wasipate wasiwasi.”Ujio wa Maximo Manji anasema Yanga ni timu kubwa na kocha Marcio Maximo ni mtu maarufu, wamepanga kumtumia kuongeza wanachama wa klabu hiyo katika kampeni ya kuwataka kuchukua kadi za uanachama zinazotolewa na Benki ya Posta Tanzania katika mpango maalumu wa kuiongozea klabu hiyo mapato.


“Maximo atakuja kwani lengo letu ni kuhamasisha wapenzi wa klabu yetu wajiunge na uanachama, tutamlipa ghali lakini tutahakikisha tunamtumia kuongeza pato la klabu, si yeye pekee bali tutaleta kila mtu tunayeona atasaidia katika hili,” anasema.


“Katika kampeni hii tutatumia pia wachezaji wetu, tutawatumia kuhamasisha vijana wenzao kuchukua kadi za uanachama ambazo pia mwanachama atafunguliwa akaunti kwenye benki ambayo itawasaidia kwenye kuweka akiba.”


Vyanzo vya mapato Yanga


Manji anasema kwa sasa klabu ya Yanga inajiendesha kwa fedha za wadhamini, viingilio vya milangoni pamoja na fedha za wafadhili na kubainisha kuwa pato halisi la klabu hiyo linakidhi nusu tu ya mahitaji ya klabu.


“Katika mapato kwanza, niliamua kufanya mambo kwa uwazi, matumizi ya timu yanakaguliwa na kuchapishwa kwenye magazeti, nimeanzisha na watakaokuja waendelee, ni changamoto,” anasema.


“Unajua ni kazi ngumu kusimamia mapato na kuyaweka kwa uwazi, lakini uzuri wake ni kwamba jambo hili linapunguza wizi wa fedha.


“Yanga inatumia Sh2.4 bilioni kwa matumizi yake ya mwaka, mapato halisi yanayopatikana ni kiasi cha Sh1.2 bilioni tu ambacho ni nusu tu.


“Yanga ni klabu tajiri sana kutokana na kuwa na wapenzi wengi, tumeamua kuzindua huduma ya kadi kwa wanachama ambayo ina makundi mawili tofauti, la kwanza ni la wanachama wanaopenda kuichangia Yanga fedha nyingi na ya pili ni ile ya kawaida ya ada ya Sh12,000 kwa mwaka.


“Kwa hiyo ya pili kila mwanachama atakatwa Sh250 kwa wiki, ni kiasi kidogo sana ila kinamaana kubwa kwa Yanga, lengo langu ni kufanya kampeni ili kuhakikisha tunakua na wanachama wasiopungua milioni moja ambao wanaichangia klabu.”


Manji anabainisha kuwa baada ya mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, atafanya kampeni nchi nzima ili kuwahamasisha wapenzi wa klabu hiyo kujiunga na huduma hiyo mpya.


“Nikifanikiwa kupata wanachama milioni moja hii inamaanisha kwa ada zao pekee kwa mwezi Yanga itaingiza Sh1 bilioni kiasi ambacho ni kikubwa. Kwa mwaka tutakua na Sh12 bilioni ambazo tukiondoa za uendeshaji wa timu tutasaliwa na Sh9 bilioni zitakazotusaidia kujenga uwanja,” anasema Manji


Uwanja wa Kaunda


“Tumeamua kuweka msimamo wa kutengeneza uwanja katika eneo letu la Jangwani kutokana na ukweli kuwa ni karibu zaidi na makazi ya watu, ni eneo ambalo watu watakwenda kutazama mpira kwa kutembea kwa miguu.


“Tunataka kujenga uwanja wenye uwezo wa kubeba watu 40,000, idadi ambayo ni kubwa, tukienda kujenga huu uwanja nje ya mji itakua ni tatizo kupata idadi hiyo ya watu kuja kutazama mechi zetu,” anasema Manji


Jina la uwanja kuuzwa


“Mbali na jina hata viti vya uwanjani ningependa viwe chanzo kikubwa cha mapato, hii itakuwa kwa wanaopenda kuweka kumbukumbu zao Yanga, tutawauzia viti kwa kuviandika majina yao, lakini akiingia uwanjani ni lazima alipe kiingilio, jina ni kwa ajili ya kumbukumbu tu,” anasema Manji.


Udhamini Azam TV


“Mimi na (Said Salim) Bakhresa ni marafiki, ni mfanyabiashara mwenzangu na sina matatizo naye, wito wangu kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni kuwa thamani ya Yanga ni kubwa, ni klabu yenye wapenzi wengi nchini hivyo inapaswa kupewa fungu kubwa, mbali ya Simba, hauwezi kuifananisha na timu nyingine yoyote.


“Tangu mechi zianze kuonyeshwa ‘Live’ katika Azam TV, ni dhahiri kuwa mapato yameshuka, watu wengi wanaona hakuna haja ya kwenda uwanjani wakati wanaweza kushughudia mechi kwenye luninga, hili si kwa Yanga pekee bali ni kwa timu nyingi na rekodi zinaonyesha,” anasema Manji na kuongeza


“Tungefanya kama Ulaya, mechi za mji huo hazitakiwi kuonyeshwa kwenye luninga za mji, wapate kuona watu wa mikoa mingine ili wale wa mkoa husika wajitokeze kwenda kutazama mechi uwanjani, hili litasaidia.”


“Changamoto kubwa ninayokumbana nayo ni kupata watendaji wazuri, wapo watu wengi wanaipenda Yanga ila tatizo wanaogopa kuingia kwenye uongozi, wanaogopa majina yao kuchafuliwa.


“Hili linachangiwa na mpira wetu kuharibiwa katika siku za nyuma, kulikua na viongozi waliokua wakijitazama wao, waliangalia klabu zinawafanyia nini na sio wao wanazifanyia nini klabu hizo, hilo lilichangia migogoro na kuiporomosha heshima ya uongozi wa klabu hizi,” anasema Manji na kuongeza


“Tatizo jingine ni matarajio makubwa wanayokuwa nayo watu juu yako, wengi wanakutazama na usipokua makini unaweza kulewa madaraka na kujisahau, unakua ukijiuliza jina langu litabaki vipi baada ya uongozi wangu.


“Kila ukipita sehemu watu wanakufahamu kwa jina la Mwenyekiti, nashindwa kutoka kwenda kupata chakula na familia yangu, mke wangu anaogopa kutembea na mimi maana kidogo utashangaa tumepigwa picha, mama yangu ananikana kabisa kwa kuogopa umaarufu huo, hii ni changamoto kubwa pia.”

No comments: