ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 5, 2014

Bomu laua wanne nje ya bunge Somalia

Wapiganaji wa Al shabaab

Bomu lililotegwa kwenye gari limelipuka na kuua watu wanne karibu na Bunge la Somalia na wengine kujeruhiwa, maafisa wa Polisi wamesema.

Habari zanasema bomu hilo lilipiga nje ya lango kuu la kuingia katika majengo ya Bunge la Somalia baada ya askari kumrushia risasi mtu anayedaiwa kulipua bomu hilo.

Mshambuliaji aliyejitolea mhanga pia alikufa, alipolipua gari lake, baada ya kukataliwa kuingia kwenye eneo la bunge.

Kabla ya hapo, mshambuliaji huyo alijaribu kuingia katika wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, lakini alizuiliwa.

Taarifa zilizonukuliwa kutoka kundi la kigaidi la Al Shabaab zinasema wapiganaji hao walifanya shambulio la kujitoa sadaka.

Wapiganaji hao Waislamu wamelaumiwa kwa shambulio hilo. Al-Shabaab ilisema itazidisha mashambulio wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Mlipuko mwingine uliofanywa na waasi hao katika majengo ya bunge mwezi Mei uliua watu 10.

Kundi la Al shabaab lilipoteza udhibithi katika mji mkuu wa Mogadishu tangu mwaka 2011 na tangu wakati huo limekuwa likiendesha mashambulizi ya mabomu na kufanya mauaji.

Mapema wiki hii Mbunge maarufu Ahmed Mohamud Hayd, aliuawa kwa kupigwa risasi katika mji huo, katika shambulio linalodaiwa kufanywa na Al Shabaab.

BBC

No comments: