Mwenyekiti wa Yanga,Yusuf Manji.
Manji aliyeonekana na uso wa furaha wakati wote wa mkutano wake na waandishi wa habari akiambatana na Makamu wake Clement Sanga, alisisitiza kwamba Yanga haiwezi kuwa chini ya mchezaji mmoja na kwamba hawajawahi kumuacha Okwi.
SIMBA kila kona nchini wanashangilia baada ya kumsainisha straika machachari mwenye mkataba na Yanga, Emmanuel Okwi. Lakini Mwenyekiti wa Yanga,Yusuf Manji, ameibuka na kutoa msimamo mkali kwa kusisitiza kwamba mchezaji huyo hatacheza Msimbazi.
Manji aliyeonekana na uso wa furaha wakati wote wa mkutano wake na waandishi wa habari akiambatana na Makamu wake Clement Sanga, alisisitiza kwamba Yanga haiwezi kuwa chini ya mchezaji mmoja na kwamba hawajawahi kumuacha Okwi.
Alisema kwamba wamemfungulia mashtaka ya kinidhamu TFF na hata katika orodha yao ya wachezaji wa kigeni waliopelekwa TFF jina la Okwi limo wakisubiri hatma ya kesi waliyoifungua.
“Siku zote tumekuwa tukiwaheshimu hawa jamaa zetu, mtamkumbuka mara kadhaa nimekuwa nikiwapongeza hata wanapoifunga timu yangu, tumekuwa tukiwasajili wachezaji wengi wa Simba kama Kaseja (Juma), Yondani (Kelvin) lakini hatukuwa tunawasajili wakati wana mikataba tunasubiri mpaka mikataba yao inapomalizika,”alisema Manji.
“Yanga hatuna desturi ya kulalamika waliondoka Kavumbagu (Didier) na Domayo (Frank) kwenda Azam hatukulalamika kwa kuwa utaratibu ulifuatwa na hata hili hatulalamiki kwa kuwa tunajua tunachokifanya, Yanga hatujamuacha Okwi, ni mchezaji wetu.
“Inashangaza sana inawezekanaje mtu akawa na ugomvi na mkewe wakati huohuo kuna mtu mwingine anajitokeza kusikojulikana na kutangaza kufunga ndoa halali na mkeo, unaweza kujiuliza hawa watu wamekutana na kupatana wakati gani, linatutia shaka hili.”
Manji alisema kwa kuwa tayari wameshafungua kesi ya kwanza ambayo kabla ya kujibiwa mchezaji husika ameongeza kosa lingine, sasa Yanga imewasilisha TFF mashtaka mengine ambayo sasa itawajumuisha Okwi, Simba na wakala wa mchezaji.
Katika kesi hiyo sasa pande hizo tatu zitatakiwa kuilipa Yanga kiasi cha Dola 500,000 (Sh825mil).
“Nina uwezo wa kuwanunua wachezaji wote wa Simba pamoja na kocha wao Phiri (Patrick) na kuwazuia wasicheze ligi wakae pale Gymkhana wachezee mpira na kulala, lakini nikifanya hivyo watu watalalamika Manji anaharibu mpira.
“Najua kwamba mishahara ya wachezaji wangu wa Yanga ya miezi miwili pale Simba inawalipa wachezaji wao wote mwaka mzima, tunataka kuona TFF inawafungia Okwi na Simba tunatoa siku saba kujua hatma ya hilo ikishindikana hapo tutaenda Fifa na CAS (mahakama ya michezo),”alisisitiza Manji.
TFF yamtambua Okwi Yanga
TFF kupitia kwa Katibu wake Mkuu, Celestine Mwesigwa, amethibitisha kwamba ofisi yake haina mamlaka ya kutoa kibali chochote maalum cha kumpeleka Okwi kuichezea Simba ambapo kwa sasa bado wanamtambua mchezaji huyo kuwa ni mali ya Yanga“Kwa sasa hatuwezi kuingia ndani sana juu ya mahusiano ya pande hizo mbili wakati ukifika tutakutana na kujadili hilo, lakini kuhusu hicho kibali kinachosemwa tumekitoa, hatuna utaratibu wa namna hiyo wa kutoa vibali kiholela kila jambo lina ngazi yake,”alisema Mwesigwa akimaanisha kwamba hawajaruhusu wala kutoa muongozo wa Okwi kwenda Simba.
Mwanasheria wa Okwi
Wakala na Mwanasheria wa mshambuliaji huyo Edgar Aggaba ametamka kwamba sasa ataiburuza Yanga Fifa. Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Kampala, Aggaba akiwa na hasira alisema Yanga wanachezea taaluma yake pamoja na uzoefu wake katika kesi ngumu kutokana na kitendo cha kumfungulia kesi TFF.
“Sijajua hawa viongozi wa Yanga wanafanyaje kazi, nafikiri hawana mshauri mzuri anayejua kanuni, wanawezaje kwanza kunishtaki mimi TFF? Hao TFF wanaweza kunifanya nini mimi lakini pia kosa langu liko wapi?,”alihoji Aggaba.
“Wanasema mimi nilitaka kumuuza Emmanuel (Okwi), najua kwamba kweli ile klabu ya Misri ilimfuata Okwi lakini Okwi hakuongea nao aliwaambia wakazungumze na Yanga sasa kosa lake lipo wapi hapo sasa nataka kuwaonyesha kuwa najua sheria zaidi yao kwa kuanzia nitaanza na kuwadai fedha na baada ya hapo nawapeleka Fifa.
“Emmanuel (Okwi) hajanishirikisha kwamba anajiunga na Simba, sasa kwa kitendo chao cha kunifungulia mashtaka nataka tukabishane Fifa kikanuni na kwa kisheria tuone nani yupo sahihi, nilidhani wangekuwa wastaraabu kwa kunieleza malalamiko yao kuhusu huyo mchezaji lakini wao wanajifanya wajuaji.
”CREDIT:MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment