ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 31, 2014

‘TUNATAKA MUUNGANO WENYE HESHIMA'

Baada ya wabunge wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) upande wa Zanzibar kugomea kushiriki Bunge la Katiba kwa madai ya kukimbia kejeli, matusi na ubaguzi katika Bunge hilo, taasisi moja ya utafiti na sera za umma (ZRPP) imeamua kuwaunganisha Wazanzibari ili kufikia
lengo la kupata Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Madhumuni ya kamati hiyo yametajwa kuwa ni kuwaweka pamoja wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka Zanzibar, hasa wanaotokana na CCM na CUF pamoja na wajumbe wateule 201 kutoka taasisi na mashirika ya kijamii na dini.
Imeelezwa kuwa nia kuu ni kupata sauti ya pamoja ya wabunge hao kwa ajili ya kutetea na kusimamia masilahi ya Wazanzibari katika uundwaji wa Katiba Mpya.
Katibu wa Kamati hiyo ya wajumbe sita, Muhamed Yussuf Mshamba amesema atahakikisha anafanya kila linalowezekana ili kabla ya kuanza kwa Bunge la Katiba, mwafaka upatikane.
Kauli hiyo ya Yussuf imekuja mara baada ya wajumbe hao sita kukutana na kumteua aliyekuwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Kiongozi Zanzibar, Ali Abdallah Suleiman kuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Wajumbe wengine Abas Juma Muhunzi, Mselem Khamis Mselem, Enzi Aboud Talib, Ali Hassan Khamis, Naila Majid Jidawi na aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Awadh Ali Said.
Yusuf anasema kamati hiyo imeundwa kupitia mdahalo wa wazi uliofanyika kwenye Ukumbi wa Suza kwa minajili ya kusaka suluhu katika mvutano wa wajumbe wa Bunge la Katiba.
Yussuf amethibitisha kukutana kwa kamati hiyo na kufungua milango ya ufanyaji kazi kwa kuwateua wajumbe wawili kuandaa rasimu ya kwanza ya waraka wa mapatano ya umoja ambao utaelezea mambo ya msingi ili kuungana na kuyatetea kwa nguvu moja kwa manufaa ya sasa na ya vizazi vijavyo.
Anasema kuwa rasimu ya waraka huo itaandaliwa na wajumbe wawili akiwamo yeye mwenyewe kama Katibu na mjumbe Abas Juma Muhunzi kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa na washiriki wa madahalo wa wazi. Lengo kuu ni kuona unapatikana Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wenye hadhi sawa, haki na heshima.
Mohamed Yussuf amekuwa ni mmoja wa makamishna ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake Jaji Joseph Warioba ambaye anaamini kuwa mfumo wa sasa si wenye kutoa haki, usawa na mlingano unaostahili katika umbile la muungano uliopo.
Anataja kuwa kazi ya rasimu hiyo ya waraka wa mapatano ikikamilika, wajumbe sita watakutana kuujadili na kuupitisha, kuboresha maeneo ambayo yataonekana ipo haja na ulazima wa kuyatia nyama au kuyapunguza, kabla ya kumkabidhi Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, akiamini kazi hiyo itawahi ndani ya kipindi cha wiki moja kabla ya Bunge la Katiba kuanza tena vikao vyake Agosti 5 mwaka huu.
Viongozi wengine wa juu ambao watapatiwa nakala ya waraka huo ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili, Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho.

MWANANCHI

No comments: