Advertisements

Wednesday, July 30, 2014

Taifa Stars kuifuata Mambas leo


Kikosi cha timu ya soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), kinaondoka nchini leo kuelekea Afrika Kusini na baadaye Msumbiji kwa ajili ya kwenda kurudiana na 'Mambas' ifikapo Agosti 3, mwaka huu mjini Maputo.

Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu kutoka Tukuyu jijini Mbeya, Meneja wa Taifa Stars, Boniface Clemence, alisema timu hiyo itarejea Dar es Salaam mapema leo asubuhi na mchana saa saba itaondoka kuelekea jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Clemence alisema maandalizi ya mechi hiyo ya marudiano yamekamilika na timu ikiwa Johannesburg itafanya mazoezi mepesi ili kutowachosha wachezaji.

Meneja huyo alisema wachezaji watatu wanaocheza nje ya nchi wameitwa na Kocha Mkuu, Mart Nooij, watajiunga na kikosi hicho nchini Afrika Kusini.

Alisema kwamba wachezaji wote ni wazima ila jana asubuhi walishindwa kufanya mazoezi kutokana na mvua iliyonyesha na ukungu kuwa mwingi.

"Tuko vizuri na mjini tunarudi kesho (leo) asubuhi na saa saba mchana tunaondoka kwenda Afrika Kusini," alisema meneja huyo.

Aliongeza kuwa, jana jioni ndiyo nyota watakaosafiri kwenda kurudiana na Mambas walitarajiwa kujulikana.

"Bado mwalimu hajatangaza wachezaji watakaosafiri...nafikiri ataweka wazi jioni katika chakula cha pamoja," Clemence aliongeza.

Alisema pia wanashukuru Mungu hakuna mchezaji aliye majeruhi hivyo Nooij atakuwa huru kuteua wachezaji wote waliomridhisha na walioonyesha kiwango cha juu mazoezini.

Wachezaji watatu wanaocheza nje ya nchi ambao watajiunga na Stars ikiwa Sauzi ni Mwinyi Kaimoto anayecheza soka la kulipwa katika Klabu ya Al Markhiya ya Qatari, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaokipiga TP Mazembe ya DR Congo.

Taifa Stars inahitaji ushindi wa aina yoyote ndani ya dakika 90 za kawaida ili iweze kusonga mbele na kutinga hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ( AFCON) hapo mwakani.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Stars na Mambas zilitoka sare ya mabao 2-2 huku kiungo wa Azam, Khamis Mcha, akiifungia Tanzania mabao yote mawili.
CHANZO: NIPASHE

No comments: