ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 23, 2014

Bilioni 54 zaokolewa wafanyakazi hewa

Naibu waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba

Serikali imeokoa zaidi ya Sh. bilioni 54 za malipo hewa ya mishahara na malimbikizo ya madai ya walimu.

Aidha, baadhi ya vigogo wa serikali waliohusika na malipo hayo, majina yao yamefikishwa jeshi la polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) kwa ajili ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema kubainika kwa fedha hizo za malipo hewa kumetokana na utaratibu wa serikali kulipa mishahara ya watumishi kwenye akaunti zao za benki pamoja na kufanya zoezi la uhakiki wa madeni.

Alisema kuanzia mwezi Julai mwaka huu serikali imegundua kulikuwa na majina 14,710 ya wafanyakazi hewa, ambapo walitakiwa kulipwa zaidi ya Sh. Bilioni 40 za mishahara.

Alisema kubainika kwa majina hayo kulitokana na utaratibu mpya wa kulipia mishahara ya watumishi moja kwa moja benki na kuachana na utaratibu wa kulipa hundi kwa taasisi za serikali.

Alisema serikali inatumia jumla ya Sh. Bilioni 400 kwa mwezi kwa ajili ya kuwalipa mishahara wafanyakazi wanaofikia idadi ya 400,000.
Nchemba alisema waliamua kusitisha malipo kwenda kwa taasisi hizo kutokana na hisia zilizokuwepo kwamba kulikuwa na ulipaji wa mishahara kwa wafanyakazi hewa.

“Kwa kutumia ulipaji wa mishahara madirishani kupitia taasisi husika, wafanyakazi waliokufa, waliohama au kuacha kazi walikuwa wakilipwa na baadhi ya watu waliopewa dhamana walitumia nafasi hiyo kujinufaisha,” alisema Nchemba.

Aliongeza kusema “kwa kutumia mfumo huu idadi kubwa ya majina yameyeyuka katika payrol (orodha ya majina ya malipo), suala hili hatuwezi kulivumilia hata kidogo, tutaendelea kulifuatilia hadi tuone tunalikomesha," alisema.

Alisema majina hewa yamesababisha kuzuia idadi kubwa ya vijana kukosa kazi, hivyo utaratibu utafanyika kwa nafasi hizo kuzibwa na vijana hao.

Aidha, Nchemba alisema malipo hewa pia yalionekana katika malimbikizo ya madai ya walimu, ambapo kati ya Sh. bilioni 19.5 zilizoidhinishwa malipo halali ni sh. Bilioni 5.4 pekee.

Akitoa mfano, Nchemba alisema kuna madai ya mwalimu mmoja ambaye awali ilionekana alitakiwa kulipwa Sh. Milioni 500, lakini baada ya kufanyiwa uhakiki ilibainika alikuwa akidai milioni 50.

VIGOGO KUKAMATWA

Katika kashfa hiyo tayari watu kadhaa (hakuwataja majina), majina yao yamefikishwa katika vyombo vya dola ikiwamo jeshi la polisi na Takukuru kwa ajili ya kuchukua hatua.

Alisisitiza kwamba hakuna mtu aliyehusika kwa namna moja au nyingine katika kuidhinisha malipo hayo atakwepa kutiwa nguvuni.“Watu walioruhusu kulipwa kwa majina haya lazima watakamatwa, hili jambo sio la masihara tumeamua kupambana, huu ni unyonyaji wa kupitiliza,” alisema.

Alitaja baadhi ya watu waliohusika na uandaaji wa majina hayo kuwa ni viongozi wa halmashauri, mashirika, taasisi za serikali pamoja na wizara yake.

Katika kuhakikisha majina mengine yanapatikana, ameagiza Wakurugenzi wa Halmashauri, waweka hazina na viongozi wanaohusika na madurufu, kuhakikisha wanapeleka majina ya watumishi wao halali na namba zao za akaunti kwa ajili ya kuhakikiwa.

Alionya watumishi wanaofanyakazi katika uwekaji wa rekodi za wafanyakazi wa serikali kuwa na maadili kwa kutojiingiza katika vitendo hivyo, alionya atakayebainika kwenda kinyume atachukuliwa hatua.
CHANZO: NIPASHE

No comments: